Baba Aliyemzaa Nje Ya Ndoa Ana Haki Kumfanyia Ihsaan?

SWALI:

 

Assalam alaikum.

Kwa ufupi tu swali langu ni kuhusu kuwatunza wazee wawili yaani baba na mama, swali langu liko hapa jee ikiwa wewe mtoto umezaliwa nje ya ndoa na baba yule ulipozaliwa hakukushughulikia wala hakukujuwa mpaka umekuwa mtu mzima, yaani maisha yote ulikuwa katika malezi ya mzazi mmoja yaani ni mama. Halafu ukaja ukaambiwa wewe baba yako ni fulani na ukawasiliana na yule baba na akakiri kama kweli wewe ni mwanawe... je una haki ya kuwashughulikiwa wote wawili?? Au haki yako ni kumtazama mzazi mmoja tu ambae nini mama aliyepata taabu na wewe? Naomba kwa ukarimu wenu nijulisheni swali hili maana linanitatiza kweli kweli..

Asanteni..


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumtazama baba yako wa nje ya ndoa. Hakika Uislamu kupitia Qur-aan na Sunnah umetuhimiza sana kuwafanyia wema wazazi wawili na hasa wakiwa wakongwe. Mama ana daraja kubwa zaidi kuliko baba kwa hali yoyote ile. Kisheria wewe umewajibika kumtazama mama yako hasa kwa kuwa alikutazama peke yake wakati u mchanga bila ya usaidizi kutoka kwa aliyemfanya upatikane kwa njia ya haramu.

 

Tufahamu kuwa kisheria huyo si baba yako, huwezi kumrithi wala hawezi kukurithi kwa hali yoyote ile. Kwa hivyo si baba yako kisheria mbali na kuwa kibinaadamu ni damu yako. Kisheria pia inafaa uvae hijaab mbele yake. Ikiwa utamsaidia itakuwa ni msaada wowote ule ambao utamsaidia Muislamu mwengine. Utapata thawabu ya kumsaidia Muislamu na sio ya kumtazama baba mzazi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share