Kila Uzushi Ni Upotofu, Hata Kama Watu Watauona Kuwa Ni Mzuri
Kila Uzushi Ni Upotofu, Hata Kama Watu Watauona Kuwa Ni Mzuri[1]
Imetayarishwa na Shaykh Saalim al-Hilaaliiy
Imetafsiriwa na Naaswir Haamid
Wanazuoni, Swahaba, Mataabi’iyna na Imaamu Waislamu waliofuata nyayo zao; ambao heshima zao zimethibitishwa, wote wanakubaliana kuhusu makosa ya bid’ah (uzushi) na madhara yake; na kwamba kila mtu anatakiwa ajiweke mbali na (kila) uzushi na yale yanayoungama nayo.
Hakuna shaka yoyote kuhusiana na (ukweli wa jambo) hili kutoka kwa yeyote miongoni mwao, wala kwa mwenye kukana hilo. Hivyo hapa kuna maelezo sahihi yaliyopokewa kutoka kwao, kama ni mifano ya maisha yao na matendo yaliyo wazi. Hivyo iwapo tutachukua baadhi ya mifano katika kiwango cha Swahaba, tunaona yale ambayo yanautuliza moyo wa yule mwenye hamu ya kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakati huo huo kukana mawazo ya wazushi:
'Abdullaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Fuata na wala usizue, kwani mumepewa yale ambayo yanayotosha (na kila uzushi ni upotofu.)”[2]
'Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Kila uzushi ni upotofu, hata kama watu watauona kuwa ni mzuri.”[3]
Na iwapo tutaangalia vitendo vyao tutaona kwamba walikuwa wakikubaliana moja kwa moja na maneno yao. Hivyo ‘Amr bin Salamah amesimulia: Tulikuwa tuna tabia ya kukaa mlangoni kwa 'Abdullaah bin Mas’uud kabla ya Swalah ya asubuhi, ili kwamba atakapotoka tufuatane naye hadi msikitini. Siku moja Abu Muusa Al-‘Ash’ariy alitujia na kusema: Je hajatoka bado Abu ‘Abdir-Rahmaan (yaani Ibn Mas’uud)? Tukajibu: Hapana! Hivyo alikaa chini pamoja nasi hadi alipotoka. Alipotoka nje sote tuliinuka pamoja naye, hivyo Abu Muusa alimwambia: Ee Abu ‘Abdir-Rahmaan! Nimeona jambo msikitini ambalo naamini kuwa ni ovu, lakini-shukrani zote ni za Allaah – sijaona chochote isipokuwa ni kizuri. Ibn Mas’uud akaulizia: “Nini umeona?”
Abu Muwsa akajibu: “Iwapo utaishi, basi nawe pia utaliona. Ndani kwenye Msikiti nimeona watu katika maduara wakisubiri Swaalah. Ndani ya kila duara kuna changarawe mikononi mwao na yupo mtu ambaye anawaambia: rudia Allaahu Akbar (Allaah ni Mkubwa) mara mia. Hivyo watarudia hilo mara mia. Baadaye atawaambia: rudia Laa ilaaha illa Allaah (Hakuna yeyote anayestahiki kuabudiwa pamoja na Allaah) mara mia. Hivyo watarudia mara mia. Baadaye atasema: sema Subhaana Allaah (Allaah Ametakasika na kasoro) mara mia. Hivyo watalitamka mara mia.” Ibn Mas’uud akauliza, “Uliwaambia nini?” Abu Muwsa akasema, “Sikuwaambia chochote. Isipokuwa nimesubiri kusikia maoni yako, au utakalotangaza.”
