Jimai: Kuzini Ramadhwaan (Usiku) Na Kutofunga Mchana Wake; Na Afanyeje Hata Asamehewe Na Allaah

Assalam aleykum

ndungu waislam wa nakala hii shukrani za ngu kwa mungu natoa kwa kuwapa nafasi na uzima kutufundisha sisi kwa kutumia teknologia hii ya kisasa mungu awape yanayo wastahali. "Amin"

 Swali langu ni kwa muislam aleye zinii katika mwezi mtukufu wa ramadhani na kuamka siku ya pili yake akiwa haja funga naomba uniambie hukumu ya mtu huyu na anatakiwa afanye nini kama anataka apate msaama wa mola wake,

Jazzaka Allahau kheri,  Assalam aleykum

 


 Jibu

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Asli Qur aan imetuhadharisha na kuikaribia zinaa kwa ubaya wake kama inavyosema katika kauli yake Aliyetukuka:

 

 

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.”  Al-Israa aya ya 32.

 

 

Hivyo basi Muislam amehadharishwa kwa kushauriwa kuwa asiukaribie uzinzi, kwa kuziingilia sababu zinazo pelekea uzinzi. Jambo hilo ni jambo la aibu na uovu usio fichikana, na hapana njia mbovu kama hiyo.  Hivyo basi kuikaribia zinaa tu ni jambo lisilo takiwa, sasa kama umeiingia na kuifikia zinaa ni jambo ovu kabisa kwani amehadharishwa kuikaribia kwa kufanya cho chote kitachopelekea kufikiria kulikaribia tendo la zinaa; kama kukaa peke yao mwanamume na mwanamke wasio kuwa mahaarim, kuangalia magazeti au filamu zenye wanawake waliojiweka uchi, kutazama wanawake, na kadhalika.

 

 

Na imethibiti kutoka kwa al Habiybi Musttafa Swalla Llaahu ‘alayhi wa’alaa Alihi Wasallam kuwa amesema kumwambia Ibn Mas’uud alipomuuliza ni dhambi gani kubwa –a’dhiym- mbele ya Allaah? Al-Habiybi Musttafa Swalla Llaahu ‘alayhi wa’alaa Alihi Wasallam akamjibu kwa kusema:

 

 

Kumuwekea Allaah mshirika hali ya kuwa Yeye ndie Aliye kuumba; Ibn Mas’uud akauliza tena kisha dhambi gani baada ya hilo? Akamjibu kwa kusema: “Kumuua mtoto wako kwa kuchelea kulishwa pamoja nawe” Ibn Mas’uud akauliza tena kasha dhambi gani baada ya hilo? Akamjibu kwa kusema:Kuzini na mke wa jirani yakoImepokelewa na Bukhaar na Muslim.

 

Ndio Allaah akashusha:

 

 

Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara, al Furqaan aya ya 68.

 

 

Pia ni vyema tuelewa kuwa kila muislamu anapozini wakati wa hili tendo Allaah humvua imaan kama mtu anavyovua kanzu/nguo yake kama ilivyothibiti katika hadiythi za Habiybi Musttafa Swalla Llaahu ‘alayhi wa’alaa Alihi Wasallam.

 

 

Mzinifu aliyezini iwe katika Ramadhaan au mwezi mwengine hukumu yake ni kama ilivyothibiti katika Qur an kama hakuwahi kuoa au kuolewa; Qur aan inasema:

 

 

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini”  An Nuur aya ya 2

 

 

Ama akiwa mmoja wao au wote wawili wamewahi kuwa wanandoa japo mara moja katika umri wao basi hukumu yao ni kupigwa mawe mpaka kufa kama ilivyothibiti katika sunnah za Habiybi Musttafa Swalla Llaahu ‘alayhi wa’alaa Alihi Wasallam.

 

 

Muislamu amezinii katika mwezi wa Ramadhaan

 

 

Amezini usiku wakati anapotarajiwa kama ni muislamu kujishughulisha na Qiyaam kwa kutafuta na kutarajia radhi na remha za Mola wa Ramadhaan, lakini yeye amefadhilisha kutafuta ghadhabu za Jabbaar kwa kumuasi wakati kila mmoja anatokwa na machozi kwa kuomba atolewe katika Moto; hivyo amejichagulia amali aliyopendekezewa na kumpambia na shayattaan ndio katika walio nunua upotofu kwa uwongofu, Qiyaam cha Ramadhaan hakikuwa muhimu.

