Nini Baada Ya Ramadhwaan?

 

Nini Baada Ya Ramadhwaan?

Alhidaaya.com

 

 

Tumeuaga mwezi wa Ramadhwaan, mwezi wenye Baraka na Rahmah. Tumeaga mchana wake tulipokuwa katika subira ya Swawm, na usiku wake tulipoonja ladha ya Qiyaamul-Layl (kusimama usiku kuswali). Tumeuaga mwezi wa Qur-aan, mwezi wa taqwa, mwezi wa jihaad, mwezi wa maghfirah, mwezi wa kuomba du'aa kwa wingi, mwezi wa kuepushwa na Moto. Amefaulu aliyetimiza Swiyaam ilivyopaswa akachuma thawabu nyingi na akajitahidi kuzidisha ‘ibaadah. Lakini amekula hasara aliyepuuza Swiyaam na hukmu zake na kutokujitahidi katika ‘ibaadah.    

 

Kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Aayah zilizofaridhishwa kufunga Swiyaam katika Ramadhwaan kuwa lengo la Swiyaam ni taqwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyoandikwa kwa wale ambao wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa [Al-Baqarah: 183]

 

Kila Muislamu aliyeingia katika mwezi wa Ramadhwaan atakuwa ameingia na ametoka katika madrasa ya taqwa. Na mtu anapoingia katika madrasa yoyote ile, hutoka humo akiwa amepata manufaa au shahada ya lile somo alilolisoma, na baada ya hapo huitumia ile elimu aliyoisoma kumsaidia katika kuendesha maisha yake. Huendelea kuitumia hiyo elimu katika maisha yake yote hadi kufa kwake. Hivyo hivyo ndivyo ipase kuhusu taqwa inayopatikana katika mwezi wa Ramadhwaan kwammba imsaidie Muislamu katika uhusiano mzuri wa utii kwa Rabb   wake. Basi ni vyema Muislamu aendelee na taqwa hadi atakapoonana na Rabb  wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):     

  وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

Na muabudu Rabb  wako mpaka ikufikie yakini (mauti) [Al-Hijr: 99]

 

Hiyo ndio maana ya istiqaamah (kunyooka au kuendelea kuthibiti katika ‘ibaadah) jambo liloamrisihwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ

basi thibitikeni imara Kwake, na mwombeni maghfirah.. [Fusswilat: 6]

 

فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا ۚ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿١١٢﴾

 

Basi thibitika imara kama ulivyoamrishwa na aliyetubia pamoja nawe, na wala msiruke mipaka. Hakika Yeye kwa myatendayo ni Mwenye kuona.  [Huwd: 112]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pia ametufundisha kuhusu kuthibitika katika ‘ibaadah;

 

 عن أبي عَمْرو، وَقِيلَ: أبي عَمْرَةَ، سُفْيَانَ بْنِ عَبْدِ اللهِ الثّقَفيِّ رَضيَ اللهُ عَنْهُ قَال: قُلْتُ: يا رَسُولَ الله، قُلْ لي في الإِسْلاَمِ قَوْلاً، لاَ أَسْأَلُ عَنْهُ أَحَداً غَيْرَكَ. قَال: ((قُلْ: آمَنْتُ باللهِ ثُمَّ اسْتَقِمْ)).

Kutoka kwa Abu 'Amr, vile vile (anajulikana kama) Abu 'Amrah Sufyaan bin Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Niambie kitu kuhusu Uislamu ambacho siwezi kumuuliza mtu yeyote ila wewe.  Akasema (Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Sema; Namuamini Allaah, kisha kuwa mwenye kunyooka. (kwa kuendelea kufanya ‘ibaadah na kuwa na msimamo madhubuti katika dini)) [Imesimuliwa na Muslim]

 

Kuthibitika katika ‘ibaadah ya Ramadhwaan au katika msimu wowote mwengineo kama vile kumaliza kutekeleza Hajj, ni dalili ya kukubaliwa ‘amali alizozifanya mtu humo. Kuhakikisha kuwa umethibitika katika ‘ibaadah, jiulize maswali yafuatayo:

