Zingatio: Mwili Una Haki Zake

 

Zingatio: Mwili Una Haki Zake

 

 Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kiwanda cha gari kinazalisha mahitaji ya usafiri kwa wanaadamu ili wapate urahisi wa maisha yao hapa duniani. Gari inayotoka hapo ni kawaida yake kuwa na maelezo ya kina kama kwenye ‘catalogue. Wala hakuna wasiwasi wowote kwamba iwapo itatumika kinyume na maelezo ya kiwanda hicho, gari hiyo itahamia gereji.

 

Mwanadamu ameletwa hapa duniani kuja kumuabudu Rabb Mlezi. Ni wajibu wake kufuata yale Anayoyataka Rabb wa mbingu na ardhi. Na wala hakuna mwengine apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah Mmoja, Mlezi wa viumbe vyote.

 

Allaah Ameiteremsha Qur-aan ili iwe ni muongozo sahihi kwa viumbe vyote. Sunnah nayo ipo bega kwa bega pamoja na Qur-aan ikitoa maelezo ya kina na masuala mbali mbali yakifafanuliwa humo. Huu ndio uteremsho ambao ni msingi mkuu wa maisha yetu hapa duniani. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema ndani ya Qur-aan Tukufu:

 

 وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ﴿٤٤﴾

Na Tumekuteremshia Ukumbusho (Qur-aan) ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao huenda wakapata kutafakari. [Al-Nahl: 44]

 

Waislamu tunaamini kwamba Qur-aan na Sunnah ndio miongozo mikuu ya maisha yetu hapa duniani. Njia nyengine yoyote itakayofuatwa itampelekea mwanaadamu kupotea kwenye udhalilifu mbaya kabisa.

 

Mengi tumeyasikia na kuyasoma; ya kwamba Uislamu umeharamisha kukaribia na kutenda zinaa, kulewa, kuiba, kutembea utupu na mengineyo mengi. Sasa yawa hakieleweki pale linapoibuka kundi moja linalodai kutetea haki za wanaadamu likasema: 'kulewa rukhsa' ama 'zinaa rukhsa'. Wengine wamefurutu ada hadi kudai kwamba 'adhabu ya kifo ifutwe' ukweli wa hili ni kusema: 'kuua rukhsa'. Hizi rukhsa rukhsa hazina kikomo wala kikwazo?

 

Cha kusikitisha zaidi ni kuona dada na kaka zetu walio wengi wakishabikia na kutetea hizo zinazodaiwa haki za binaadamu. Sasa cha kujiuliza kwani mwili nao hauna haki zake? Kama mwili leo utapewa nafasi ya kujitetea, utasema hautaki kupenyezewa pombe wala sigara. Hizi ndimi na nafsi zetu tumezipa nafasi ya juu tukisahau kwamba mwili nao wataka haki zake!

 

Ulimwengu umekosa dira kutokana na kuidharau Qur-aan pamoja na Sunnah yake. Ingawa ukweli ni kwamba mengi wanayoyavumbua walimwengu yameshaelezwa ndani ya vyanzo hivyo vya Uislamu. Alichotufunza Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hatuna budi kukifuata. Hiyo sio khiari, bali ni wajibu. Ajabu ya Waislamu ndio wa mwanzo kukimbilia kwa makafiri kutaka misaada au wakiomba kusuluhishiwa matatizo yao. Mbio hizi zinafanywa bila ya kugonga mlango wa Qur-aan na Sunnah.

 

Kuna kisa ambacho kinatudhihirishia kwamba kufuata kile alichokiamrisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio wajibu wetu. Kuna yahudi mmoja alikuwa na mgogoro pamoja na Muislamu. Yahudi akataka kusuluhishwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati huyo Muislamu alitaka kwenda kwa Ka'b bin al-Ashraf ambaye ni Yahudi adui Mnafiki mkuu. Hatimaye ukapelekwa kwa Nabiy na ikaamuliwa kwamba yahudi ndie mwenye haki. Muislamu hakuridhika akaenda kulalamika kwa Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Alipotambua kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwishatolea uamuzi mgogoro huo, Sayyidna 'Umar alitoka na upanga wake na kumpiga nao wa shingo huku akisema: "Hivi ndivyo ninavyomuhukumu yule ambaye hakuridhika na amri ya Allaah na Nabiy Wake."

 

Tunachojifunza hapa ni kwamba Waislamu wenyewe hawazipi kipaumbele kanuni zao na badala yake wanakimbilia kwa wanafiki na makafiri. Pia ni wajibu wa Waislamu kufuata yale ambayo Ameyaamrisha Rabb Mlezi pamoja na Nabiy Wake. Hapo mjadala umefungwa kwa kudai kwamba ni haki ya mwanaadamu kuzini, kulewa, kuiba ama kuua.

 

 

 

 

 

Share