Kusoma Uradi Kwa Pamoja Kila Mwezi Kwa Kukusanyika Inafaa?

 

Kusoma Uradi Kwa Pamoja Kila Mwezi Kwa Kukusanyika Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalaam alaykum

Sisi huwa tunakusanyika pamoja kwa kila mwezi mara moja kwa ajili ya kuswali, kuleta adhkar na kuomba dua ya pamoja. Dua ambazo huwa tunatumia ni zile zilizomo kwenye Quran na mapokezi sahihi ya Nabiy (s.w). Je kufanya hivi inakubalika katika uislam?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ‘ibaadah na ‘ibaadah inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Swahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

 

Tumekuwa tukisema mara nyingi kuwa katika Uislamu kila kitu ambacho kinamridhisha Allaah (‘Azza wa Jalla)    ni 'Ibaadah pamoja na kufuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).    Hakuna utata kuhusu kuswali Swalaah ya Sunnah kwa Jama'ah na kufanya I’tikaaf katika Msikiti kwa siku moja.

 

 

Hata hivyo, haijakuwa kukutana huko ni fursa kwenu nyinyi kufanya mengine kama kuleta Adhkaar na du'aa kwa pamoja. Hilo halijapokewa katika Qur-aan, Sunnah wala Wema Waliotangulia (Salaf Swaalih). Ikiwa ni Adhkaar za asubuhi au usiku kila mmoja anapaswa awe ni mwenye kuleta pekee yake isipokuwa ikiwa ni kufunzwa ili aweze kuzisoma yeye peke yake baada ya hapo.

 

 

AlhamduliLlaah, siku hizi suala hilo limekuwa sahali kupatikana vijitabu vidogo kama vile Hiswnul Muslim, ambacho kina du'aa takriban zote ambazo tunazihitajia. Pia kuna kitabu kinachoitwa “Hiswnul-Muumin”. Hizi Adhkaar za pamoja ndio zimeleta matatizo mpaka watu wakawa wanalichezea jina la Allaah (‘Azza wa Jalla)  kwa kufanya katika kiza na kuwa ni wenye kutoa maneno hata yasioeleweka au kufanya Adhkaar kwa kukohoa.

 

 

Na du'aa nayo ni hivyo hivyo mbali na kuwa kuna wakati ambao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefundisha kuwa iletwe kwa sauti kama wakati wa kuomba mvua, Swalaah ya kupatwa kwa jua au mwezi. Ama wakati mwengine inabidi kila mmoja wetu alete kivyake kwani kila mmoja wetu ana tatizo tofauti na mwenziwe. Katika hili utapata Maimaam kwa kutojua au kwa kujua huwa wanajiombea wenyewe na Maamuma wanaitikia “Aamiyn”.

 

 

Tunapata makatazo hayo na madhara yake katika usimulizi ufuatao:

 

Kutoka kwa ‘Amru bin Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Tulikuwa tumeketi mlangoni mwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd kabla ya Swalaah ya Alfajiri, akatoka nje. Tukaenda naye Msikitini. Kisha Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akatujia na kusema: “Je, Abuu ‘Abdir-Rahmaan ameshakuja kwenu?” Tukasema: “Hapana!” Akaketi hadi akatoka nje na alipotoka nje tukasimama. Abuu Muwsaa akamwambia: “Ee Abaa ‘Abdir-Rahmaan! Sasa hivi nimeona jambo Msikitini sijapatapo kuliona kabla, lakini sidhanii baya ila ni jambo jema”. Akasema: “Jambo gani?” Akasema. “Ukiendelea kuishi utaliona”. Akasema: “Nimeona Msikitini watu wameketi kwa mkusanyiko wa duara wakisubiri Swalaah. Katika kila duara alikuweko mtu na mikononi mwao mna changarawe. Mmoja wao akisema: “Semeni Allaahu Akbar mara mia!” nao wakisema “Allaahu Akbar!” mara mia. Kisha husema: “Semeni laa ilaaha illa-Allaah mara mia”! Nao husema “laa ilaaha illa-Allaah!” mara mia. Kisha husema: “Semeni Subhaana-Allaah mara mia!” Nao husema “Subhaana-Allaah!” mara mia. Akasema: “Je umewaambia nini?” Nikasema: “Sikusema lolote, nilikuwa nasubiri nione utaonaje na nikisubiri amri yako”. Akasema: “Kwa nini usiwaambie wahesabu vitendo vyao viovu na kuwahakikishia kwamba vitendo vyao vyema havitopotezwa?”

 

 

Kisha akasogea nasi tukaenda hadi alipofikia moja kati ya maduara hayo akasimama na kusema: “Mnafanya nini?” Wakasema. “Ee Abaa ‘Abdir-Rahmaan, hivi ni vijiwe tunavyohesabia takbiyr, tahliyl na tasbiyh”. Akasema: “Hesabuni vitendo vyenu viovu, kwani nakuhakikisheni kwamba vitendo vyenu vyema havitopotea hata kimoja! Ole wenu Ee Ummah wa Muhammad! Ni kwa haraka gani mnakimbilia kwenye uharibifu! Hawa ni Maswahaba wa Nabiy wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao wameenea. Hizi ndizo nguo zake ambazo bado hazijachakaa, na bakuli lake ambalo halijavunjika! Naapa kwa Yule Ambaye roho yangu ipo mikononi Mwake! Aidha mpo kwenye dini iliyoongoka zaidi kuliko Dini ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ama mnafungua milango ya upotofu!”

 

 

Wakasema: “Ee Abaa ‘Abdir-Rahmaan, hatukukusudia lolote ila khayr tu”. Akasema: “Wangapi waliokusudia khayr hawakuzipata?” Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia: ((Watu wataisoma Qur-aan, lakini haitovuka zaidi ya koo zao)) “Naapa kwa Allaah! Mimi sijui, lakini pengine mengi kati ya hayo yanatoka kwenu!” Baadaye akaondoka. ‘Amr bin Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Tumewaona wengi kati ya watu hao wakipigana dhidi yetu katika siku ya Nahrawaan, wakiwa pamoja na Khawaarij [Sunan Ad-Darimy 206 – Ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (5/11)]

 

 

Kila mmoja wetu ajifunze katika Adhkaar na du'aa ambazo anaweza kuleta katika hali ya upweke. Tukumbuke kuwa Allaah (‘Azza wa Jalla)    si kiziwi bali Anasikia hata minong'ono yetu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾

Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka. [Al-A’raaf: 55]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta’aala):

 

 وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta’aala):

  وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

  Na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo. [Qaaf: 16]

 

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta’aala):

 

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾

Nasi Tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni. [Al-Waaqi’ah: 85]

 

 

 

Hizi ni sifa za Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa), hivyo tumuombe Yeye kwa unyenyekevu na taadhima ya hali ya juu, na si kumuomba mpaka watu wengine wasikie na mikusanyiko ambayo huenda ikaingia riyaa (kujionyesha).

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share