 

1.  Je, Umekufikia mchana mmoja ukiwa katika kufunga Swawm za Sunnah?

 

2.  Je, Umekufikia usiku mmoja ukiwa katika Qiyaamul-Layl?

 

3.  Je, Umeburudika na kusoma Qur-aan kama ulivyokuwa ukisoma katika Ramadhwaan?

 

4. Je, Umemdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa wingi kama ulivyokuwa ukimdhukuru katika Ramadhwaan? 

 

5.  Je, umetokwa na machozi kwa kukumbuka madhambi na kuhofia adhabu za Allaah (Subhaanah wa Ta’aalaa)?

  

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anapenda ‘amali za mwana Aadam anazoziendeleza japokuwa ni chache kuliko ‘amali nyingi kisha asiziendeleze:

 

قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((أَحَبَّ الْأَعْمَالِ إِلَى اللَّهِ أَدْوَمُهَا وَإِنْ قَلَّ))  متفق عليه

Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam) ((‘Amali Anazozipenda zaidi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  ni zile zinazodumishwa japokuwa ni kidogo)).  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Basi thibitika katika miezi mingineyo kwa amali zifuatazo:

 

1- Swiyaam za Sunnah zifuatazo:

 

i-Sittah Shawwaal; thawabu zake ni kama Swiyaam za mwaka mzima:    

 

عَنْ أَبِي أَيُّوبَ الْأَنْصَارِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ صَامَ رَمَضَانَ ثُمَّ أَتْبَعَهُ سِتًّا مِنْ شَوَّالٍ كَانَ كَصِيَامِ الدَّهْرِ))   رواه مسلم و الترمذي وابن ماجه, أبو داود و أحمد 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ayyuwb Al-Answaariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayefunga mwezi wa Ramadhwaan, kisha akafuatia sita za Shawwaal ni kama swawm za dahari)). [Imepokewa na Maimaam Muslim, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Abu Daawuwd na Ahmad]  

 

ii-Swawm za Jumatatu na Alkhamiys

iii-Siku tatu katika mwezi, (Ayaamul-Biydhw)

iv-Swawm ya Arafah

v-Swawm ya 'Ashuraa.

 

Bonyeza kiungu kifuatacho upate fadhila za Swiyaam hizo:  

 

 Swawm Baada Ya Ramadhwaan 

 

 

2-Qiyaamul-Layl (kisimamo cha kuswali usiku)

 

Ni Swalaah ya Sunnah iliyo bora kabisa baada ya Swalaah ya fardh kwa dalili:   

((أَفْضَلُ الصَّلاةِ بَعْدَ الْفَرِيضَةِ صَلاةُ اللَّيْلِ)) رواه مسلم.

((Swalaah iliyo bora kabisa baada ya fardh ni Swalaah ya usiku)) [Muslim]

Fadhila zake zinapatikana katika kiungo kifuatacho:

Fadhila Na Faida Za Qiyaamul-Layl

 

 

3-Swadaqah: 

 

Ikiwa ulikuwa ukitoa swadaqah katika Ramadhwaan kwa wingi, basi endelea kutoa swadaqah japo kidogo kidogo miezi mingineyo. Swadaqah ni kinga kubwa dhidi ya adui, maradhi na humtakasa mtu kutokana na uhasidi, chuki n.k. Juu ya hivyo, humzidisha mtoaji kheri na baraka nyingi katika mali yake na maisha yake kwa ujumla, na Hadiyth ifuatayo imetaja mengineyo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ،  وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إلاَّ عِزًّا،  وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ)) مسلم               

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kutoa swadaqah hakupunguzi mali, Allaah Hamzidishii mja msamaha ila Humpa utukufu, na yeyote anayenyenyekea kwa ajili ya Allaah, Allaah Aliyetukuka Atampandisha Daraja [Atamtukuza])).[Muslim]

 

