Wanawake Hawaogi Josho Kwa Masiku Kuhofu Nywele Zisiharibike

SWALI

 

Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh 

 

Namuomba Allah awalipe malipo mema katika kazi yenu kubwa mnayofana kutujibia maswali yetu. Mmetufunza sana hasa sisi wanawake ambao tuna matatizo mengi. Mimi ni mwanachama wa Alhidaaya na hufaidika na kuwanufaisha wenzangu kwa maswali yenu na makala na wengi wanarudi kushukuru na kupata uongofu.

 

Kwa vile nafanya kazi na wanawake wengi nimetambua yafuatayo ambayo yamenitia shaka. Hivo nakuombeni mashekhe wetu mtujibu haya yanayotendeka katika jamii yetu nayo ni: Baadhi ya wanawake wanapokwenda kwa hair-dresser kusuka au kuchana nywele kwa staili ima kwa ajili ya harusi au kujipamba tu – huwa hawataki kuharibu nywele zao kuziosha hivyo wanakaa masiku hawaoshi – kwa sababu huona hasara kupoteza hela kwenda kwa hair dresser kila mara. Hali hii huwafanya:

1- Wakatae kulala na waume zao kufanya kitendo cha ndoa kwa hofu ya kuosha nywele, na waume hupiga huwa hawapati haki zao.

2- Au huwa hawaogi janaba wanabakia na nywele zao zisiharibike.

3- Wengine hawaogi josho la hedhi au janaba wanadai kwamba nywele hazitokauka asubuhi akiosha na atachelewa kwenda kazini.

Hali hiyo huwafanya hata wasiweze kusali kwa siku kadha.

 

Tunaomba majibu ya ufafanuzi ili tuwafahmishe dada zetu mtindo wao huo kama unafaa au haufai. Mungu awape nguvu za kujibu maswali yetu na awalipe.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako muhimu kuhusu masuala yako mchanganyiko ya mambo ya kike. Mwanzo ni muhimu sana wanawake wafahamu kuwa ni muhimu wawapatie malezi mema binti zao hasa wanapokaribia kubaleghe mas-ala ya kujipamba kihalali. Kwa sababu ya kuiga mataifa mengine ambayo yanataka kutuharibia maadili na tabia zetu tumeingia katika maafa mengi sana. Kujipamba mwanamke mwenyewe ni fani ambayo kwa sasa imesahaulika sana na wanawake wetu hivyo kuwafanya watumie pesa nyingi kwenda kwa hair-dresser.

 

Tufahamu kuwa ni madhambi makubwa kwa mwanamke kumkatalia mumewe anapomtaka bila udhuru wa kisheria kama ugonjwa na mengineo. Sababu ya kusuka nywele haimo katika nyudhuru hizo. Tufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia na kutahadharisha kuwa mwanamke yeyote mwenye kumkatalia mumewe tendo la ndoa basi hulaaniwa na Malaika na viumbe vyengine. Na akatuambia tena mume anapomtaka mkewe inatakiwa amtimizie haja yake hata kama alikuwa kwenye tanuri.

 

Ni ajabu kwa wanawake kujipamba tu wanapotaka kwenda harusini na kazini lakini hawawapambii waume zao. Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaah 'anhuma) alikuwa anajipambia kwa ajili ya mkewe kama alivyokuwa mkewe akijipamba kwa ajili ya mumewe. Kukataa huko hakufai kwa mwanamke hivyo kutomlazimu yeye kwenda saloon kununua laana kwa pesa zake.

 

Wanawake wengi pia hukosea kwa kuongeza vipande vya nywele bandia au za kweli juu ya nywele zao na hiyo ni haramu kabisa. Zipo Hadiyth nyingi kuhusu hilo. Kwa Hadiyth mbalimbali tafadhali tazama Riyaadhw asw-Swaalihiyn, mlango wa 296. Au ingia kwenye viungo vifuatavyo kwa faida zaidi:

 

Kuweka Madawa Ya Nywele Na Kuvaa Nywele Za Bandia

Mwanamke Kupaka Dawa Ya Nywele

Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nywele Turkey Kwa Sababu Ya Kukatazwa Hijaab

Nini Hukumu Ya Nywele Za Bandia?

Kusuka Nywele Na Kuchanganya Na Nyuzi Inafaa?

Hukmu Ya Mtu Kuswali Na Kaweka Nywele Za Bandia

 

Ama kutokuoga kwa ajili ya janaba au hedhi pia ni makosa kwani hiyo inaonyesha utovu wa maadli na kuwa umezifanya nywele zako kuwa ni mungu wako. Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Je, umemuona yule aliyefanya matamanio yake (kila anachokipenda) kuwa Mungu wake?" (25: 43).

Na ikiwa ni hivyo basi watu hao watakuwa mahali pabaya sana. Pili, mwanamke anayefanya hivyo na kisha asiweze kuswali, hali hiyo inamuweka pabaya zaidi kwani Swalah ndio tofauti baina ya Muislamu na kafiri na ndiyo amali ya kwanza itakayotazamwa kesho Akhera. Ikiwa mwanamke ameacha siku nyingi bila udhuru wa kisheria atakuwa wapi. Ni hakika kuwa tunanunua moto kwa pesa zetu.

 

Inafaa dada yetu uwashauri wanawake hao wasiwe ni wenye kufanya hivyo na Allaah Aliyetukuka Atakupa tawfiki katika juhudi hizo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share