Maulidi: Shaykh Fawzaan: Hukumu Ya Kusherehekea Kuzaliwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
Hukumu Ya Kusherehekea Kuzaliwa Kwa Nabiy
(Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Shaykh Duktuwr Swaalih Al-Fawzaan
Imetafsiriwa Na: Naaswir Haamid
Himdi ni Zake Allaah Rabb wa walimwengu, na rahmah na amani ziwe juu ya Nabiy wetu Muhammad na watu wake wa nyumbani na Swahaba zake wote.
Amri zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah katika kufuata sheria za Allaah na Rasulil Wake, na makatazo ya kuingiza uzushi ndani ya diyn yapo wazi. Allaah Anasema:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-'Imraan: 31]
Na Anasema pia Allaah (‘Azza wa Jalla):
اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٣﴾
Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Rabb wenu na wala msifuate badala Yake marafiki walinzi. Ni machache mnayoyakumbuka. [Al-A'raaf: 3]
Na pia:
وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾
“Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa.” [Al-An'aam: 153]
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Maneno bora ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika diyn) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni motoni)). Na amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Yeyote anayenizushia kitu ndani ya jambo letu hili (Uislamu), atarudishiwa mwenyewe.)) [Imepokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Miongoni mwa mambo maovu yaliyozushwa na watu ni sherehe ya kuzaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndani ya mwezi wa Rabi'ul-Awwal. Wanaadhimisha sherehe hii katika njia tofauti.
Baadhi yao wanafanya mkusanyiko wa kukusanyika katika kusoma Siyrah ya Mawlid, risala na qasiydah katika kuadhimisha huku.
Wengine wanatengeneza vyakula na peremende na kadhalika, na kuwapatia watu kama ni zawadi.
Baadhi yao wanaadhimisha sherehe hizi Misikitini, na wengine majumbani mwao.
Wengine wala hawajiwekei kiwango kwenye matendo yaliyotajwa hapo juu; haya yanahusisha katika mikusanyiko ya haramu na mambo maovu, kwa mfano mchanganyiko wa wanaume na wanawake, kucheza na kuimba, au kutenda matendo ya shirki kama vile kuomba msaada wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kumuita, kuomba msaada dhidi ya maadui zao na mengineyo.
Kwa namna yoyote na kwa nia yoyote itakayokuwa kwa wale wanaofanya haya, hakuna shaka yoyote kwamba jambo hilo limezushwa, uzushi ulio haramu ulioanzishwa na Mashia (Faatwimiyyuun) baada ya karne tatu bora, kwa lengo la kuiharibu diyn ya Waislamu. Mtu wa mwanzo kufanya hili baada yao alikuwa ni mfalme al-Muzaffar Abu Sa'iyd Kawkabuuri, mfalme wa Irbil, mwishoni mwa karne ya sita au mwanzoni wa karne ya saba H, kama ilivyosimuliwa na wanahistoria kama vile Ibn Khalkaan na wengineo. Abu Shaamah amesema: mtu wa mwanzo kufanya hilo ndani ya Mosul alikuwa ni Shaykh 'Umar bin Muhammad al-Malaa, alitambulika kuwa ni miongoni mwa wachaji Allaah maarufu. Baadaye mtawala wa Irbil na wengineo wakafuatia mfano wake.
Al-Haafidh bin Kathiyr amesema ndani ya al-Bidaayah wan-Nihaayah (13/137), katika wasifu wa Abu Sai'yd Kawkabuuri: "Alikuwa na kawaida ya kuadhimisha Mawlid ndani ya Rabi'ul-Awwal na kufanya sherehe kubwa katika kuadhimisha huko… baadhi ya waliokuwa wakihudhuria katika karamu kubwa ya al-Muzaffar katika baadhi ya maadhimisho ya Mawlid wamesema kwamba alikuwa akiwakirimu karamu ya kondoo alfu tano waliochomwa, kuku alfu kumi na majungu makubwa mia moja, na sinia thelathini za peremende… alikuwa akiwapatia nafasi ya Masufi kuimba kuanzia Adhuhuri hadi Alfajiri, na yeye mwenyewe akicheza pamoja nao.
