Nasiha 40 Za Ramadhwaan – Zitekeleze Ufaidike na Mwezi Mtukufu

 

Nasiha 40 Za Ramadhwaan – Zitekeleze Ufaidike na Mwezi Mtukufu

 

Alhidaaya.com

 

 

1-Anza kwa kuzingatia mwezi huu mtukufu uwe wa kujihesabu, kutenda amali nyingi na kujirekebisha hali yako na uhusiano wako na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) uwe bora zaidi:

 

2- Kumbuka kwamba huu mwezi ni mgeni ambaye amekutembelea kisha ataondoka, hivyo mpokee mgeni wako na mkirimu kwa mazuri yote anayostahiki.

 

3-Tahadhari na kutokufunga bila ya sababu au udhuru wowote, kwani kufanya hivyo, Swawm yako haitolipika hata ukifunga mwaka mzima. 

 

4-Swali kwa wakati wake, usiache Swalah ikakupita. Na jua kuwa ukiwa huswali Ramadhwaan huna Swawm kwa mujibu wa fatw za Maulamaa wengi.

 

5-Soma sana Qur-aan kadiri uwezavyo kwani ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan. Kamilisha msahafu mzima japo mara moja, ukishindwa basi hata nusu yake, robo yake.  

 

6-Zidisha ibada za Sunnah, kama Sunnah zilizo Muakkadah (zilizosisitizwa) na zile Ghayri Muakkadah (zisizosisitizwa). Tazama ratiba katika kiungo kifuatacho:

 

Ratiba Ya Swalah Za Sunnah Zilizosisitizwa Na Zisizosisitizwa

 

7-Chukua fursa kuomba du'aa sana kila mara nyakati za kukubaliwa du'aa, khaswa ukiwa bado katika Swawm. Tumia wakati wa baina ya adhana na iqaamah kuomba du'aa na haja zako kwani ni wakati wa kukubaliwa du'aa. Vile vile nyakati za thuluthi ya mwisho ya usiku.

 

8-Iborishe Swalah yako kwa kuiswali ipasavyo na kuzidisha khushuu (unyenyekevu).

 

9-Usiache kuswali Taraawiyh pamoja na jama‘ah, usiondoke hadi Imaam amalize upate thawabu za Qiyaamul-Layl.

 

10-Tahadhari na kufanya israaf ya mali, chakula na neema nyinginezo, kwani israaf ni mbaya na itakuondoshea neema ulizojaaliwa.

 

11- Tumia wakati wako vizuri na zingatia kwamba umri wako unazidi kupunguka.

 

12-Mwezi huu ni wa ibada na sio kula, kulala na kufanya ya upuuzi.

 

13-Zoesha ulimi wako uwe umerutubika kwa kumtaja Mola wako, usiwe miongoni mwa wasiomkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ila kidogo tu.

 

14-Chukua fursa kufanya da‘awah. Amrisha mema na kataza maovu, kwani yule unayemuongoza atakapotekeleza mema, utazibeba nawe thawabu zake pia. Tuma ujumbe wa dini kwa wenzako. Chapisha idadi nyingi ya makala zenye mafunzo ya dini, chapisha du'aa ugawe misikitini, vyuoni, majumbani. Unaweza kupata makala na du'aa mbali mbali katika Alhidaaya.com Pia kama una uwezo zaidi rekodi mawaidha yaliyomo ndani ya tovuti na wagawie wenzako upate ujira zaidi. Gawa bure na usiuze, kwani si ya kuuzwa.

 

15-Fanya kila aina ya wema uwezavyo, patanisha waliokhasimiana, msaidie mwenye haja na muokoe mwenye shida.  

 

16-Wakumbuke wazazi, ndugu, jamaa na marafiki katika du'aa zako kwani kuwaombea wao bila ya wao kujua Malaika hukuombea na wewe vile vile.

 

17-Wasiliana na ndugu, jamaa kwani ni jambo lililosisitizwa sana na lenye kukuongeza umri, kheri na baraka nyingi. Walio mbali na wewe wasiliana nao kwa simu.