Baadaye tukaenda pamoja naye, hadi alipofikia moja kati ya maduara hayo akasimama na kusema: “Hili ni jambo gani ninaloliona munalifanya?” Walijibu, “Ee Abu ‘Abdur-Rahmaan! Hivi ni vichangarawe ambavyo tunavihisabia takbiyr, tahliyl na tasbiyh.” Akawaambia, “Ni afadhali muyahisabu matendo yenu maovu. Kwani nakuhakikishieni kwamba hakuna maovu yenu yatakayopotea. Hasara iliyoje kwenu enyi Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Ni kwa haraka gani munakimbilia kwenye uharibifu! Hawa ni Maswahaba wa Nabiy wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao wameenea. Hizi ndizo nguo zake ambazo bado hazijachakaa, na bakuli lake ambalo halijavunjika. Naapa kwa Yule Ambaye roho yangu ipo mikononi mwake! Aidha mupo kwenye dini ambayo imeongoka zaidi kuliko Diyn ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ama munafungua milango ya upotofu.”
Walisema: “Ee Abu ‘Abdir-Rahmaan! Tunaapa kwa Allaah! Hatukunuwia zaidi ya kutenda mema.” Aliwaambia: “Ni wangapi wananuia kutenda mema, lakini hawafanikiwi kwa hilo. Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia: "Watu wataisoma Qur-aan, lakini haitovuka zaidi ya koo zao." Naapa kwa Allaah mimi sijui, lakini pengine mengi kati ya hayo yanatoka kwenu.”
Baadaye akaondoka. ‘Amr bin Salamah amesema: “Tumewaona wengi kati ya watu hao wakipigana dhidi yetu katika siku ya Nahrawaan, wakiwa pamoja na Khawaarij.”[4] Hivyo simulizi hii safi kabisa inayo ndani yake kanuni muhimu, ambazo hazitambulikani isipokuwa kwa wale wanaomfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wale ambao hawaweki chochote kabla ya Allaah na Nabiy Wake, isipokuwa wanasema: “Tumesikia na tunatii.” Kutokana na hayo, kanuni wenyewe ni:
Kwanza: Kwamba Yule Ambaye Ameamuru taratibu zake, Hakusahau kuamuru namna zake. Hivyo pale Allaah Alipowaamuru watumwa Wake dhikr (ukumbusho kwa Allaah), Hakusahau kuamuru namna na njia za kufanya hivyo. Hivyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihisabu tasbiyh (utakaso kwa Allaah) katika mkono wake wa kulia[5] na alisema kwamba hivyo (yaani vidole) vitaulizwa na vitazungumza.[6]
Pili: Kwamba al-bid’atul-idhwaafiyyah ni upotofu. Na al-bid’atul-idhwaafiyyah ni aina ambayo uzushi unaegemezwa juu ya ushahidi kwa mnasaba wa msingi wake, lakini hauna ushahidi kwa mnasaba wa taratibu au mtindo. Ndio maana inaitwa idhwaafiyyah (kitu kilichoongezwa juu yake). Na aina hii ya uzushi ni, kwa upande mmoja, unakwenda kinyume na uongofu moja kwa moja, na kwa upande fulani, unakubaliana nayo (upotofu). Hivyo watu hawa hawakusema kitu ambacho ni kufr (kutoamini), wala hawakuwa ni wenye kufanya jambo ambalo asili yake wenyewe ni ovu, isipokuwa walikuwa wakimkumbuka Allaah – na hichi ni kitu ambacho kimeamrishwa na Uteremsho. Hata hivyo, namna ambayo utekelezaji wake umefanywa ulienda kinyume na uongofu uliowekwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hivyo Swahaba waliwapinga na kuwaambia kuhisabu badala yake matendo yao maovu.
Tatu: Allaah – Mkamilifu, Mtukufu – Hapaswi kuabudiwa, isipokuwa kwa namna Aliyoamrisha Mwenyewe. Hivyo Asiabudiwe kwa namna ya kufuata matakwa, utamaduni na uzushi.
