Anapata Matatizo Na Meneja Wake Kazini Nchi Za Kigeni Afanyeje?

Anapata Matatizo Na Meneja Wake Kazini Nchi Za Kigeni Afanyeje?

www.alhidaaya.com

 

  

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum swala langu leo, ilikuwa naomba kupata maoni kutoka kwenu, maoni yenyewe ni kuhusu kazi ninayofanya, mimi niko Uingereza na ndiko nnako fanya kazi, sasa basi huko kazini yuko mzungu mmoja ambae yeye ndio manager lakini ananichukia sana mimi sijui kwa nini ananifanyia madharau sana hanifanyi usawa kama anavyo wafanyia wengine, na mengineo baya, sasa naomba maoni yenu nifanye nini ahsantum.     

 

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika ni kuwa kazi nyingi hapa duniani zina matatizo na mitihani. Wewe si wa kwanza kupata matatizo hayo wala hutokuwa wa mwisho. Na ni hakika wapo Wazungu ambao ni wazuri kwa muamala wao na wafanyakazi walio chini yao na wengine ni waovu na wabaguzi.

 

Nasaha ambazo tunaweza kukupatia ni kama zifuatazo:

 

1-Huenda Mzungu huyo ana nadhariya zake kukuhusu wewe. Ima hajakuelewa vyema au anaona hutekelezi kazi yako inavyohitajika, au unazembea au sababu nyingine yoyote. Hivyo, unatakiwa uwe na ujasiri wa kuweka miadi naye ili umueleze unayohisi akilini mwako. Kwa kumuelezea kinaganaga huenda yakajitokeza mengi katika hayo mazungumzo. Huenda akakuelezea anayoona ni makosa kwa upande wako au kukiri kuwa kweli amefanya makosa hivyo ajirekebishe.

 

2-Mripoti kwa Meneja mkuu, au waone Jumuiya ya Wafanyakazi kama mnayo hapo kazini waweze kuzungumza naye ili akupe haki zako kama wafanyakazi wengine.

 

 

3-Kuomba Du’aa katika kila nyakati ambazo du’aa inakubaliwa kama unapoamka usiku kwa ajili ya Tahajjud, unapokuwa umefunga, baina ya Adhaan na Iqaamah na nyakati nyingine. Muombe Allaah ('Azza wa Jalla)   Akutengenezee mambo yako na Akuepushe na shari hizo.

 

 

4-Huenda kazi hiyo ikawa haina kheri nawe, kwako binafsi au kwa Dini yako kwa zote mbili. Hivyo, kitu ambacho unaweza au unatakiwa kufanya ni kutafuta kazi sehemu nyingine. Pindi tu utakapopata, basi aacha hiyo uende kufanya huko kwengine, lakini kabla ya hapo Swali Swalaah ya Istikhaarah utake ushauri kutoka kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa jambo ambalo linafaa wewe ufanye katika tatizo hilo ulilo nalo.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo yake:

 

Swalaah Ya Istikhaarah Iswaliwe Kwa Ajili Ya Nini Na Ipi Du'aa Yake?

 

Na timiza fadhi zako ipasavyo kisha mdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Istighfaar (kuomba maghfirah), kuswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Adhkaar nyenginezo zilizothibiti.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share