Ibn Khalkaan amesema ndani ya Wafiyaat al-A’yaan (3/274): "Inapofika mwanzo wa mwezi wa Swafar walikuwa wakipamba majengo hayo kwa aina tofauti za marembo, na katika kila jengo likikaa kundi la waimbaji na kundi la waitikiaji na watumiaji wa ala za muziki, na walikuwa hawaondoki katika jengo lolote hadi pale wanapoanzisha hapo kundi (la wachezaji).
Watu wakiachana na kufanya kazi katika kipindi hichi, na walikuwa hawafanyi kazi isipokuwa kuzunguka na kuangalia burudani hizo. Katika kipindi cha siku mbili za Mawlid zinapofika, wanawatoa ngamia, ngo'mbe na kondoo, kwa idadi kubwa bila ya kuelezeka, na wanakuwa nao (hao wanyama) pamoja wakiwa na ngoma zao, nyimbo na ala za muziki, hadi wanapowafikisha wanyama hao katika sehemu watakayoonekana vyema… Katika usiku wa Mawlid kuna waimbaji wa Nashiyd baada ya Magharibi ndani ya ngome.
Hii ndio asili ya sherehe hizi za kuadhimisha kuzaliwa kwa Nabiy. Siku hizi, kumekuwa na burudani za kijahili, israfu, na kupoteza pesa na wakati. Matendo ambayo yameshirikishwa katika uzushi ambao Allaah Hajauteremsha kwa mamlaka yoyote.
Jambo ambalo Waislamu wanatakiwa kufanya, ni kuirudisha Sunnah na kuondosha bid'ah (uzushi); hawatakiwi kufanya tendo lolote hadi watakapoelewa hukumu ya jambo hilo.
Hukumu Ya Kusherehekea Kuzaliwa Kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kunazuiliwa na jambo hilo likataliwe kwa sababu nyingi:
1 – Mawlid si sehemu ya Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Makhalifa waliomrithi yeye. Kwa kesi hii, basi ni uzushi unaozuiwa, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Habash. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh].
Kusherehekea Mawlid ni uzushi ulioanzishwa na Shia Faatwimiyyuun baada ya karne tatu bora kabisa kwa lengo la kuharibu diyn ya Waislamu. Iwapo mtu atafanya jambo lolote kwa lengo la kujikurubisha kwa Allaah ambalo hakupatapo kulifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au kuliidhinisha, na halikufanywa na Makhalifa waliomrithi, tendo hili lina maana kwamba anamzulia Nabiy kwa kutofafanua diyn kwa watu, na kwamba Nabiy haamini maneno ya Allaah:
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]
Kwa sababu anaingiza jambo la ziada na kudai kwamba ni sehemu ya diyn, lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakulileta jambo hili.
2 – Kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wigo wa Wakristo, kwa sababu wanasherehekea kuzaliwa kwa Masiyh (‘Alayhis Salaam). Ni makosa makubwa kuwaiga na ni haramu. Hadiyth inatwambia kwamba hairuhusiwi kuwaiga makafiri, na tunaamrishwa kujitofautisha nao. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote anayeiga watu ni mmoja wao.)) [Imesimuliwa na Ahmad]. Na pia amesema: ((Kuweni tofauti na mushrikiyn.)) [Imepokelewa na Muslim] – haswa kwa mnasaba wa mambo ambayo ni alama au mila za diyn yao.