Nne: Uzushi huo unaua Sunnah. Hivyo kundi hili la watu limezua njia mpya ya kufanya dhikr (kumkumbuka Allaah), ambayo haikuwahi kusimuliwa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo kwa kufanya hilo, wameua uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni kanuni ambayo, Salafus-Swaalih (Waja wema waliotangulia) wameifahamu vizuri, na wameijua kwa hakika kwamba uzushi na Sunnah haviwezi kuungana pamoja. Hasan bin ‘Awtiyyah (amefariki mwaka 120H) (Rahimahu Allaah) – amesema: “Hakuna watu watakaoanzisha uzushi ndani ya dini, isipokuwa kwamba mfano wake kutoka kwenye Sunnah wanauvuta mbali.”[7]
Tano: Uzushi huo unapelekea kwenye uharibifu, kwani unapelekea kuiacha Sunnah, na hii inasababisha upotofu mkubwa kabisa. Swahaabah maaarufu 'Abdullaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Iwapo utaitupa Sunnah ya Nabiy wako basi utaenda kwenye upotofu.”[8] Hivyo iwapo Ummah unakwenda kombo basi unaharibika. Halikadhalika, 'Abdullaah bin Mas’uud amesema kuliambia kundi lile: Enyi Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Ni kwa haraka gani munakimbilia kwenye uharibifu.” Hivyo ufahamu wa Ibn Mas’uud kwa kulinganisha tokea lile ulilinganisha maandiko ya simulizi hiyo hapo juu.
(Ni dhahiri kwamba) Abu Muwsa al-‘Ash’ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuwapinga, isipokuwa alisubiri wazo au amri ya 'Abdullaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Na msimamo huu haukutolewa kutoka kwenye mapenzi au kuonesha athari za uongo kwa Ibn Umm ‘Abd (yaani Ibn Mas’uud). Isipokuwa, Abu Muusa alijiridhisha mwenyewe kwa lile ambalo ameliridhia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummah wake, kwani yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Nimeridhia kwa Ummah wangu kwa lile ambalo Ibn Umm ‘Abd ameliridhia."[9] Pia kwenye simulizi hiyo ni ushahidi kwamba Swahaba wote walikubaliana kulipinga tendo hili, kwani 'Abdullaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ametumia kama ni ushahidi na ukweli kwamba Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) walienea kwa mapana (na hivyo wangeliweza kuulizwa kwa urahisi).
Sita: Kwa njia ya haraka, uzushi unapelekea kwenye kukufuru (kutoamini). Hii ni kwa sababu mzushi amejifanya kuwa yeye mwenyewe ni mwenye uwezo wa kutunga sheria na kuweka utaratibu; na hivyo kujifanya kuwa kama ni mshirika pamoja na Allaah, akiongeza mambo kwenye kanuni zilizowekwa na Allaah, akidhani kwamba yeye yupo kwenye dini sahihi iliyo ongofu zaidi kuliko Diyn ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Saba: Uzushi huo unafunua milango wazi kwa kutokea malumbano, na huu ni mlango wa upotofu. Kwa hivyo, yeyote anayeanzisha njia ya uovu ndani ya Uislamu, basi atabeba dhambi yake na dhambi ya wale wanaolitendea, hadi ya Siku ya Hukumu, bila ya dhambi zao kupunguzwa kwa chochote. Na hili ni kwasababu yule ambaye anayewaongoza watu kwenye uovu ni kana kwamba naye anaufanya (uovu huo.).
Nane: Kutotilia mkazo katika kukemea uzushi, inapelekea kwenye uovu na madhambi. Je huoni kwamba watu walikuja kuwa ni miongoni mwa wakuu wa kundi lililojitenga lilioitwa Khawaarij siku ya Nahrawaan, wakipigana dhidi ya Swahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum), ambao waliongozwa na Kiongozi wa Waumini ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu), ambaye alilikata kundi hili lililojitenga, kwenye siku hiyo yenye kumbukumbu.
