Inafaa Kufanya Kazi Kunakouzwa Nguruwe Na Pombe Na Hawezi Kuswali Anakidhi Swalah Zote

SWALI:

 

Mimi niko nje ya Nchi yangu, pia nafanyakazi katika Duka, na kazi yangu ni msafishaji Au (CLEANER) katika duka hilo kunauzwa ulevi, na nyama za nguruwe.

 

Wakati wowote ule huwa huwajibika kusafisha panapofunjika chupa ya ulavi, au kuondosha mifuko ya takataka za Bucha ambapo panauzwa hio nyama ya nguruwe na hunibidi kutamata na kusafisha mara kwa mara. Pia choo havina maji hutumia karatasi tu.

 

Pia hakuna mahala hata pakuweza kusali kwa wakati wote unapokuwa kazini.

 

SUALA

1. Sala zangu zote huzisali baada ya saa za kazi jee inafaa kusali hivyo?

2. Kwa sababu baadhi ya wakati huwezekana kukamata mifuko ndani yake mlikuwa na nyama ya nguruwe, jee nikijitoharisha inatosha na kusali? Naomba unifafanulie masuala yangu kwa ufasaha zaidi


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kufanya kazi katika duka linalouza vya haramu. Uislamu ni njia kamili ya maisha hakuna lolote isipokuwa tumepatiwa muongozo ili tusiwe ni wenye kusumbuka kwa lolote.

 

Suala lako la kwanza, inapaswa ifahamike kwa kila mmoja wetu kuwa Swalah kwa Muislamu imewekewa wakati maalumu. Haifai kwa Muislamu kuitoa katika wakati wake isipokuwa kwa sababu maalumu zinazokubalika katika sheria. Nazo ni:

 

  1. Mtoto mdogo kabla ya kubaleghe, akianza kubaleghe udhuru huo unaondoka.

  2. Kusahau. Pindi unapokumbuka unahitajika uswali wakati huo huo.

  3. Kulala mpaka wakati ukapita, unapoamka tu unafaa uswali.

  4. Usingizi, ukiwa umepitiwa utaswali mara tu uamkapo.

  5. Mwanamke katika damu ya hedhi na nifasi hafai kabisa kuswali. Anaanza kuswali tu anapotwaharika.

 

Mbali na sababu hizo Muislamu hafai kabisa kuchelewesha Swalah mpaka wakati wake ukatoka. Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Kwa hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa wakati makhsusi" (4: 103).

Kuitoa katika wakati wake ni kujitafutia adhabu kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Lakini wakaandamia baada yao watoto wabaya. Wakapuuza Swalah na wakafuata matamanio mabya; kwa hivyo watakutana na adhabu kali" (19: 59).

Na Anasema tena aliyetukuka: "Basi adhabu itawathubutikia wanaoswali. Ambao wanapuuza Swalah zao" (107: 4 – 5).

 

Ama kuhifadhi wakati wa Swalah inamyakinishia mtu kuingia Peponi (tazama Surah 70: 23 na 34).

 

Hata lau kazi yenyewe unayoifanya ingekuwa ni halali isingekuruhusu wewe uache kuswali Swalah kwa wakati wake, achilia mbali hiyo kazi ya haramu unayoifanya.

 

Kila Muislamu, hata yule wa kawaida kabisa anafahamu kuwa pombe na nguruwe ni haramu. Ule uharamu wa kunywa na kula unafanya kuuza au kufanya kazi katika maduka yenye kuuza ni haramu vilevile. Huu ni ule msingi wa kutosaidia katika haramu. Hivyo ndugu yetu, unatakiwa utafute njia na kazi nyingine kwani hiyo haikufai Kiislamu. Na pindi unapoacha jambo kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah Aliyetukuka, Allaah Hatakuacha kabisa bali Atakupatia badala iliyo njema zaidi.

 

Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Ninafanya Kazi Ya Kuchinja Nguruwe, Je, Halali?

 

Anafanya Kazi Inayohusu Ubebaji Wa Maboksi Yenye Ulevi

 

Kufanya Kazi Katika Duka Au Sehemu Inayouzwa Nyama Ya Nguruwe

 

Swalah Zote Zinanipita Ni Sawa Kuzikidhi?

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie kupata njia na kazi nyengine ya halali ya kukuwezesha kujikimu kimaisha.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share