3 – Achilia mbali ya kwamba ni bid'ah na ni wigo wa Wakristo, ambapo yote ni haramu, kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni njia inayopelekea katika kuchupa mipaka na kufuru katika kumsifu, na inakwenda mbali hadi kumuita (kumuomba du'aa) na kuomba msaada wake, badala ya kumuomba Allaah, kama inavyofanyika sasa miongoni mwa wengi wanaoadhimisha bid'ah hii ya Mawlid, pale wanapomuomba Nabiy badala ya Allaah, na kuomba msaada wake, na kuimba Qaswiydah za shirki za kumsifu, kama vile Qaswiydah al-Burdah na nyenginezo.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuchupa mpaka katika kumsifu, kwani amesema: ((Msinitukuzekama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi na mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]. Yaani musichupe mpaka kama Wakristo walivyochupa mipaka katika kumsifu Masiyh na kumtukuza hadi wakawa wanamuabudia yeye badala ya Allaah. Allaah Amewakataza kufanya hivyo pale Anaposema:
يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ وَلَا تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ ۚ إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّـهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ ۖ
Enyi Ahlal-Kitaabi! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Allaah isipokuwa ukweli. Hakika Al-Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam ni Rasuli wa Allaah na ni neno Lake (la Kun!) Alompelekea Maryam na Ruwh (roho Aliyoumba kwa amrisho) kutoka Kwake. [An-Nisaa: 171]
Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuzuia kumsifu sana kupita mpaka kwa kuhofia kutokezea kama yale yaliyowapata wao, amesema: ((Epukeni na kuchupa mipaka, kwa hakika wale waliokuja kabla yenu waliangamizwa kwa sababu ya kuchupa mipaka.)) [Ameisahihisha al-Albaani katika Swahiyh Sunan an-Nasaaiy]
4 – Kuadhimisha uzushi wa kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy kunafungua mlango wa aina nyenginezo za bid'ah na kuharibu Sunnah. Hivyo, unakutia kwamba wazushi wapo mbele sana linapokuja suala la bid'ah na wavivu katika suala la Sunnah; wanaichukia na wanatambua kwamba wale wanaofuata ni adui, hadi pale diyn yao yote iwe na mambo ya uzushi na Mawlid. Wamegawa makundi tofauti, kila moja likiwa na maadhimisho ya kuzaliwa imamu, kama vile kuzaliwa kwa al-Badawi, Ibn 'Arabiy, al-Dasuuqiy na ash-Shaadhiliy. Kabla ya kumaliza sherehe moja wanachupia kusherehekea nyengine. Hili linapelekea katika kuchupa mipaka kuhusiana na watu hawa waliokufa na wengineo, na kuwaomba badala ya kumuomba Allaah, wakiamini kwamba watanufaika lakini watakutana na madhara mabaya kama vile kuibadili diyn ya Allaah na kurudi enzi za kale za diyn ya Jaahiliyyah ambazo Allaah Amesema:
وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ ۚ
Na wanaabudu pasi na Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” [Yuwnus: 18]
Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):
أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ
Tanabahi! Ni ya Allaah Pekee Dini iliyotakasika; na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha karibu kabisa kwa Allaah” [Az-Zumar: 3]
Mjadala Wa Hoja Zisizokuwa Na Mashiko Wa Wale Wanaosherehekea Mawlid
Wale wanaodhani kwamba bid'ah hii iendelezwe wanaleta hoja za uongo ambazo ni nyepesi kuliko unyuzi wa buibui. Hoja hizi za uongo zinaweza kujadiliwa kama ifuatavyo:
1 – Dai lao la kwamba jambo hili ni la kumtukuza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Jibu ni kwamba, njia ya kumtukuza ni ya kumtii, kufanya kama ambavyo ameamrisha na kujiepusha na yale aliyoyakataza, na kumpenda yeye; haihusiani na kumtukuza kupitia mambo ya uzushi, ya kutunga au madhambi. Kusherehekea kuzaliwa kwake ni aina hii ya kulaumiwa kwa sababu ni dhambi. Watu waliokuwa wakimtukuza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zaidi walikuwa ni Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum), kama vile 'Urwah bin Mas'uud aliposema kuwaambiwa Maquraysh: "Enyi watu, ninaapa kwa Allaah kwamba nimewatembelea wafalme. Nimeenda kwa Kaizar, Kosros na Nigas, lakini kwa Allaah sijapata kuona mfalme ambaye wafuasi wake wanamtukuza zaidi kuliko Maswahaba wa Muhammad wanavyomtukuza Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Naapa kwa Allaah, pale anapotema mate hayaanguki ardhini, isipokuwa yanaangukia juu ya mkono wa Swahaba zake, baadaye wanapangusia nyuso zao na ngozi zao. Iwapo amewaamrisha kufanya kitu, hawataacha kufanya kama alivyoamrisha. Anapotia wudhuu, wanakaribia kupigana kwa kugombea maji yake. Wanapozungumza wanazishusha chini sauti zao mbele yake; na walikuwa hawamuangalii macho kupe kwa heshima zao juu yake." [Al-Bukhaariy].