Imaam al-Barbahariy (aliyefariki mwaka 329 H) (Rahimahu Allaah) amesema: “Tahadhari na mambo ya uzushi madogo, kwa sababu yanakuwa na kufikia kuwa makubwa. Hii ndio ilikuwa kadhia ya kila uzushi ulioanzishwa ndani ya Ummah huu. Ulianza kama ni kitu kidogo, ukifanana na ukweli, ndio sababu ya wale waliouingia walipotoshwa, na baadaye wakawa hawawezi kuuacha. Hivyo ukakuwa na kuwa ni dini ambayo waliifuata, hivyo walijitenga kutokana na Njia Sahihi na hivyo kuuacha Uislamu. Rahmah za Allaah ziwe juu yako! Angalia vizuri mazungumzo ya kila mmoja unayemsikia, haswa ndani ya kipindi chako. Hivyo usifanye haraka kulitenda, wala kuingiza chochote ndani yake, hadi uulize na uone: Je kuna Swahaba wowote wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliozungumzia kuhusu hilo, au Mwanazuoni yeyote (wa mwanzo)? Hivyo kama utapata simulizi kutoka kwao, gandana nayo na wala usiivuke juu yake kwa lolote, wala usitoe hukumu juu yake na hivyo kuingia kwenye Moto[10]
Tisa: Matendo mema ni kwa mujibu wa niyah njema, na niyah njema haifanyi jambo ambalo lisilo na mashiko kuwa ni sahihi. Hii ni kwa sababu niyah pekee haziwezi kufanya tendo kuwa ni sahihi, isipokuwa ziongezewe juu yake kwa kuendana pamoja na Shari’ah (Sheria za Uteremsho) [11]
Mwisho: Kuongeza katika jambo zuri sio vizuri, kwa sababu kuongeza ndani ya jambo zuri ni uovu, na hili ni jambo ambalo tunalishuhudia katika kila kitu. Hivyo, jambo linapokwenda nje ya mipaka yake, linabadilika na kuwa kinyume chake. Hivyo ukakamavu unapoengezewa, unabadilika na kuwa ulegevu, na unapopunguzwa, unakuwa ni ujinga. Na ukarimu, mipaka yake inapovushwa, basi unageuka na kuwa ni israfu, na iwapo utapunguzwa, basi unakuwa ni uchoyo. Kwa hivyo mambo haswa ili yawe mazuri ni yale ambayo yapo kwenye wastani. Na 'Abdullaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) hakuwa peke yake miongoni mwa Swahaba waliokataza uzushi.
Kwa hivyo hapa tunamkuta 'Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alikuwa miongoni mwa Swahaba wakali kabisa kwenye kukemea uzushi na kuwapuuzilia mbali wazushi. Kwa hivyo siku alipomsikia mtu aliyechemkwa (chafya) akisema: ‘Shukrani zote ni za Allaah na swalah na salaam (shukrani za Allaah na rahmah za amani) ziwe juu ya Rasuli wa Allaah.’ Hivyo alimwambia: ‘Ni nini hichi? Hivi sivyo ambavyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyotufundisha, isipokuwa amesema: Mmoja wenu anapochemkwa basi na amshukuru Allaah. Na wala hakusema kumwambia: Na pia mpelekee swalah na salaam juu ya Rasuli wa Allaah.’[12]
Vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa mwenendo wa taabi’iyn (wale ambao wamekutana na Swahaba na kushikamana na mwenendo wao). Kwa hivyo kwa mnasaba huu kuna simulizi iliyopokewa kutoka kwa Sa’iyd bin Muswayyib (aliyefariki mwaka 90) – (Radhwiya Allaahu 'anhu) – kwamba amemuona mtu akiswali baada ya jua kuchomoza (ishraaq), zaidi ya rak’ah mbili, akifanya ruku’u na sajdah nyingi, kwa hivyo alimzuia kufanya hivi. Yule mtu alisema: ‘Ee Abu Muhammad (yaani Ibn Al-Muswayyib)! Je, Allaah Ataniadhibu kwa Swalah yangu?’ Alimwambia: “Hapana! Lakini Atakuadhibu kwa kuipinga Sunnah (muongozo wa Ki-Unabiy).”[13] Na simulizi hizi zina nukta nyingi nzuri zenye manufaa, kwa mfano:
i. Swahaba walimpinga kila mtu aliyekwenda kinyume na Sunnah, mara nyengine ilikuwa inauma zaidi katika upingaji wao, hata kama itakuwa dhidi ya baba zao na watoto wao.
