Kufanya Kazi Katika Shirika La Ribaa Nini Hukmu Yake

SWALI:

Asssalam aleykum

 

Nakushukuruni sana nyote mlio jitahidi kutuelimisheni sisi ndugu zenu kupitia web site hii.Nakutakieni kila la kheri dunia wal akhera.

 

Napenda ndugu waisalamu munitoe ujahili kuhusu Riba. Naelewa kuwa Riba ni haramu katika dini yetu tukufu ya kislamu lakini naomba nielimisheni zaidi. Swali langu ni nimepata kazi kwenye offisi ya Micro-finance je ni haramu mshahara wangu?

 

Kabla sija pata kazi nili swali swalatul Istighaar rakaa 2. umu uliza mwenyezi mungu kazi ya kheri  baadaye ndio kupata kazi hii .nifenyeje? Niache kazi au vipi?

 

Asanteni ndugu zangu.

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu zetu kwa kututakia mema na kutuombea kila la kheri katika juhudi zetu hizo ndogo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuwafikishie sote hapa duniani na kesho Aakhirah. Tunamuomba Atupe mema na Atuepushe na balaa na mitihani na Atuonyeshe njia nyoofu na Atupatie hima ya kuweza kuifuata.

Hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ameharamisha kuchukua na kutoa riba katika njia zake zote. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Allaah Amehalalisha biashara na kuiharamisha riba” [2: 275].

Na Amesema tena Aliyetukuka: “Enyi Mlioamini! Mcheni Allaah, na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini. Na kama hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtakuwa mmetanganza vita na Allaah na Mtume Wake” [2: 278-279].

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa: “Allaah Amemlaani mwenye kula riba, mwenye kuitoa na mashahidi wake na mwandishi wake” [Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah].

Na amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu uovu wa riba: “Dirhamu ya riba anayokula mtu na huku anajua ni mbaya zaidi kuliko kuzini mara thelathini na sita” [Ahmad].

Amesema tena: “Riba ina milango 73 iliyo nyepesi na sahali ni mtu kulala na mama yake” [Al-Haakim].

Pia, “Jiepusheni na maangamivu saba… kula ribaa” [Al-Bukhaariy na Muslim).

Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Anatutaka tusisaidiane katika uovu na uadui kama alivyosema: “Na saidianeni katika wema na taqwa, wala msisaidiane katika dhambi na uadui” [5: 2].

Kufanya kazi katika benki au taasisi ambazo zinaendeshwa kwa riba ni kusaidia dhulma, dhambi na uadui hivyo Muislamu hafai kufanya kazi katika sehemu na taasisi hizo.

Swalah ya kumtaka Allaah Aliyetukuka ushauri inaitwa Swalatul Istikhaarah, nayo haiwezi kukuonyesha jambo ambalo ni haramu, wala haifai kuiswali kwa kutaka muongoza katika jambo la haraam. Inawezekana kuwa umeiswali huku ukiwa na niya ya kujiunga katika taasisi hiyo. Kupata hiyo kazi ni mtihani kwako kwani Allaah Anatutakia mema na ya kheri wala sio ya makosa na madhambi.

Nasaha kwetu kwako ni uache kazi hiyo na umtegemee Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) naye Atakupatia nyengine yenye kheri kwa Dini yako, maisha yako na hatima yako. na tunamuomba Allaah Akubadilishie kazi iliyo halali na nzuri zaidi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share