Maulidi: Kusherehekea Kuzaliwa Kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
Maulidi: Kusherehekea Kuzaliwa Kwa
Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Sallam)
Imetarjumiwa Na Naaswir Haamid
Alhidaaya.com
Kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni bid'ah (uzushi ndani ya diyn); Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakupata kuwaamrisha wengine kufanya hivyo, na wala hakuwa na Swahaba pembeni mwake wenye kufanya jambo hilo na hivyo hakuna ruhusa iliyotolewa (ikiwemo ile ya kuridhia).
Hatutakiwi kutofautisha miongoni mwa Nabiy yeyote. Kwa mfano tofauti ya hadhi, kama vile mmoja ni bora kuliko mwengine. Hili linapelekea kwenye ibada ya kishirikina, kama vile walivyofanya Wakristo walipoanza kumuabudia Yesu badala ya kumtambua kama ni Mtume tu. Ukweli ni kwamba wamechupa hatua mbali zaidi… na waliendelea kumuabudia, hadi hatua tunayoiona leo.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Msinitukuze Kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja kwa hiyo semeni mja wa Rasuli na Wake". [Al-Bukhaariy na Muslim]
Lililo muhimu baina ya kila Nabiy na/au Mjumbe ni UJUMBE.
Hatari Ya Kuzusha Mambo Ndani Ya Diyn
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Maneno bora ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na Uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika diyn) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni motoni". [Muslim katika Swahiyh yake]
Usitofautishe Baina Ya Rasuli/Manabiy
Qur-aan Tukufu inasema:
آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٢٨٥﴾
Rasuli ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Rabb wake na Waumini (pia). Wote wamemwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Rusuli Wake. (Nao husema): Hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Rusuli Wake. Na wakasema: Tumesikia na tumetii, tunakuomba maghfirah Rabb wetu na Kwako ni mahali pa kuishia [Al-Baqarah: 285]
Na Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa anasema:
قُولُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ ﴿١٣٦﴾
Semeni: Tumemwamini Allaah na yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl na Is-haaq na Ya’quwb na Al-Asbaatw na aliyopewa Muwsaa na ‘Iysaa na waliyopewa Manabii kutoka kwa Rabb wao, hatutofautishi baina ya mmoja yeyote miongoni nasi ni Waislamu (tunajisalimisha) Kwake. [Al-Baqarah: 136]
Na anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَالَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَلَمْ يُفَرِّقُوا بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ أُولَـٰئِكَ سَوْفَ يُؤْتِيهِمْ أُجُورَهُمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١٥٢﴾
Na wale waliomwamini Allaah na Rusuli Wake na hawakumfarikisha yeyote baina yao; hao Atawapa ujira wao. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An-Nisaa: 152]
Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ لَا تَسْفِكُونَ دِمَاءَكُمْ وَلَا تُخْرِجُونَ أَنفُسَكُم مِّن دِيَارِكُمْ ثُمَّ أَقْرَرْتُمْ وَأَنتُمْ تَشْهَدُونَ ﴿٨٤﴾
Na pindi Tulipochukua fungamano lenu (Tukawaambia): Msimwage damu zenu, wala msitoe nafsi zenu kutoka miji yenu; kisha mkakubali nanyi mnashuhudia. [Al-Baqarah: 84]
Ushirikana Wa Kukithirisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Hivyo, sasa, tunawauliza wale wanaosisitiza kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume… wakiwa na ithibati zilizo wazi bila ya kutofautisha baina ya Rusuli ('Alayhim-salaam)… kwa nini hawasherehekei kuzaliwa kwa Rusuli Wote? Mfano 'Iysa? Unaweza kusherehekea tarehe 25 ya Disemba au kuchagua tarehe nyengine kama hawahitajii hii. Ahaa, sasa nimeona, munazo (hoja) nzuri za kutosherehekea kuzaliwa kwa 'Iysa?? Labda sababu ya kwamba musisherehekee kuzaliwa kwa 'Iysa, ndizo hizo hizo za kwamba musisherehekee kuzaliwa kwa Muhammad? Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
فَلَمَّا آتَاهُمَا صَالِحًا جَعَلَا لَهُ شُرَكَاءَ فِيمَا آتَاهُمَا ۚ فَتَعَالَى اللَّـهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿١٩٠﴾
Basi Anapowapa (mwana) mwema asiyekuwa na kasoro, wanamfanyia (Allaah) washirika katika kile Alichowapa. Basi Ametukuka Allaah kwa Uluwa kutokana na yale yote wanayoshirikisha. [Al-A'raaf: 190]
Ushahidi wa wazi kabisa. Lakini baadhi yao wanaita "mapenzi" na huko ni kwenda mbali kwa yale waliyoamrishwa.
