Mwenye Kuhudumia Kituo Cha Mafuta (Petrol Station) Anafaa Kumjazia Mafuta Mteja Aliyebeba Ulevi?

 

SWALI:

Ama ndugu zangu nina swali moja linani tatiza Mfano mimi nina petrol station au jaalia wewe ndio mwenye hiyo petrol station au ni ya ndugu yako na kuna siku na wewe huwa na kawaida ya kumsaidia. Sasa linakuja gari la tanzania breweries limebeba kreti za bia linahitaji huduma ya mafuta kama kama vinavyofanya vyombo vingine vya moto vikija ktk vituo vya mafuta je unaalihudumia au mtihani au ufanye nini?

Nategemea fatawa nzuri kutoka kwenu wabillah tawfiq alkm



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu biashara. Bila shaka inaeleweka kuwa biashara ina nidhamu zake katika sheria ya Kiislamu. Haifai kwa Muislamu kuuza kitu kilicho haramu wala kusaidia katika uovu. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu” (5: 2).

Kwa hiyo unapolihudumikia gari lenye kuuza pombe utakuwa umeshiriki katika kueneza ulevi kwa watu na sehemu tofauti. Hivyo haitakuwa sawa kwako kuliuzia mafuta gari hilo. Lakini ikiwa gari lenyewe limebeba pombe bila wewe kujua na halina chapa au nembo yoyote ya kukujulisha wewe kuwa ni la kampuni ya pombe n.k. utawauzia na hutakuwa na madhambi yoyote.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share