 

18-Unapohisi njaa, wafikirie masikini wasio na uwezo wa kula, na utambue kuwa uko katika neema ya Mola wako.

 

19-Muombe msamaha uliyemdhulumu kabla hajalipwa mema yako.

 

20-Mfuturishe aliyefunga upate thawabu zake juu ya thawabu zako.

 

21-Omba maghfirah na msamaha kwa Mola wako, kwani tambua kwamba Yeye ni Mwingi wa Msamaha na Mwingi wa Rahma.

 

22-Ikiwa umetenda maasi kisha Akakusitiri Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), tambua kuwa hiyo ni onyo utubie na weka azma kutokurudia tena.  

 

23- elimu ya dini yako kwa kujifunza tafsiyr ya Qur-aan, Hadiyth, Fiqhi n.k. upate kuongeza taqwa.

 

24-Sikiiza mawaidha japo moja kwa siku kwani kusikiliza kunaleta taathira kubwa ya kuongeza Iymaan na Taqwa.

 

25-Jiepushe na marafiki waovu na vikao vyao na ungamana na marafiki wema na vikao vya kheri.

 

26-Usipoteze muda wako kutazama televisheni vipindi visivyokupa faida na dini yako, bali tumia wakati wako kwa yatakayokuongezea elimu na Taqwa.

 

27-Usiharibu Swawm yako kwa kunena ya upuuzi, au Ghiybah (kusengenya), au kubishana au kupandisha sauti. Jizuie unapokuwa na hamaki.

 

28-Fika msikitini mapema zaidi, kwani hivyo ni dalili ya hamu na mapenzi ya ibada na kuwa karibu na Mola wako.

 

29-Waamrishe na kuwafunza mema ya dini yao walio katika majukumu yako; mke, mume, watoto, ndugu, jamaa n.k. kwani wako karibu yako zaidi na kukutii.  

 

30-Usijaze tumbo sana katika suhuur (daku) kwani itakufanya uwe mvivu na ushindwe kukaa macho nyakati za asubuhi na mchana na ushindwe kufanya ibada vizuri na kusoma sana Qur-aan.   

 

31-Usijaze tumbo sana katika iftwaar (kufuturu) kwani itakushinda kusimama Qiyaamul-Layl au kuzingatia Aayah za Qur-aan zinaposomwa na Imaam.

 

32-Punguza kwenda madukani/sokoni khaswa kumi la mwisho kwani utakosa kheri na thawabu nyingi zilizomo katika masiku hayo ya thamani kubwa.

 

33-Tilia hima kubwa kuswali Qiyaamul-Layl kumi la mwisho upate Laylatul-Qadr, usiku ambao ibada yake ni bora kuliko miezi elfu.

 

34-Jitahidi ufanye I'tikaaf msikitini katika kumi la mwisho japo siku chache, upate fadhila zake na uchume mema mengi pamoja na kupata Laylatul-Qadr.  

 

35-Tambua kwamba siku ya 'Iyd ni siku ya kumshukuru Mola wako na sio siku ya kutenda yale uliyojizuia ya maovu katika Ramadhwaan.

 

36-Siku ya 'Iyd , wafanyie wema wazazi, watembelee ndugu, jamaa na marafiki kuboresha uhusiano wako nao.

 

37-Usiache kutoa Zakatul-Fitwr - wakumbuke maskini, yatima na wanaohitaji na wasaidie na kuwagawia chochote wabakie katika furaha.

 

38-Tamka Takbiyrah siku ya 'Iyd kwa sauti unapokwenda msikitini ili kuwakumbusha wengine wanaokwenda au kufuatana nawe ili nawe waweze kupiga Takbiyrah hizo.

 

39-Weka azma baada ya Ramadhwaan kujiendeleza katika hali ya ibada uliyokuwa nayo katika Ramadhwaan, ukifanya hivyo itakuwa ni dalili ya kukubaliwa Swawm yako.

 

40- Funga Sita Shawwaal upate thawabu za Swawm ya mwaka mzima.

 

 

 

 

Share