ii. Kwamba bid’atu-tarkiyyah ni upotovu: Na aina hii ya bid’ah (uzushi) ni miongoni mwa zile ambazo kuna thibati ya kutetea tendo, isipokuwa kwamba watu kwa makusudi wameacha tendo hilo, wakidhani kwamba ni sehemu ya Diyn, au kwamba kitu kinachofanana nacho. Kwa mfano, baadhi ya Masufi walioacha ndoa kwa lengo la kujidhoofisha wenyewe. Ushahidi wa hili kwamba ni upotovu ni kutoka kwa Allaah – Mtukufu – Akisema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحَرِّمُوا طَيِّبَاتِ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٨٧﴾ وَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ ﴿٨٨﴾
Enyi walioamini! Msiharamishe vizuri Aliyokuhalalishieni Allaah, na wala msipindukie mipaka. Hakika Allaah Hapendi wapindukao mipaka. Na kuleni katika vile Alivyowaruzuku Allaah vya halali na vizuri. Na mcheni Allaah Ambaye nyinyi mnamwamini. [Al-Maaidah: 87-88]
Hivyo Aayah hii inahusiana na maana moja, ambayo ni: kuharamisha yale ambayo Allaah Ameruhusu katika mazuri na vitu safi, na kufanya hivyo kama ni jambo la Diyn. Na Allaah Ameharamisha hili, na kulihusisha kama kwenda zaidi ya mipaka, kwani ni kukiuka haki ya Allaah, ni kwamba Yeye pekee ndiye mwenye haki ya kuweka na kutunga shari’ah. Na Allaah Hawapendi wale wanaochupa mipaka. Kisha Allaah Amehakikisha malipo ya vitu hivi kwa mkazo zaidi pale Aliposema:
وَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ
Na kuleni katika vile Alivyowaruzuku Allaah vya halali na vizuri. Na mcheni Allaah Ambaye nyinyi mnamwamini. [Al-Maaidah :88]
Kisha Akawaamrisha kuwa na taqwaa (uchaji Allaah). Hili linaonesha kwamba uharamishaji wa kile ambacho Allaah Amehalalisha, kwa namna yoyote, ni nje ya sifa za taqwaa. Hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kwa wale watu watatu waliofika katika nyumba za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakiuliza kuhusu ibada zake na baada ya kuelezwa kuhusu hilo, walijitambua kwamba uabudiaji wao ni mdogo mno, hivyo walisema: “Kuna tofauti kubwa baina yetu na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye dhambi zake za kabla na baada zimesamehewa na Allaah.” Hivyo mmoja wao alisema: “Mimi nitaswali usiku wote.” Mwengine akasema: “Mimi nitafunga mchana na wala sitofungua.” Na wa tatu akasema: “Mimi nitajiweka mbali na wanawake na sitaoa.”