Juu ya kiwango cha kumtukuza hivi, hawakupatapo kuifanya siku ya kuzaliwa kwake kama ni 'Iyd (sikukuu). Iwapo hilo limeelezwa ndani ya Uislamu, wasingeacha kulitenda.
2 – Kutumia ushahidi wa kwamba watu wengi katika nchi nyingi wanafanya hili.
Jibu ya hilo ni kwamba ushahidi unahusisha lile ambalo limekubaliwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na lililokubaliwa kutoka kwa Nabiy ni kwamba mambo ya uzushi yanazuiwa moja kwa moja, na hili ni jambo la uzushi. Wanayofanya watu, iwapo linakwenda kinyume ya ushahidi (dalili), halithibitishi lolote, hata kama wengi wao watalitenda. Anasema Allaah ('Azza wa Jalla):
وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾
Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah. Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo. [Al-An'aam: 116]
Kwa upande mwengine, katika kila zama, sifa zote zimwendee Allaah, kunakuwa na watu wanaopinga bid'ah hii na kueleza waziwazi kwamba ni uongo. Wale wanaosisitiza kulitenda baada ya ukweli wameelezwa kwamba wamekosa uthibitisho.
Miongoni mwa walioporomosha sherehe za maadhimisho haya alikuwa ni Shaykh al—Islaam bin Taymiyah ndani ya Iqtidhwaa' as-Swiraat al-Mustaqiym; Imaam as-Shaatwibiy ndani ya al-'I'tiswaam; Ibn al-Haaj ndani ya al-Madkhal; Shaykh Taaj ad-Diyn 'Aliy bin 'Umar al-Lakhami aliyeandika kitabu kizima kukataa maadhimisho haya; Shaykh Muhammad Bashiyr as-Sahsawaaniy al-Hindi ndani ya kitabu chake cha Swiyaanah al-Insaan; as-Sayyid Muhammad Rashiyd Ridhwaa ameandika kuhusiana na mada hii; Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal ash-Shaykh aliyeandika katika hili; Shaykh 'Abdul-'Aziyz bin Baaz; na wengineo wanaoendelea kuandika na kukataa bid'ah hii kila mwaka ndani ya kurasa za magazeti na majarida, kipindi kile bid'ah hii inapoadhimishwa.
3 – Wanasema kwamba kwa kusherehekea Mawlid wanahuisha kumbukumbu za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Jibu la hili ni kwamba kumbukumbu za kuwepo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinaendelea kuhuishwa na Waislamu, kwa mfano pale jina lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) linapotajwa ndani ya Adhaana na Iqaamah na kwenye Khutbah, na kila wakati Muislamu anaposoma Shahaadatayn baada ya kutia wudhuu na ndani ya Swalah, na kila wakati anapomswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maombi yake na anapotajwa, na kila wakati Muislamu anapofanya tendo aliloamrishwa (wajibu) au lililopendekezwa (mustahabb) miongoni mwa yale aliyoyaeleza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Katika njia zote kama hizo, Muislamu anamkumbuka na malipo sawa ya mtendaji yanamrudia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, Muislamu anaendelea kuhuisha kumbukumbu za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na anaungana naye usiku na mchana maisha yake yote kupitia yale ambayo Allaah Ameyaeleza, sio tu katika siku ya Mawlid na mambo ambayo ni ya bid'ah na yanayokwenda kinyume na Sunnah, kwani hayo yanamuweka mbali na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Nabiy atamkataa kwa sababu hiyo.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hana haja ya sherehe za kuzusha kama hizi, kwa sababu Allaah Ameshamtukuza na kumpa heshima juu yake, kama Alivyosema:
وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ ﴿٤﴾
Na Tukakutukuzia kutajwa kwako? [Ash-Sharh: 4]
Kwani Allaah Hatajwi ndani ya Adhaana, Iqaamah au Khutbah, isipokuwa mbele yake atatajwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); hili latosha kumtukuza, kumpenda na kuhuisha kumbukumbu zake, na linatosha kuwa ni hamasa ya kumfuata.
