Mama Yetu Hataki Kuchukua Urithi Wa Baba Yetu Aliyefariki

SWALI:

 

Assalam alaikum.

 

Mimi ni kijana ambaye nimefiliwa na baba yangu tangu mwaka 2004, lakini kwa bahati mbaya kwa kipindi hicho chote mpaka leo hatujafanya urithi, sisi watoto tumeamua zile mali alizoacha baba yetu tumeamua tuzifanye kama za ushirika. Sasa mama yetu inatubidi tumpe urithi wake, kwa bahati mbaya muda wote tulikuwa hatuna uwezo wa kumpa urithi wake kwa sababu tulikuwa tunataka kupiga thamani ya vitu vyote alivyoacha baba yetu halafu kufanya mahesabu kwa ajili ya kumpa urithi mama yetu, lakini sasa mungu katujaalia tumepata uwezo wa kumpa urithi wake. Swali langu ni hapa tulipomwambia huyo mama yetu kutaka kumpa urithi wake alisema yeye hataki chochote kutoka huo urithi, jee sheikh kwa hili sheria ya kiislam inasemaje ikitokea hali hii, Jee bado tuna jukumu kwa mungu kwa kuwa hatujampa urithi kwa kusema hataki kuchukua urithi huo kutoka kwa mumewe?


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu urithi wa mama mzazi.

Kwa hakika ndugu yetu kulingana na swali lako inaonyesha mlikosa busara ya kuweza kutaka kumgawia mama yenu mzazi urithi wake ambao ni thumuni (1/8) kutoka kwa mumewe. Njia iliyotumiwa pia si ya heshima kwa mama yenu mzazi ambaye mlifaa kutumia njia nzuri na ya upole.

 

Mwanzo ilikuwa ni makosa kungojea kwa muda wa miaka 4 mpaka mkaamua sasa mgawe urithi huo na kumpa mama yenu. Na pia sijui ilikuwaje katika vikao vya kutaka kushirikiana hamkumuita mama yenu naye akatoa mchango wake kuhusu ushirikiano huo. Ilikuwa ni busara kwenu zaidi kumshirikisha mama yenu katika mazungumzo hayo ambayo huenda naye angewapatia ushauri mwema zaidi kwani yeye pia ana haki ya mali hiyo kama nyie.

 

Jibu la mama yenu hilo ni kama amehisi kuwa hamkumpatia heshima ya kutosha anayostahiki kutoka kwenu vijana wake. Ushauri wetu kuhusu hilo ni kuwa jaribuni tena kumshirikisha na kutaka mawazo yake kwa njia bora ambazo mnaweza kuzitumia ili kurekebisha hayo yaliyopita. Pia ikiwa nyie mmefanya ushirika kati yenu kwa kuvikodisha viwanja au nyumba zenu, mnaweza kila mnapopata kodi mkamgawia naye sehemu yake ya urithi.

 

Lau ikiwa ameshikilia kuwa hataki chochote katika mirathi ya mumewe hiyo ni haki yake kwani yeye mwenyewe ana haki hiyo. Kwa hivyo, kwa njia hiyo sehemu yake ya urithi itagawiwa kwa warithi wake ambao ni nyie vijana wake. Ikiwa ameshikilia kabisa rai yake hiyo nyie hamtakuwa na jukumu mbele ya Allaah Aliyetukuka lakini rekebisheni njia zenu na InshaAllaah kutapatikana suluhisho muafaka.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share