Amepokea Bidhaa Si Zake, Kuzifungua Ni Pombe, Afanyeje?

SWALI:

 

Mmi ni mfanyabiashara ya vitabu vya kiislamu. Siku moja nilinunua bidhaa, ikabidi nitangulie mzigo ufuatie baadae. Nilipofika ofisi ya gari nikakuta boksi lenye sura kama la kwangu, nikalichukua mpaka dukani.  SubhanaLlaah nilipofungua ni makopo ya bia, nifanyeje?

Nilisita kuurudisha mpaka mwenyewe akaufuata. Mzigo wangu uliletwa kabla huyo jamaa hajaja. Jee ilikuwa niurudishe, niutupe au nifanyeje?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu upokeaji wa bidhaa ambazo si zako.

 

Ifahamike kuwa Muislamu ni mtu ambaye yuko makini sana katika kufanya mambo katika maisha yake hapa duniani. Uliwajibika mwanzo kabisa kuutazama mzigo kabla ya kwenda nao dukani kwako kwani kufanya hivyo kungekupunguzia mengi katika taabu hizo ulizozieleza. Na kila wakati unatakiwa uwe hivyo kuhakikisha mambo na vitu kabla ya kujiingiza, kwani usipofanya hivyo huenda ukapata shida ambayo hukuitarajia kabisa.

 

Mbali na hayo, Muislamu anakuwa ni muaminifu na uaminifu unakuja hapa ni kuwa ulichukua mzigo wa watu kimakosa na hivyo unatakiwa umjulishe mwenye mzigo huo aufuate kuuchukua haraka kwani wewe kukaa nao pia haifai kwani ni katika mambo yaliyokatazwa kuyahifadhi Muislamu.

 

Tanbihi: Inatakiwa kama Waislamu tusaidianeni katika uchaji Mungu na wema wala tusisaidiane katika uadui na madhambi. Kwa minajili hiyo inatakiwa tuwe waangalifu sana katika utumaji wa bidhaa kupitia usafiri wowote. Kwa hiyo, ni wajibu wako kwa kuwa gari hilo linapakia pombe na vitu vingine vya haramu nawe umejua utafute usafiri wa gari jingine ambalo halitakuwa kama hilo. Ikiwa mwenye gari ni Muislamu ni wajibu wako kumueleza kuwa hilo linalofanyika ni makosa. Ikiwa atajirekebisha endelea kutuma kupitia kwa gari lake na lau ataendelea basi tafuta usafiri mwengine wa Muislamu na ikiwa hakuna Muislamu basi tuma kupitia kwa mwengine ambaye si Muislamu lakini habebi pombe au vitu vya haramu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share