Vijitabu Vya Surat Yaasiyn Na Surah Maalum Za Kusomwa Na Yaasiyn, Vinafaa Kuvitumia?
Vijitabu Vya Suwrah Yaasiyn Na Suwrah
Maalum Za Kusomwa Na Yaasiyn, Vinafaa Kuvitumia
SWALI:
ningependa kuuliza swali, kuna vitabu vimetoka navyo ni vitabu ambavyo kuna sura yassin na kila ukifika kwenye mubbin kuna sura nyengine ndogo uzisome mara tatu kisha waendelea na sura yassin .,na vyengine ni kila ukifika mubbin waanza tena kusoma sura yassin mwanzo, je vitabu hivyi ni sawa kuvisoma wa jazakum Allaah bil kher
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako hilo.
Jambo hilo halipo kabisa katika mafunzo ya dini yetu. Tutambue kuwa kila jambo linalohusu ibada katika dini linahitaji dalili kutoka Qur-aan au Sunnah, ikiwa hazikupatikana dalili basi huwa ni jambo la kuzushwa. Na kutekeleza ibada za kuzushwa huwa ni kumpotezea Muislamu muda wake kwa kufanya jambo ambalo halina thamani na pia kumuingiza katika dhambi kwani tumeonywa kuwa kila uzushi ni upotofu na kila upotofu ni kujitayarishia makazi ya motoni.
Mambo mengi yamezushwa yanayohusu kusoma Suwrah kadhaa, mfano kuna walioweka du’aa khaswa ya Suwrah hii ya Yaasiyn ambayo hakuna dalili yake. Suwrah nyinginezo ambazo zimewewekea du’aa khaswa au zinazosemwa kuwa zisomwe kwa wakati fulani kama Al-Waaqi’ah, Ad-Dukhaan, Al-An’aam, Al-Hashr n.k. zote hizo hakuna dalili inayothibitisha.
Watu huacha kusoma Qur-aan tokea mwanzo yaani tokea Al-Faatihah – Al-Baqarah hadi kukhitimisha msahafu kwa kufikia Suwrah An-Naas ambavyo nidvyo inavyopaswa na ilivyoamrishwa. Lakini huacha kufanya hivyo na kusoma Suwrah moja pekee au Suwrah fulani kila siku hizo hizo. Kufanya hivi ni kudharau Suwrah nyingine zote jambo ambalo halipasi.
Khaswa Suwrah hii ya Yaasiyn ndio watu wengie wameipa umuhimu mkubwa sana na hali fadhila zote zinazotajwa kuhusiana na Suwrah hii zimekuja katika Hadiyth za kuzuliwa na dhaifu. Hivyo fahamu kuwa hakuna Suwrah nyingine zinazosomwa kati kati yake.
Kwa maelezo zaidi soma Swali na Jibu lifuatalo:
Surat Yaasiyn Na Al-An'aam Zina Fadhila?
Tunakushauri ndugu yetu usipoteze wakati wako kwa kuchagua Suwrah Fulani tu kila wakati na kuisoma hiyo hiyo na ukaacha zingine kama vile hazina maana wala umuhimu. Jitahidi sana kusoma Qur-aan nzima na kusoma kila Suwrah kila unapopata wasaa. Kufanya hivyo utakuwa unapata fadhila kubwa na thawabu, na pia utakuwa umeikirimu na kuipa heshima istahikiyo Qur-aan.
Na Allaah Anajua zaidi