Rajab: Bid’ah Za Kujipeusha Nazo Katika Mwezi Wa Rajab Na Khaswa Tarehe 27
Bid’ah Za Kujipeusha Nazo Katika Mwezi Wa Rajab Na haswa Tarehe 27
1. Swawm siku hiyo ya tarehe 27 Rajab:
Imesemekana kuwa 'Umar alikuwa akiichapa mikono ya wale waliokuwa wamefunga mwezi wa Rajab mpaka walipofungua, na alikuwa akisema huu ni mwezi uliokuwa ukiheshimiwa sana wakati wa jaahiliyyah(kabla ya Uislamu). Na ulipokuja Uislam Ukaachwa.
[Majma'u Az-Zawaaid Mj. 3, uk. 194].
2. Du’aa maalum ambazo husomwa hasa wakati wa mwezi huu wa Rajab zote ni za kuzushwa; ni Bid’ah.
3. Kuzuru makaburi haswa kwenye mwezi huu wa Rajab ni Bid’ah kwa sababu makaburi yanapaswa kufanyiwa ziara muda na wakati wowote ule wa mwaka.
4. Swalaatur-Raghaaib (Swalaah Ya Ar-Raghaaib). Swalaah hii huswaliwa mwanzo mwa mwezi wa Rajab. Hakukujulikana Swalaah ya aina hii katika zama za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake watukufu wala kwa Watangu Wema (Salafus-Swaalih), bali ilikuja kuzushwa na kuwa maarufu katika zama hizo bora kupita.
‘Ulamaa wengi wakubwa wameikemea. Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaahu) amesema: “Swalaat Ar-Raghaaib ni bid’ah kwa mujibu wa maafikiano (Ijmaa’) ya Wanachuoni wa Dini. Kama Imaam, Maalik, Imaam Ash-Shaafi’iy, Imaam Abuu Haniyfah (Allaah Awarehemu wote) anasema kuwa Hadiyth iliyosimuliwa kuhusiana nayo ni Hadiyth mbovu na ya kuzushwa kwa mujibu wa kongamano la Wanachuoni mabingwa wa Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo ni bora Waislamu wakae nayo mbali na wakemee aina za bid’ah kama hizo zinazoenea katika jamii ya Kiislamu.
5. Swalaatu Ummi Daawuwd kwenye nusu ya Rajab.
6. Kuna madai baatwil kwamba matukio makubwa yametokea kwenye mwezi huu wa Rajab. Lakini hakuna mapokezi yoyote katika hayo yaliyokuwa ni sahihi.
Inadaiwa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa kwenye usiku wa mwanzo wa mwezi wa Rajab! Na kwamba alishushiwa Wahyi kwa mara ya kwanza kabisa kwenye tarehe 27 au tarehe 25 ya mwezi huu wa Rajab. Hakuna ushahidi wowote sahihi juu ya haya, na wala hakuna riwaayah iliyothibiti kuhusiana nayo.
Imaam Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema:
"Iliripotiwa kuwa ilikuwa katika mwezi wa Rajab kwamba kulikuwa na matukio makubwa, na hakuna hata moja ya hayo yaliyo sahihi. Ikasemwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa usiku wa kwanza, na kwamba alipewa Unabii siku ya ishirini na saba ya mwezi huo, na ikasemwa kuwa siku ya ishirini na tano, lakini hakuna kilichokuwa sahihi katika hayo.” [Latwaaif Al-Ma’aarif (290)].
Pia imepokewa katika Isnaad ambayo si sahihi kutoka kwa al-Qaasim bin Muhammad kwamba safari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya Israa na Mi’iraaj ilifanyika kwenye tarehe 27 ya mwezi wa Rajab. Madai kama hayo yamepingwa vikali na wanachuoni wengi.
