Anamkhalif Imaam Kwa Kusoma Du'aa Ya Qunuut Wakati Imaam Anasujudu

SWALI:

ASALAMU ALEYKUM WARAHMATULLAHY WABARAKATU, MIMI MSIMAMO WANGU KUHUSU KUNUTI KATIKA SWALA YA ALFAJIRI NI LAZIMA NIISOME IMA NIWE MAAMUMA AU IMAMU, YAANI HATA KAMA IMAMU HAKUISOMA BASI MIMI HUWA NAMUHALIFU NAISOMA YEYE ANAPOKWENDA KUSUJUDU. JE? KWA HALI HII NIPO SAHIHI? NA SWALA YANGU INAKUBALIWA?

NA HILI MBONA NI JAMBO DOGO TU? NAOMBA UFAFANUZI ZAIDI WA KIELIMU.

WASLMU ALEYKUM.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumhalifu Imaam kwa kusoma Qunuut. Kwa jinsi swali lilivyokuja inaonyesha dhahiri kuwa muulizaji anaegemea katika dhehebu la Ki-Shafi‘iy katika Fiqh yake. Mbali na hayo inafahamika katika madhehbu zote kuwa Qunuut si nguzo wala wajibu wa kukamilika na kutimia Swalah ya Muislamu. Inafahamika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuweka ada ya kusoma Qunuut katika kila Swalaah ya Alfajiri bali wakati wa matatizo alikuwa anasoma Qunuut katika Swalaah zote kwa muda fulani.

Zipo nyakati ambazo alisoma Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Qunuut katika Swalaah ya Alfajiri lakini haikuwa kila siku. Hata hivyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituwekea msingi katika Hadiyth yake sahihi: “Imaam amewekwa ili afuatwe”. Kwa hiyo, haifai kwa maamuma kumkhalifu Imaam, kumkhalifu Imaam ni kuharibikiwa na Swalah yake. Mfano mzuri wa kuonyesha kuwa Qunuut si wajibu wala ukiikosa hutawajika hata kuleta Sijdah ya kusahau ni yale yaliyotokea pale Imaam ash-Shafi‘iy alipokwenda kuzuru Kufah. Aliombwa Imaam aswalishe Swalah ya Alfajiri katika Msikiti ambao Imaam Abu Haniyfah alikuwa akifundisha na kuswali. Maamuma walitarajia kuwa Imaam atashikilia msimamo wake wa kusoma Qunuut lakini hakusoma wala hakuleta Sajdah ya kusahau, hilo likawastaajabisha wengi. Hivyo, wakamuuliza imekuwaje naye akawajibu je, basi hata nisiheshimu rai ya Imaam mkubwa wa sehemu hii? Ibara hiyo alikuwa anamaanisha Imaam Abu Haniyfah aliyezikwa katika mji huo wa Kufah.

Hivyo, ndugu yetu ikiwa Imaam hatasoma Qunuut itabidi umfuate na Swalaah yako itakuwa sahihi kabisa. Na pia kauli yako ya kusema kuwa, ‘NA HILI MBONA NI JAMBO DOGO TU? Inathibitisha kuwa huna wewe haja ya kulazimisha jambo hilo na hali ni suala dogo na lisilohitaji fujo hizo za LAZIMA uisome ukiwa ni Imaam au maamuma. Kwa hiyo tunakushauri ufuate alivyofanya Imaam wako alipokwenda Kufah na zaidi ya yote ufuate Sunnah za Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilizokamilika na kuacha kung’ang’ania umadhehebu hadi ukakhalifu Sunnah za Mtume wetu mhashamu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Tunakuombea kila la kheri katika kushikamana na mafunzo sahihi ya Dini yetu.

Pia unaweza kupata faida zaidi kwenye viungo vifuatavyo:

Kusoma Duaa Ya Qunuut Katika Swalah Ya Alfajiri Ni Sunnah?

Du'aa za Qunut Ziko Ngapi Na Je Lazima Zisomwe Katika Swalah Ya Alfajiri?

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share