Kukithiri kumsifu mtu inazuiliwa. Inaangukia mara moja kwenye shirki. Kufanya jambo lolote kupindukia mpaka wa kile tulichoamrishwa kufanya, ni kuchupa mipaka na kujikalifisha nafsi yake mwenyewe.
Bedui mmoja alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuuliza kuhusu wudhuu. Alifafanua (akiosha kila kiungo cha mwili wake) mara tatu, na kusema: "Hivyo ndio (namna) ya wudhuu. Na anayefanya zaidi ya hivi amefanya kosa, kuchupa mpaka na kujikalifisha (mwenyewe)." [Imepokewa na Nasa'i, Ibn Maajah na Abu Daawuud]
Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ وَلَا تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ ۚ
Enyi Ahlal-Kitaabi! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Allaah isipokuwa ukweli. [An-Nisaa: 171]
Wale Wanaosema: "Nitampenda Zaidi Yako, Kwa Kutomtii"
Ni lazima tumpende Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko Rusuli wengine yoyote, na pale Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anaposema:
Imesimuliwa na Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Naapa kwa Yule Ambaye maisha yangu yamo Mikononi Mwake, hakuna mmoja atakayeamini hadi anipende mimi kuliko baba yake na watoto wake." [Imepokewa na al-Bukhaariy]
Hii ina maana kwamba Taratibu zake, Sunnah zake – (ni bora zaidi) kuliko ukaribu wa kifamilia; kumbuka, tunaonesha mapenzi kwa kuwa watiifu. Kwa mfano, huwezi kwenda kumpiga mtu katika kichwa chake na kisha kusema: "lakini unajua kwamba nakupenda kweli kweli." Au, wadhalilishaji wanavyofanya, wanapiga kipigo kwa mwenza na kisha wanakiita kitendo hicho ni kitendo cha mapenzi (ndivyo, baadhi yao wanasema haswa kwamba Ndio Sababu ya kumpiga!)
Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefikisha Ujumbe bora. Alikuwa na dhamana malumu. Lakini yeye, mwenyewe, alikuwa ni mtu kama alivyo mwengine – masikini, asiyejua hata kusoma - isipokuwa alikuwa na sifa malumu ya hayaa. Hilo linaweza kusemwa kuwepo kwa Rusuli na Manabiy wote; walikuwa na hayaa nyingi. Sifa hii – hayaa – inaweza kutumika. Hakuna sifa nyengine inayoweza kutumika kumpa heshima mwengine juu ya mwengine. Hivyo, tunaweza kusema kwamba Rusuli wote walikuwa ni wacha wa Allaah.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ﴿١٣﴾
Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana namwanamme na mwanamke, na Tukakujaalieni mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye na hadhi zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni mwenye taqwa zaidi kati yenu. Hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Al-Hujuraat: 13]
Imesimuliwa na Abu Dharr kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwambia: "Nyinyi sio wabora kuliko watu wenye ngozi nyekundu au nyeusi isipokuwa pale mutakapowazidi kwa uchaji wa Allaah." [Imepokewa na At-Tirmidhiyy]
Sifa kubwa ya Masufi wa sasa ni kuwa na "mapenzi" kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi waaalihi sallam) sana hadi wanajihusisha na shirki pamoja na mapenzi haya. Hata hivyo, sio sahihi kuwa na kiwango hicho cha mapenzi pale inaposababisha kuchupa mipaka na kuingiza uasi.
'Iyd Mbili Zinachukua Nafasi Ya Sikukuu Zote
Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anaeleza ya kwamba alipohama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah walikuwa na siku mbili walizokuwa wakicheza ndani yake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Hakika Allaah Aliyetukuka Amewabadilishia siku zilizo bora kuliko hizo – Siku ya Fitr ('Iydul Fitwr baada ya kufunga mwezi wa Ramadhwaan) na Siku ya Adh-haa ('Iyd kubwa ya baada ya Hijjah)" [Imepokelewa na Abu Daawuud]
Fatwa Kutoka Kwa Shaykh Bin 'Uthaimiyn[1]
Mwanachuoni mkubwa Muhammad Swaalih bin 'Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) aliulizwa kuhusiana na sherehe za kuzaliwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambapo alijibu:
Kwa kuanzia, siku haswa ya kuzaliwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haijulikani kwa uhakika. Isipokuwa, wachunguzi wa sasa wamethibitisha kwamba alikufa tarehe 9 ya Rabi'ul Awwal na sio tarehe 12 (kama inavyoaminika sana), na hivyo hakuna msingi wa historia kwa kunasibisha tarehe 12 na sherehe.