Kumbuka pia ee ndugu Muislamu, kwamba chochote unachotoa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi Yeye Ametoa ahadi kuwa Atakulipa na kukughufuria madhambi yako. Ametoa ahadi hiyo katika Aayah kadhaa za Qur-aan, mojawapo ni:   

مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١١﴾

 

Nani ambaye atamkopesha Allaah karadha nzuri kisha (Allaah) Amuongezee maradufu na apate ujira mtukufu. [Al-Hadiyd: 11]

 

 

4-Kulisha masikini:

 

Ni jambo Analolipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Amelisisitiza katika Qur-aan na kuwasifu wenye kulisha maskini na wengineo kwamba ni waja wema na jazaa yao ni Jannah:

 

إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا﴿٥﴾

 

Hakika Waumini watendao wema kwa wingi watakunywa katika vikombe vya mvinyo mchanganyiko wake ni (kutoka chemchemu iitawayo) kaafuwraa.

 

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا﴿٦﴾

Chemchemu watakayokunywa humo waja wa Allaah, wataibubujua kwa wingi.

 

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا﴿٧﴾

Wanatimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea kwa upana.

 

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka.

 

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

“Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kwenu jazaa na wala shukurani.

إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا﴿١٠﴾

“Hakika sisi tunakhofu kutoka kwa Rabb wetu siku ya masononeko, ngumu na ndefu mno.

 

فَوَقَاهُمُ اللَّـهُ شَرَّ ذَٰلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا﴿١١﴾

Basi Allaah Atawakinga na shari ya siku hiyo, na Atawapa nuru ya ujamali na furaha.

 

وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا﴿١٢﴾

Na Atawalipa kwa sababu ya kusubiri kwao, Jannah na nguo za hariri.    [Al-Insaan: 5-12 na zinaendelea Aayaat kutaja neema za Jannah] 

 

 

5-Kutenda wema na ukarimu:

 

Bila shaka Ramadhwaan ulikuwa ukizidisha wema kwa wazazi, ndugu, jamaa, jirani na marafiki, na wenye kuhitaji; basi endelea kutenda wema miezi yote mingine.  

 

Ndugu Muislamu, usije kuwa kama yule mwanamke wa Makkah ambaye alikuwa akifuma uzi wake ukiwa madhubuti kisha huufumua. Ametajwa katika Qur-aan:

 

وَلَا تَكُونُوا كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ أَنكَاثًا  

Na wala msiwe kama yule mwanamke aliyezongoa uzi wake vipande vipande baada ya (kuusokota na) kuwa mgumu.  [An-Nahl: 92]

 

Hivyo ni sawa na ambaye anarudi katika maasi baada ya kutoka katika utii wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na hao ni watu wanaomtambua Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Ramadhwaan pekee. 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alipofariki, Swahaabah walikuwa katika vilio na huzuni kubwa za ajabu hadi kuchanganyikiwa akili! Imepokelewa katika Al-Bukhaariyy kwamba 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisimama akasema: "Wa-Allaahi Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam hakufa!” Kisha baadaye akasema: “Wa-Allaahi hakuna kilichonipitia akilini isipokuwa hilo” Akasema: “Hakika Allaah Atamfufua na atakata mikono na miguu ya baadhi ya watu”  

 

 Kisha Abuu Bakar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akawaambia:

 

أَلا مَنْ كَانَ يَعْبُدُ مُحَمَّدًا صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَإِنَّ مُحَمَّدًا قَدْ مَاتَ، وَمَنْ كَانَ يَعْبُدُ اللَّهَ فَإِنَّ اللَّهَ حَيٌّ لاَ يَمُوتُ،

"Yeyote aliyekuwa anamuabudu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi Muhammad ameshafariki. Na yeyote aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Yu hai Hafi! …. [Al-Bukhaariy (4452)]

 

Basi ni sawa na kusema: “Aliyekuwa anaabudu Ramadhwaan, basi Ramadhwaan inapita na aliyekuwa anamwabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hatoweki (Hafi)."

