Maulidi: Kuna Ushahidi Aliyerudi Hajj Asomewe Maulidi?

 

Kuna Ushahidi Aliyerudi Hajj Asomewe Maulidi

 

Alhidaaya.com

Swali:

 

Namshukuru Allaah Subhana Wataala kunipa fersa hii ya kuuliza.Jamaa yangu amerudi Hijja hivi watu wa nyumbani wanataka kumsomea Maulidi jee inafaa? Kama haifai kuna Adhabu kwa kufanya Maulidi ua kumsomea dua huyo hujaj,na imetokea wapi?kuna uthibitisho gani  katika Qur an na hadithi? Nitafurahi kwa kupata jibu lenu kwani bado tupo nyuma.
 

 

Jibu:
 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika Maulidi ni dhahiri kabisa kwamba ni bid'ah (uzushi) uliozushwa miaka baina 400 na 600 baada ya kufariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kundi potofu la Mashia Ismailiya (Aga Khan) walipokuwa wakitawala Misr. Kisha yakasambaa na kuenea kufikia pande mbali mbali za dunia hadi kufika kwetu Afrika Mashariki.
 
 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ametuonya mara nyingi kujiepusha na uzushi na alikuwa akitanguliza khutba zake kwa kutoa maonyo hayo:

 

((إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم  وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار))  أخرجه مسلم في صحيحه 

((Maneno bora  ni kitabu cha Allah (Qur-aan) na uongofu bora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi)  na kila bid'ah ni motoni)) [Muslim katika Swahiyh yake]

 
Maudhui haya yameelezewa kwa upana ndani ya tovuti, ni vizuri kuyasoma ili Muislamu atambue ubaya wake  na aweze kuusalimisha Uislamu wake kwani hakika uzushi ni ufisadi mkuu wa Dini yetu ya Kiislamu. Hivyo bila ya shaka mwenye kutaka kubakia katika usalama wa Dini yake ni lazima ajifunze kujua yepi ni ya uzushi na yepi ni ya Sunnah ili asalimike na abakie katika radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). 
 
 
Juu ya hivyo, mwenye kutenda uzushi hana ila kupoteza muda wake kwa kutenda amali ambazo hazina thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na zaidi ni kutumbukia katika madhambi na kujitayarishia makazi mabaya. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika.  [Al-Furqaan: 23]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
 

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate makala muhimu kuhusu mas-ala haya ya Maulidi

Sababu 35 Muislam Asisherehekee Maulid

Mawlid – Mtazamo Wa Kisheria
 
Hoja Za Wanaosherehekea Maulid Na Majibu Yake
 
 

Muislamu anayerudi kutoka Hajj hahitaji kufanyiwa lolote, kwani ikiwa ametimiza Hijjah yake basi atakuwa amerudi akiwa amefutiwa dhambi zake zote kwa dalili:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: "سَمِعْتُ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((مَنْ حَجَّ لِلَّهِ فَلَمْ يَرْفُثْ وَلَمْ يَفْسُقْ رَجَعَ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أُمُّهُ)) متفق عليه

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  kasema: “Nilimsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema: ((Atakayefanya Hajj, kisha asiseme maneno machafu wala asitende vitendo vichafu atarudi akiwa kama siku aliyozaliwa na mama yake)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Watu wake wanaweza kumuombea du'aa kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amthibitishie Iymaan yake, Azidi kumuongoza na Amtakabalie hijjah yake. Kumuombea huko kuwe ni kila mtu binafsi katika Swalaah zake au nyakati nyinginezo na sio kwa kukusanyika pamoja kumuombea kwani hilo pia ni jambo   lisilofaa na kukubalika katika Dini yetu kwa vile hatukupata mafunzo hayo katika Sunnah. Na juu ya hivyo kukusanyika watu kwa ajili ya kuwaombea au kuwapongeza mahujaji ni jambo linalopeleka katika Riyaa (kujionyesha) na hivyo huenda wakapoteza amali zao na wakakosa thawabu zake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share