 

 

Jambo lililo muhimu hapa ni hili mtu ye yote anae zini iwe katika Ramadhaan au mwezi mwengine huwa na hali mbili:

 

 

1. Anazini kwa imaan kuwa zinaa sio haramu, kwani hakuna tofauti yo yote katika tendo zaidi ya kuwa moja linaitwa tendo la ndoa na jengine linaitwa zinaa, na yeye anazini kwa kuwa haoni tofauti bali ni katika haki yake ya kuishibisha jinsia yake na hakuna mwenye haki ya kumuingia katika hilo, huyu huwa amehalalisha alichoharamisha Allaah, na mwenye kuhalalisha Alichokiharamisha Allaah huwa amejiweka nafsi yake kuwa ni mshirika wa Allaah katika yenye kumhusu Allaah pekee nako ni kuhalalisha na kuharamisha na huyo huwa ametoka nje ya duara la Uislam na huwa mshirikina na kila ataekubaliana nae huwa anamuabudu, tunajilinda kwake al Waahidul al Ahad na kumshirikisha na tunamuomba atufishe hali ya kuwa ni waislam.

 

 

2.  Anazini huku akiwa na imaan kuwa analolifanya ni haramu na yeye ni mkosa na aasi; huyu ndie katika wenye kuvuliwa imaan wakati wa tendo la zinaa na adabu yake ndio kama ilivyothibiti na itamlazimu toba kwani imethibiti katika hadiythi ya ‘Ubadah bin As Saamit radhiya Llaahu ‘anhu kuwa Al-Habiybi Musttafa Swalla Llaahu ‘alayhi wa’alaa Alihi Wasallam baada ya kuahidiwa na Sahaba radhiya Llaahu ‘anhum hawatafanya mambo sita likiwemo zinaa; alisema:

 

 

“… Basi ye yote miongoni mwenu ataeshikamana na kutekeleza ahadi hizo basi ujira wake uko kwa Allaah; na atae fanya lolote katika hayo na akapewa adhabu inayostahiki –kupigwa mawe au mijeledi mia kwa mzinifu- basi hiyo itakuwa ndio kafara yake, na atae fanya lo lote katika hayo na Allaah akamsitiri basi itakuwa juu ya Allaah akipenda atamsamehe au akipenda atampa adhabu huko Akhera Imepokelewa na Bukhaar.

 

 

Kuamka siku ya pili yake akiwa haja funga

 

 

Jambo lililo muhimu hapa ni kama lililo tangulia kwa mzinifu; hivyo ye yote asiyefunga Ramadhaan na pia asiyeswali huwa na hali mbili:

 

 

1. Hakufunga kwa imaan kuwa funga sio wajibu sio lazima, bali ni kujitesa tu, na yeye hajafunga kwani haamini kuwa Allaah Amefaradhisha swawm kwa waja wake, huyu huwa ametoka nje ya duara la Uislam, amekufuru kwa alichoteremshiwa Al-Habiybi Musttafa Swalla Llaahu ‘alayhi wa’alaa Alihi Wasallam; hivyo basi atatakiwe atubie; akitubia na kukubali na kukiri kuwa Swawm ni wajibu na ni faradhi aliyoifaradhishwa Allaah kwake vyenginevyo akifariki na hali yake hii hatokoshwa wala watoswaliwa kama waswaliwavyo waislamu kwani yeye si muislam, na kama imani yake kuwa kula mchana wa Ramadhaan bila ya udhuru wo wote ule ni halali jambo aliloliharamisha Allaah basi huwa amejiweka nafsi yake kuwa ni mshirika wa Allaah katika yenye kumhusu Allaah pekee nako ni kuhalalisha na kuharamisha na huyo huwa ametoka nje ya duara la Uislam na huwa mshirikina na kila ataekubaliana nae huwa anamuabudu.

 

 

2.  Hakufunga tu huku akiwa na imaan kuwa analolifanya ni haramu na yeye ni mkosa na aasi; huyu aelewe kuwa hata akija kutaka kuilipa siku aliyokula bila ya udhuru wenye kukubaliwa kisharia kulipa kwake huwa haikubaliwi –kulingana na kauli iliyo sahihi zaidi katika kauli za ahlul ‘almi- kwani kila ibadah iliyowekea wakati wake maalum na mtu akakusudia kuitoa nje ya wakati wake uliopangiwa bila ya udhuru basi haitokubaliwa ibadah hiyo; hivyo itamlazimu kujuta kuleta istighfaar, kukithirisha amali njema, kukithirisha sunnah mithilli ya hiyo amali aliyoiwacha; kwani ibadah yo yote iliyopangiwa wakati wake huwa haikubaliwi kama itafanya kabla ya wakati iliyopangiwa,  basi hivyo hivyo huwa haikubaliwi kama itafanywa baada ya wakati wake bila ya kuwepo udhuru wenye kukubalika kisharia.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share