7. Miongoni mwa bid’ah kubwa kubwa zinazofanyika kwenye mwezi huu ni usomaji wa Kisa cha Mi’iraaj na kusherehekea na kuadhimisha tukio hilo kwenye tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab, au kuutenga usiku huu kwa aina fulani fulani za ‘Ibaadah au kufanya ‘Ibaadah za ziada kama vile Qiyaam Al-Layl (kusimama kuswali usiku) au kufunga (Swawm) kwenye mchana wake. Vilevile kufanya sherehe kusherehekea.
Baadhi ya sherehe huambatana na mambo ya haramu kama vile kuchanganyikana wanaume na wanawake kuimba na kucheza miziki, mambo haya yote hayaruhusiwi hata kwenye zile sherehe kuu mbili za ‘Iyd (‘Iyd Al-Fitwr na ‘Iyd Al-Adhwhaa) ambazo ndizo zinazotambuliwa kisheria katika Uislamu na ambazo tumewekewa sheria nazo na Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sembuse ya sherehe hizi za kuzushwa ambazo hazina mashiko sahihi katika Uislamu. Mbali ya hilo hakuna Ushahidi wowote kwamba Israa na Miraji ilifanyika kwenye Mwezi Ishirini na saba ya Mwezi huu wa Rajab!
Hata kama itathibitishwa basi hakuna sababu iliyo wazi ya kuandaa sherehe kwenye siku hii kwa sababu hakuna mapokezi yoyote yaliyopokewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au kutoka kwa Maswahaba wake watukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) au kutoka kwa Watangu Wema (Salafus Swaalih) wa Ummah huu.
Kama hilo lingekuwa ni jambo zuri basi bila shaka wangalilifanya wao mwanzo kabla yetu sisi.
Basi kwa nini Muislamu ajitakie mashaka zaidi ya kufanya ‘Ibaadah isiyokuwa na dalili?
Kwa nini kwanza asitimize hizo ambazo tayari dalili zake ziko wazi?
Kama Muislamu anapenda sana ‘Ibaadah ya kufunga basi afunge Swawm ya Nabiy Daawuwd lakini wangapi wanaoweza kufanya ‘Ibaadah hiyo?
Juu ya hivyo kufuata bid'ah (uzushi) ni upotofu na kujitakia mtu mwenyewe kuwa na makazi mabaya siku ya Qiyaamah kama alivyoonya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار)) أخرجه مسلم في صحيحه
((Maneno bora ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi wa jambo jipya, na kila jambo jipya (katika Dini) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni upotofu, na kila upotofu unapeleka motoni)) [Muslim katika Swahiyh yake]
Tukinaike na yaliyo Swahiyh na tushukuru kuwa muongozo tulioletewa kwetu kutoka kwa Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) umekamilika na hatuja haja ya kujipa mashaka zaidi ya kufanya ‘Ibaadah za bid'ah wakati tunashindwa kutimiza zile tulizofaridhishiwa ambazo zimethibiti.
Tunatumai kwa maelezo hayo tuliyonukuu yatamtosheleza mwenye kutaka kufuata haki kwamba kuipwekesha siku ya tarehe 27 Rajab kwa ‘Ibaadah yoyote au kusherehekea kwa aina yoyote kwamba sio katika mafunzo ya dini, hiyo ni bid'ah ipasayo kuepukana nayo. Muislamu akipenda kufunga apate thawabu za uhakika afunge Jumatatu na Alkhamiys, au siku za Ayyaamul-Biydhw (Masiku meupe nayo ni tarehe 13, 14 na 15 katika kila mwezi), na Swawm ya Nabiy Daawuwd yaani siku afunge na siku aache.
Na pia mwezi wa Sha'abaan unakaribia ambao anaweza kufunga siku zozote atakazo bila ya kuipwekesha siku fulani maalum wala kuupa umuhimu wa nusu ya Sha'baan kwa kufunga na kuswali sana usiku. kama tunavyoona katika makala zifuatazo:
Mwezi Wa Rajab: Fadhila Zake Na Yaliyozuliwa Ndani Yake
Sha'abaan - Fadhila Zake Na Uzushi Wa Nisfu Sha'abaan
Na Allaah Anajua zaidi