Mashairi: Ya Habibi Ya Nabiya

 

                  

         Muhammad Faraj Salim As-Sa’ay

 

Makka ulikozaliwa,          Madina ukapokewa

Kwa mashada ya mauwa, Ya Habibi ya Nabiya

 

Maka ilikochomoza,        nuru ya Mola Muweza

Madina ikaangaza          kisha  kote kueneya,

 

Ulikuja na risala,               kutoka Kwake Taala
isomwe kila mahala,       kila pembe ya duniya

Ni Risala kamilifu,             Yake Mola Mtukufu
aso mwana wala kufu,   yenye kunawiri njiya

 

Yote ukayatimiza,            hapana ulichosaza
tena bila kupunguza,      kamili kutufikiya

Ukatufunza shahada,     akhlaqi na ibada
na kutoa misaada,           kwa wenye kuhitajiya

Allahu katakasika,            Mola aso mshirika
ni shahada ya hakika,     na wewe wake nabiya

Hiyo ndiyo ya awali,        alotufunza rasuli
ni nguzo iliyo ghali,          nyoyoni mwetu jamiya

Swala akatufundisha,     asubuhi hadi Isha
zote twazikamilisha,       nyakati zikiingiya

Twaziswali kwa wakati,  kwa ikhilasi na dhati
tena bila hatihati,             Ya Rabbi takabaliya

Kisha tutowe na Zaka,    wakati unapofika
kwa hesabu kila mwaka, nisabu ikitimiya

Ilitiliwa mkazo,                  tajiri na walo nazo
tugawe bila vikwazo,      tuwape wahitajiya

Kisha kutoa sadaka,        hiyo kama tukitaka
mali inatakasika,               na kurudisha afiya

Kuhiji Maka ni nguzo,     kwa kila mwenye uwezo
hiyo haina mchezo,         yataka kuipaniya

Kaaba nyumba tukufu,  nyumba kongwe takatifu
hapo lazima utufu,          shoti saba kutimiya

Nyumba hiyo ipo Maka, ni mji wenye baraka
Dhambi hapo hufutika,  Mola Ametuambiya

Arafati ndiyo hija,            huko nako kwakungoja
kwake aliye Mmoja,       dua zinaelekeya

Siku hiyo ikifika,                watu tena patashika
machozi yamiminika,      wakiomba na kuliya

Labeka Rabi labeka,        Mola uso mshirika
Arafati tumefika,              nawe watushuhudiya

 

Mwenye sifa ya uluwa, La ilaaha illa Huwa
ziwe zitakavyokuwa,      dhambi utatufutiya

 

Uturudishe tukiwa,         kama tulivyozaliwa

ndivyo tulivyoambiwa,  na Muhammadi nabiya

Kisha Mina siku tatu,      wanakusanyika watu
wanapiga jamaratu,        na kuchinja adhuhiya

Yabaki shughuli moja,    hiyo pia yakungoja
ni shoti saba za hija,        tawafu na sayi piya

 

safari ikishafika,                ukataka kuondoka

usibaki hapo Maka          Widaa itabakiya

 

Hiyo ni tawafu moja,      ukesha moja kwa moja

Hapana tena kungoja     Garini utaingiya

Hizo ndizo nguzo zake,  na hiyo risala yake
kutoka kwa Mola wake, ni amana ya Jaliya

Ni nzito kweli kweli,        Ilikataa jabali
wewe ukaikubali,             kubeba ukairidhiya

Mola amekuhitari,           mbele ya wote bashari
uifikishe habari,                kwa jini na insiya

 

Anachokitaka huwa,       Mwenyewe kakuchaguwa
kwa sababu akujuwa,    kipenzi chake nabiya

Mwenye khuluqa adhimu, mpole tena karimu
kwa uma wake rahimu, kuliko kila nabiya

 

Ni mwenendo mtukufu, ulotimu kamilifu
mkweli muaminifu,         mwenye sifa maridhiya

Mfano wa Quruani,         inotembea njiani
kakufundisha Manani,   utukufu wa tabiya

 

 

 

Share