Kisha Rasuli wa Allaah aliwajia na kuwaambia: "Je ni nyinyi ambao mumesema kadhaa na kadhaa? Naapa kwa Allaah! Mimi ni ambaye mwenye elimu ya juu kuhusu Allaah miongoni mwenu, na ni mbora kwa taqwaa juu Yake. Ilhali ninafunga na kufungua, ninaswali na kulala, ninaoa wanawake. Kwa hivyo yeyote anayegeuka kinyume na Sunnah (uongofu) yangu sio miongoni mwangu."[14]
Hivyo Swahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum) wametuachia maneno yenye uono wa ndani na ambayo yanaangaza nyoyo, baadaye watu baada yao, ambao vivyo hivyo wamepokea ukweli huu kutoka mwangaza huu, nao pia wametuachia maneno yenye kufanana na maneno ya Swahaba. Na hii ni kwa sababu walikuwa ni wale ambao walikuwa karibu kabisa na nyayo za Swahaba – na mfano wa maneno yao yaliyotangulia. Hata hivyo tunaongeza hapa mfano wa mwisho kuhusu msimamo wao wa ukweli:
Kuna mtu alikuja kwa Imaam Maalik (aliyefariki mwaka 179H) (Rahimahu Allaah) – na kusema: “Ee Abu 'Abdullaah! Ni wapi niingie kwenye ihraam (nguo ambayo inavaliwa kwa yule anayefanya Hijjah)?” Hivyo Imaam Maalik alimjibu: “Kutoka Dhul-Hulayfah, ambapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwenye ihraam.” Baadaye yule mtu akasema: “Lakini mimi nina hamu ya kuingia kwenye ihraam katika Msikiti ulio karibu na kaburi lake.” Hivyo Imaam Maalik alisema: “Usifanye hivyo, kwani ninakukhofia fitnah (mtihani).” Hivyo yule mtu akasema: “Ni fitnah gani unayoieleza, kwani ni sehemu tu ya masafa (maili) chache zaidi.” Imaam Maalik akasema: “Na ni fitnah gani itakayokuwa kubwa zaidi ya wewe kufikiri kwamba umefikia baadhi ya wema, ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakupata kuufanya. Hujasikia maneno ya Allaah:
فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ
Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr: 63][15]
[1] Al-Bid’ah wa Atharuhas-Sayyi‘ah fil-Ummah (uk.22-36)
[2] Imepokewa na Waki’i ndani ya az-Zuhd (namba 315) na Abu Khaythaman ndani ya Kitaabul-‘Ilm (namba 54), ambapo al-Albaaniy ameisahihisha. Toleo hili linahusiana na at-Tabaraaniy ndani ya al-Kabiir (9/154) na ni sahihi.
[3] Imepokewa na al-Bayhaqiy ndani ya al-Madkhali ilas-Sunan (namba 191) na pia Ibn Naaswir ndani ya as-Sunnah (uk. 24).
[4] Imepokewa na ad-Daarimiiy ndani ya kitabu chake cha Sunan (1/79), atw-Twabaraanii ndani ya al-Kabiir (9/126) na Abu Nu’aym ndani ya Hilyatul-Awliyaa (4/381). Ilisahihishwa na al-Haythamiy ndani ya Majma’uz-Zawaa’id (1/181).
[5] Swahiyh: Imepokewa na Abu Daawuud ndani ya Sunan (namba 1502), kutoka kwa 'Abdullaah bin ‘Amr (Radhwiya Allaahu 'anhu). Ilisahihishwa na al-Albaaniy ndani ya Sahiih Sunan Abii Daawuud (1/280).
[6] Hasan: Imepokewa na Abu Daawuud ndani ya kitabu chake cha Sunan (namba 1501), kutoka kwa Yusayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu). Ilisahihiswa na Shaykh al-Albaaniy ndani ya Sahiih Sunan Abii Daawuud (1/280).
[7] Imesimuliwa na ad-Daarimii (1/45) na ni sahihi.
[8] Imepokewa na Muslim (5/156).
[9] Swahiyh: Imepokewa na al-Haakim (3/317-318) na Ibn ‘Asaakir ndani ya al-Majlis (namba 350). Ilisahihiswa na al-Albaaniy ndani ya as-Swahiyhah (namba 1225).
[10] Sharhus-Sunnah (namba 8).
[11] Rudia kitabu cha Madaarijus-Saalikiyn (1/85) cha Ibn al-Qayyim.
[12] Imepokewa na at-Tirmidhiy (namba 2738) na al-Mizzii ndani ya Tahdhiibul-Kamaal (namba 552-553). Isnaad yake ni nzuri.
[13] Imepokewa na al-Bayhaqii ndani ya as-Sunanul-Kubraa (2/466) na isnaad yake ni sahihi.
[14] Imepokewa na al-Bukhaariy (9/104) na Muslim (9/175).
[15] Imesimuliwa na Imaam ash-Shaatibii ndani ya al-I’tisaam (1/132).