Allaah Hakutufikishia kusheherekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndani ya Qur-aan, isipokuwa Ametufikishia ujumbe Wake, na Anasema:
هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِّنْهُمْ
Yeye Ndiye Aliyepeleka Rasuli kwa wasiojua kusoma wala kuandika miongoni mwao [Al-Jumu'ah: 2]
4 - Wanaweza kusema kwamba sherehe ya kuzaliwa Nabiy ilianzishwa na watu wenye elimu na mfalme aliyeazimia kutokana na jambo hilo kuwa karibu na Allaah.
Jibu letu kwa hilo ni kwamba bid'ah hairuhusiki, kwa yeyote anayeitenda. Dhana nzuri haiwezi kuwa ni ruhusa ya tendo baya na hata kama mtu atakufa akiwa ni mwenye elimu na mwenye kuheshimika, hili halina maana kwamba alikuwa ni mkamilifu.
5 – Wanasema kwamba kusherehekea Mawlid inaangukia chini ya mada ya bid'ah hasanah ("uzushi mzuri") kwa sababu msingi wake ni kutoa shukurani kwa Allaah kwa ajili ya Nabiy!
Jibu letu kwa hilo ni kwamba hakuna uzushi ulio mzuri. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote anayezua jambo ambalo sio letu (Uislamu), ambalo sio sehemu ya hilo, litakataliwa.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]. Na amesema: ((Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh]. Hukumu ya uzushi ni kwamba yote ni yenye kupotosha, lakini hoja hii isiyo na ukweli inashauri kwamba sio kila bid'ah inapelekea njia ovu, kwani kuna uzushi mzuri.
Al-Haafidh bin Rajab amesema ndani ya Sharh al-Arba'iyn: "Maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), 'kila bid'ah ni upotofu' ni ya jumla lakini yenye maelezo maalumu inayohusisha kila kitu; ni mojawapo ya kanuni muhimu ya msingi wa diyn. Ni mfano wa maneno: ((Yeyote anayezua jambo ambalo sio letu (Uislamu), ambalo sio sehemu ya hilo, litakataliwa.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]. Yeyote anayezua jambo na kulihusisha na Uislamu hali ya kuwa halina msingi wa diyn, hili linapelekea kwenda kwenye upotofu na halina mnasaba wowote na Uislamu, iwapo hilo litanasibishwa na mambo ya imani ('Aqiydah) au maneno na matendo ya dhahiri au siri." (Jaami’ al-‘Uluum wal-Hikam, uk. 233)
Watu hawa hawana ushahidi wowote kwamba kuna jambo la "uzushi mzuri" isipokuwa kwa maneno ya 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuhusiana na Swalah za Taraawiyh: "Hili ni jambo zuri kabisa lilozushwa." [Swahiyh al-Al-Bukhaariy
Pia wanasema kwamba kulikuwa na mambo yaliyozushwa ambayo Salaf hawajayakataa, kwa mfano kukusanya Qur-aan katika msahafu na kuandika na kukusanya Hadiyth.
Jibu kwa hilo ni kwamba, mambo haya yana msingi wa Uislamu, hivyo sio mambo mapya yaliyozushwa.
'Umar amesema: "Hili ni jambo zuri kabisa lilozushwa." Likiwa na maana ya kilugha, sio katika Shari'ah. Lolote lenye msingi wa Uislamu, iwapo limetambuliwa kuwa ni uzushi, ni uzushi kilugha, sio katika Shari'ah, kwa sababu uzushi ndani ya Shari'ah una maana ya lile lisilo na msingi wa Uislamu.
