Amri Ya Kufuga Ndevu
SWALI:
Ushahidi wa kufuga ndevu kwa mwanamume na faida zake.
Shukran.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako. Amri ya kufuga ndevu iko wazi kabisa katika sheria yetu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameagiza:
"Nendeni kinyume na washirikina, fugeni ndevu na mpunguze masharubu" (al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy).
Hadiyth kuhusu kufuga ndevu na kutonyoa zipo nyingi sana katika vitabu vya Hadiyth mbali mbali za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hadiyth iliyopo juu imebainisha sababu ya kufuga ndevu nayo ni kuwa kinyume na mushirikina na kutotafautiana nao kwani wao walikuwa wakinyoa na wanaendelea kunyoa.
Kunyoa pia kunakwenda kinyume na maumbile ya mwanamme na kujinasibisha na wanawake, kwani ndevu ni ukamilifu wa wanaume. Kunyoa ni kuwaiga maadui zetu wa Dini na watawala wa nchi za Kinasara na Mayahudi. Huku ni kwenda kinyume na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:
"Mwenye kujishabihisha na watu huwa ni mmoja wao" (Abu Daawuud).
Pia hakuna katika watangu wema walioacha wajibu huo.
Faida tunayopata ni kuwa katika kufuga ndevu huwa tunafuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hivyo kupata thawabu kwa kufanya hivyo.
Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Kufuga Ndevu Ni Sunnah Au Wajib?
Na Allaah Anajua zaidi