 

Yafuatayo ni ambayo yatamdhihirishia Muislamu baada ya Ramadhwaan kwamba hakuthibitika katika ‘ibaadah:   

 

1-Kupuuza Swalaah

 

Kwa kutokuswali Swalaah za fardhi, au kutokuziswali kwa wakati wake au kutokuziswali kwa kwa utulivu kama ipasavyo.

 

2-Kuacha kuswali Swalaah za jamaa Misikitini:

 

Swalaah ya jamaa imesisitizwa sana na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam); lakini haikusisitizwa kwa ajili ya Ramadhwaan pekee, bali kwa miezi yote. Inasikitisha kuona Misikiti inajaa watu Ramadhwaan lakini ikimalizika tu Ramadhwaan watu hawaonekani kwa wingi Misikitini. Muislamu asiyeswali jamaa Msikitini anajikosea fadhila nyingi zilizotajwa katika Qur-aan na katika Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).    

 

3-Kuacha kusoma Qur-aan:

 

Baadhi ya watu huisoma Qur-aan katika Ramadhwaan pekee. Ikimalizika Ramadhwaan, misahafu hurudishwa kabatini ikasahauliwa mpaka Ramadhwaan nyingine na hali Muislamu anahitaji kusioma kupata Uongofu na manufaa mengineyo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):    

 يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini.

 

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴿٥٨﴾

Sema: “Kwa fadhila za Allaah na kwa rahmah Yake basi kwa hayo wafurahi.” Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.     [Yuwnus: 57-58]

 

Vile vile ni muhimu sana Muislamu ajifunze maana na tafsiri ya Qur-aan ili atambue maamrisho na makatazo yake. Pia Qur-aan ni kiburudisho cha nyoyo kwa sababu humo mna visa vya watu wa kale ambavyo vina mafunzo mazuri na mazingatio.

 

4-Kurudia katika maasi na mambo ya upuuzi:

 

Inampasa Muislamu aendelee kujiepusha na maasi na mambo ya upuuzi yanayompotezea muda wake kama kusikiliza nyimbo, kukaa barazani kupiga soga, kusengenya na kadhaalika. Ni vyema mtu autumie wakati wake kutafuta elimu ya Dini yake na katika yale yenye kumridhisha Rabb   wake. Kujiepusha na mambo ya upuuzi ni sifa mojawapo miongoni mwa sifa za kuipata Jannah ya Al-Firdaws kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

  ...وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ....  أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾  الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾    

  Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi  …. Hao ndio warithi… Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.  [Al-Muuminuwn: 1 -11]

 

Ndugu Muislamu, endelea kunyooka katika taqwa na ‘ibaadah wakati wote, kwa sababu hujui lini Malaika wa kuchukua roho atakufikia. Jihadhari kukutana naye ukiwa katika maasi na badala yake jiandae kw amauti ukiwa katika hali kama ifuatayo:

 

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾

. Hakika wale waliosema: “Rabb wetu ni Allaah.” Kisha wakathibitika imara; Malaika huwateremkia: (kuwaambia): “Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa.”

 

نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾

 “Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba.

نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾

 “Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.”  [Fusw-swilat: 30-32]

 

Usiache kuomba Du'aa za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizokuwa akipenda sana kuzisoma kuhusu kuthibitika katika Dini na utii:

 

 اَللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك

Allaahuuma yaa Muqallibal-quluwubi Thabbit qalbiy 'alaa Diynik

 

(Ee Allaah! Ee Mgeuza nyoyo, thibitisha  moyo wangu katika Dini Yako)

 

اّللَّهُمَّ ياَ مُصَرِّفَ الْقُلُوب صَرِّف  قُلُوبَناَ عَلَى طَاعَتِك         

Allaahuumma yaa Muswarrifal-quluwbi, Swarrif Quluwbanaa 'alaa twaa'atik

(Ee Allaah! Ee Muelekezaji wa nyoyo, Elekeza nyoyo zetu katika utii Wako

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share