Kukusanya Qur-aan katika kitabu kimoja lina msingi wa Uislamu, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwisha amrisha Qur-aan kuandikwa, lakini ilitapakaa sehemu mbali mbali, hivyo Swahaba wakaikusanya katika msahafu ili kuilinda na kuitunza.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewaongoza Swahaba katika swala za Taraawiyh kwa muda, baadaye akasimamisha kufanya hilo, isije ikaja kuwa ni wajibu juu yao. Swahaba Radhwiya Allaahu ‘Anhum) waliendelea kuswali mbali mbali wakati wa uhai wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia baada ya kifo chake, hadi 'Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alipowakusanya nyuma ya Imaam mmoja kama walivyokuwa wakifanya nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hili sio uzushi uliobuniwa ndani ya diyn. Kuiandika Hadiyth pia lina msingi wa Uislamu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha kwamba baadhi ya Ahaadiyth kuandikwa kwa baadhi ya Swahaba pale walipomuomba. Kwa ujumla, kuweka tu katika maandiko kulikuwa hakuruhusiwi wakati wa uhai wake, kwa khofu ya kuichanganya Qur-aan na vitu visivyohusiana navyo. Pale Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki, khofu hii haikuwa ni kikwazo, kwa sababu Qur-aan imekwishakamilika na kupangwa vizuri kabla ya kufa kwake.
Waislamu waliikusanya Sunnah baadaye ili kuihifadhi na kuizuia isije kupotea. Tunamuomba Allaah Awapatie malipo mema kwa niaba ya Uislamu na Waislamu, kwa sababu wamehifadhi Kitabu cha Rabb wao na Sunnah ya Nabiy wao (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na kupotea au kuharibiwa.
Pia tunaweza kuwaambia: kwanini tendo hili la kutoa shukurani, kama wanavyoliita, halikufanywa na vizazi bora, Maswahaba, Matabiina na wafuasi wa Matabiina, waliompenda zaidi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na walikuwa na shauku ya kutenda mema na kutoa shukurani? Je wale walioanzisha uzushi wa Mawlid ndio wa kuheshimiwa zaidi kuliko wao? Je, wao wanatoa shukurani zaidi kwa Allaah? Hakika hapana!
6 – Wanaweza kusema kwamba kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni dalili ya kuonesha mapenzi kwake; hii ni njia mojawapo ya kuonesha kwamba, na kuonesha mapenzi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inavyoelezwa ndani ya Uislamu!
Jibu kwa hilo ni kwamba hakuna shaka yoyote kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni faradhi kwa kila Muislamu; ampende zaidi kuliko nafsi yake, mtoto wake, baba yake na watu wote – baba yangu na mama yangu waweza kuwa ni kafara kwa ajili yake – lakini hilo halina maana kwamba tuzue mambo kwa kufanya yale yasiyoelezwa kwetu. Kumpenda yeye kunamaanisha kwamba tumtii na tumfuate, kwani hilo ni miongoni mwa sera ya juu ya mapenzi, kama ilivyosemwa:
"Kama mapenzi yake ni ya kweli basi mtii; kwani mwenye kupenda anamtii yule anayempenda."
Kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inamaanisha kuhuisha Sunnah yake, kushikamana nayo barabara, kuepukana na maneno na matendo yanayokwenda kinyume na Sunnah. Hakuna shaka yoyote kwamba kile kinachokwenda kinyume na Sunnah ni kosa la uzushi (bid'ah) na tendo la uasi. Dhana nzuri ina maanisha kwamba inaruhusika kuingiza uzushi ndani ya diyn. Uislamu umeegemezwa katika mambo mawli, usafi wa Niyah na kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Anasema:
بَلَىٰ مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَلَهُ أَجْرُهُ عِندَ رَبِّهِ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿١١٢﴾
Ndio! Bali yeyote aliyeusalimisha uso wake kwa Allaah, na ilhali yeye ni mwenye kufanya ihsaan basi atapata ujira wake kwa Rabb wake, na wala haitokuwa khofu juu yao wala hawatohuzunika. [Al-Baqarah: 112]
Kuelekeza uso wa mtu kwa Allaah ina maana kwamba kuwa mtiifu mbele ya Allaah, na kumfanyia matendo mema ina maana ya kumfuata Nabiy na kutekeleza Sunnah.
