Zingatio: Kidogo Kidogo..... Hujaza Kibaba

 

Zingatio: Kidogo Kidogo….Hujaza Kibaba

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Akili za wanaadamu maisha zinakubali mazingira na ni rahisi kufuata yale yanayoona mbele yake. Kwake si kazi ngumu kufuata kile nafsi yake inachotaka. Lakini, daima na daima daaimah wa dawaam nafsi imeshuhudiwa kuwa ni dhaifu pale inapoendekezwa.

 

Lengo la Uislamu ni kuja kumtofautisha mwanaadamu na mnyama kwa kumuwekea kanuni madhubuti na malengo ya kuishi kwake hapa duniani. Tunapokosa kufuata kanuni hizo tunakuwa kuliko mnyama: 

ثُمَّ رَدَدْنَاهُ أَسْفَلَ سَافِلِينَ ﴿٥﴾

Kisha Tukamrudisha chini kabisa ya walio chini. [At- Tiyn: 5]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) ndio vigezo bora kwetu. Inatakikana wazee kuwasimulia watoto wao angalau dakika 15 kwa siku kuhusu maisha ya Swahaba. Mtoto ni rahisi kukamata na kupenda kuiga kuanzia umri wa miaka miwili. Usisubiri kumsimulia akifikia umri wa miaka 13, utaumia!

 

Kinyume na hayo ya kufuata Swahaba ni kuwawekea vijana redio, TV, DVD na kadhalika zisizokuwa na usimamizi madhubuti. Na wazee wengine huwawekea makusudi ili vijana wao wasikilize muziki na wapate kuwaiga hao wanaoitwa wasanii.

 

Bongo/Zenji fleva, taarabu na miziki mengineyo ya Kiswahili ni miongoni mwa chimbuko baya lilionea Afrika Mashariki. Si vitu vya kujivunia kwa Waislamu, wala kushiriki kwa kusikiliza, wala kuwaiga hao wasanii. Wasanii hao hushindanishwa kwa kupewa udhamini au tunuku. Na kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Watu katika Ummah wangu watakunywa pombe wakiipa jina jengine lisilokuwa hilo, miziki itapigwa kwa ajili yao na watakuweko waimbaji wanawake. Allaah Atawadidimiza ardhini na Atawageuza wawe nyani na nguruwe”. [Ibn Maajah na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Sahiyh]

 

Bila ya kusahau kuna mashindano ya kumuweka mtu ndani ya jumba akipumbazwa kwa kupewa maagizo yasiyo na maana huku akimulikwa mpaka sehemu za faragha.

 

Picha na maneno yanayotoka humo si mengine ila kuwaingiza vijana kwenye uzinifu, pombe pamoja na kuziteka akili zao kushughulishwa sana na kutafuta mali ili wawe na maisha ya kifakhari yenye kuchupa mipaka. Yote hayo ni ndoto, kwani ni wachache wenye kuyafikia.

 

Tunashuhudia nyimbo (miongoni mwa maelfu) ikiwa na maneno machafu machafu ya kuhamasisha zinaa, tamaa za dunia na utovu wa maadili.

  

Wazee, vijana na wanawake wa Kiislamu ni vyema wakawa wanazingatia kwamba tulipo sasa ni hatari, na tunapoendea ni kubaya mno zaidi. Kwani, adui wa leo haji kwa panga wala jiwe. Anakuja kwa njia za pole pole zenye anasa kama hizi ambazo zinahitaji kupigwa vita ndani ya majumba yetu.

 

Kuna kiongozi mmoja aliwahi kumpa pongezi mshindi aliyekwenda kwenye utwaaghuti wa Big Brother kwa kusema kuwa Watanzania wana malezi mazuri na hayo ndio maadili mema. Matokeo yake ni hayo hayo yanayozungumzwa na viongozi wetu: Elimu imeshuka, wizi umekithiri, ubakaji umeongezeka, ukimwi unaua na kadhalika

Tuzungumze Kiislam, tule, Kiislam, tusikilize Kiislam, tutembee Kiislam, urafiki tujenge Kiislam, hadi kulala tulale Kiislam… kwa kujua hayo, tufuatilize Zingatio lijalo In shaa Allaah.

  

Mzazi anayetusi asimchape mtoto kwa kutusi kwani huenda ikawa hayo matusi yalianza kutoka kwake mzazi na mtoto akalihifadhi ndani ya ubongo wake, akamalizia kwa kulitamka. Bali, ajirekebishe yeye binafsi mzazi na baadaye afuatie kumuwekea vikwazo mtoto.

 

Kuna haja ya kubadili nyumba zetu kimaadili.

 

Tuanze kuishi Kiislam.

 

Share