Tukienda mbali zaidi, sherehe hizi hazina msingi ndani ya mafunzo ya diyn, kwani kama ingeshurutishwa, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliifanyia kazi au kuliamrisha ummah wake kufanya hivyo. Kama angekuwa amefanya au ameamrisha taifa lake kufanya hivyo, ingekuwepo na (kila) sababu ya kuiendeleza, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amesema:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijri: 9]
Kwa vile (jambo) hili halijasimuliwa, tunakuja kufahamu kwamba halijatokana na diyn ya Allaah. Kama sio kutokana na diyn ya Allaah, basi hapana ruhusa kwetu sisi kumuabudia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuomba kuwa karibu Naye kwa mtindo huu. Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ametuwekea njia malumu kwetu kuifuata ili kupata Radhi Zake, ambayo pia ni njia ya Mjumbe wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwa nini iruhusike kwetu sisi, wakati sisi ni waja tu, kutengeneza njia nyengine inayopelekea kwenye Radhi za Allaah kutokana na nafsi zetu wenyewe (yaani sio iliyoshushwa)? Hakika ni uasi dhidi ya Haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuweka Sheria ndani ya diyn Yake ambayo sio sehemu ya hilo. Juu ya hivyo, hili linaingiza ukanushaji wa yale Aliyoyasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndani ya Qur-aan:
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]
Iwapo sherehe hizi zimetokana na Ukamilifu wa Diyn, basi ni lazima itakuwa ilikuwepo kabla ya kifo cha Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kama haitokani na Ukamilifu wa Diyn, basi haiwezekani kwamba ikawa inatokana na diyn, kwani Allaah Amekwisha sema: "Leo Nimekukamilishieni Diyn yenu". Yeyote anayedai kwamba ni sehemu ya Ukamilifu wa Diyn iliyotokea baada ya kifo cha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi dai lake linapelekea kukana Aayah hii ya Qur-aan. Bila ya shaka yoyote kuwa wale wanaosherehekea kuzaliwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wanapendelea kuongeza mambo, kukithirisha kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kuonesha mapenzi kwake yeye, na kuzidisha hisia zao ili kudhihirisha yaliyomo ndani ya nyoyo zao kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Matendo yote haya ni matendo ya ibada. Mapenzi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ibada ambayo inahitajika kwa ajili ya iymaan, kwani iymaan ya mtu haikamiliki hadi ampende Nabiy kuliko nafsi yake, mtoto wake, baba yake, na viumbe vyote. Kupamba ibada, kuiga matendo na kumswalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yote ni matendo ya ibada na yanatokana na diyn, kama ilivyo kuonesha hisia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa vile (matendo hayo) yanamkaribisha mja kwa diyn ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Kinachofuata hapo ni kwamba sherehe za kuzaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa lengo la kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kumswalia Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanatambulika kama ni matendo ya ibada, na kwa vile ni matendo ya ibada basi hakuna ruhusa ya kuzusha chochote kipya ndani ya diyn ambacho hakina mnasaba. Hivyo, sherehe za kuzaliwa ni uzushi na zinazuiwa. Pia, tunasikia ripoti kadhaa kwamba sherehe hizi zina matendo mengi yasiyofaa ndani yake, ambayo sio ya diyn, hisia za mtu, wala mtu yeyote mwenye akili timamu atayafanya kuyaruhusu. Wanaimba nyimbo na mashairi ambayo yanaenda mbali kabisa dhidi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), mbali zaidi hadi kumtukuza kuliko Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na hifadhi haiombwi isipokuwa kwa Allaah. Pia tunasikia kuhusu ujinga wa baadhi ya washiriki, kwamba pale msomaji anaposimulia hadithi ya kuzaliwa kwake na kufikia sehemu ya kutoka tumboni mwa mama yake, wote wanasimama pamoja kwa heshima wakisema na kuamini kwamba roho na karama zake za Rasuli wa Allaah, zimehudhuria pamoja nao kwenye sherehe, na kwamba wanasimama bila ya desturi malumu. Hili hakika ni wazimu na ushirikina ulio wazi. Pia, sio mnasaba kumsimamia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa vile alikuwa halipendelei hilo. Swahaaba, waliokuwa wakimpenda na kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko mtu mwengine yeyote, katu hawatomsimamia pale akiwa yuhai pamoja nao kwa kukasirika kwake (kutokana na jambo hilo), basi ni ujinga ulioje wa ushirikina huu usiokuwa na msingi wowote?
Sherehe za kuzaliwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni uzushi mkubwa usiopata kutokea hadi baada ya vizazi vitatu vya wacha wa Allaah baada ya kifo cha Rasuli wa Allaah, na ni sherehe iliyojaa mambo yasiyopendeza na ya kiajabu ambayo yanapingana na msingi wa diyn ya Kiislamu, baya zaidi ni mchanganyiko na mwingiliano wa wanaume na wanawake pamoja ndani ya eneo moja (pamoja) na (kuwepo kwa) matendo mengi yasiyokubalika.
[1] Majmuu’ Fataawaa, Muhammad bin Swaalih al-'Uthaymiyn juz. 2/ uk.297-300