7 – Hoja yao nyengine isiyokuwa na mashiko ni pale wanaposema kwamba kwa kusherehekea Mawlid na kuisoma Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maadhimisho haya, wanashajiisha watu kufuata mfano wake!
Tunawaambiwa kwamba kuisoma Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kufuata mfano wake ni mambo yanayotakiwa kufuatwa wakati wote, mwaka mzima na kipindi chote cha maisha yake. Kuiweka siku maalumu kwa ajili ya hilo bila ya ushahidi kwa kufanya hivyo ni uzushi, na kila uzushi unapelekea katika upotovu. Bid'ah haitoi matunda yoyote isipokuwa mambo maovu na inapelekea mtu kujiweka mbali ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kwa kuhitimisha, kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa namna yoyote itakayokuwa, ni jambo la uzushi. Waislamu wanatakiwa kusitisha hili na aina nyengine yoyote ya bid'ah, na kujiweka karibu kwa kuihuisha na kuisimamisha Sunnah.
Wasihadaike na wale wanaohamasisha na kutetea bid'ah hii, kwani watu kama hawa wanapendelea zaidi kuhuisha mambo ya uzushi kuliko kuhuisha Sunnah; wanaweza hata wasijali kuhusiana na Sunnah hata kidogo. Yeyote aliyekuwa mfano wa hili, hakuna ruhusa ya kumuiga au kufuata mfano wake, hata kama wengi wa watu ni kama hawa.
Tunachotakiwa kufuata, ni mfano wa wale waliofuata njia ya Sunnah, miongoni mwa Salafus Swaalih na wafuasi wao, hata kama ni wachache. Ukweli haupimwi na mtu anayeuzungumza, isipokuwa watu wanapimwa na ukweli.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Habash. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh].
Hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea ndani ya Hadiyth hii nini tufanye pale kunapoibuka maoni tofauti, kama alivyoeleza kwamba kila kinachokwenda kinyume na Sunnah yake, iwapo ni maneno au matendo, ni bid'ah, na kila bid'ah inapelekea kwenye upotofu.
Iwapo tunaona hakuna msingi wa kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), iwapo ndani ya ya Sunnah ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au ndani ya makhalifa waongofu, basi ni moja kati ya mambo mepya yanayozushwa, moja kati ya bid'ah inayowapelekea watu kupotea. Hii ni kanuni ambayo inatolewa ufafanuzi na Hadiyth hii na ndilo linalooneshwa katika Aayah:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾
Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi [An-Nisaa: 59]
Kurudi kwa Allaah ina maana ya kurudi kwenye Kitabu Chake, na kurudi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ina maana ya kurudi kwenye Sunnah baada ya kufariki. Qur-aan na Sunnah ni sehemu kuu ya marejeo pale tunapotokezewa na mgogoro. Ni wapi ndani ya Qur-aan au Sunnah inaeleza kwamba imeruhusiwa ndani ya Uislamu kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy? Yeyote anayeona kwamba au kufikiria kwamba ni (jambo) zuri ni lazima atubu kutokana na hili na aina nyinginezo za bid'ah. Hii ndio tabia ya Muislamu anayetafuta ukweli. Lakini yeyote asiyekubali kubadilika na mkaidi baada ya kumthibitikia ukweli, basi mchezo wake utakuwa pamoja na Mola wake.
Tunamuomba Allaah Atusaidie kushikamana na Kitabu Chake na Sunnah ya Rasuli Wake hadi Siku tutakayokutana Naye. Allaah Ampe rahmah na amani Nabiy wetu Muhammad na watu wake na Maswahaba wake.
Huquwq an-Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bayna al-Ijlaal wal-Ikhlaal, uk. 139
Shaykh Duktuwr Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
Mjumbe wa Kamati ya Wanachuoni Wakuu, Saudi Arabia.