Zingatio: Tupo Tayari Hata Kutumbukia Hata Ndani Ya Shimo La Kenge? (April Fool)

 

Zingatio: Tupo Tayari Hata Kutumbukia Hata

Ndani Ya Shimo La Kenge? (April Fool)

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ujahili ulipokatwa panga zile enzi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ulihakikisha umeondosha mambo yote ya kijahili kama vile kuwazika mabinti wakiwa hai, ribaa, uzinifu, pombe na mengineyo.

 

Kwa hali zilizokuwepo sasa, yaonesha dhahiri kwamba ujinga uliopo leo umepindukia mipaka ya hizo enzi alizokuwa akiishi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake (Radhwiya Allaahu ‘Anhum). Majahili wa siku hizo hawakuwa na siku maalumu za kuadhimisha afya, maji wala mfano wa hayo. Ujahili wao uligandana na kupata mali pamoja na starehe kwa njia zozote. Kwa ufupi hawakuwa na wakati wa kupoteza, iwe ni wajinga ama werevu.

 

Na kwa hakika, ujinga wa akina Abu Jahal na wenziwe umeshavunjwa rekodi kwa kutufikia Siku ya Wajinga duniani. Juu ya ujinga wao kina Abu Jahal, hawakufikia hatamu ya kufanya ujinga kuwa ndio ibada yao kwa siku nzima. Leo imefikia wakati hata kiongozi mkuu wa nchi anafanyiwa mzaha wa kumtoa machozi, lakini akajifanya kucheka ilhali ndani ya nafsi yake anaungua kwa uchungu. Kwa lipi?! Ati ni April Fool!

 

Ndugu Waislamu, hizi ni siku ambazo zimewekwa kuzidhibiti vyema akili za Waislamu ili wasiweze kuzitambua hila zinazofanywa dhidi yao. Yatosha Muislamu kuiharamisha siku hiyo kwa kupotezewa muda pamoja na kufanywa punguwani (mkosefu wa akili). April Fool ni siku iliyoanza kuadhimishwa huko Magharibi ikaenea ndani ya miji ya Waislamu kwa kasi sana na ikashtadi katika vyombo vya habari na kuendelea kwa uvumbuzi wa teknolojia haswa internet.

 

Makafiri hukaa na kufurahi kwa kicheko cha juu wanapotuona nasi tunawasaidia kulisukuma gurudumu la ujinga. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kwamba hila za Mayahudi na Manaswara hazitafikia mwisho hadi watuone tupo sawa na wao:

 

وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ۗ

Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao. [Al-Baqarah: 120]

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

“Mtafuata desturi (mwenendo) za waliokuwa kabla yenu shibri kwa shibri na pima kwa pima hata wakiingia katika shimo la mburukenge (yaani ndani ya shimo lenye mnyama anayeweza kukudhuru) mutaingia nao.” Wakauliza: “Je, unakusudia Mayahudi na Manaswara?” Akasema: “Ni nani wengine ikiwa si wao”. [Imesimuliwa na Al Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Sa‘iyd al-Khudriy].

 

Ni ajabu pale Muislamu anapoumia kwa kukosa kumfanya mwenziwe mjinga ndani ya siku hii, lakini si mwenye kuhuzunika kwa kuwaona Waislamu wanatolewa roho zao Palestina na Iraaq. Wala hana hisia kwamba Swalaah za faradhi zinampita ama kuna Kitabu cha Allaah chahitaji kufanyiwa kazi.

 

Tuelewe kwamba makosa mengi yamefanyika kwa kuiadhimisha siku hii, miongoni mwa hayo ni pale masikini walipotangaziwa kwenda kupokea msaada wa chakula katika kituo kimoja cha redio, na walipofika wakaambulia maneno hata wasiyoyafamu: "April Fool". Hii ni dhulma kubwa na dua'a ya mwenye kudhulumiwa hairudi.

 

Basi ndugu zangu Waislamu, haujafikia wakati tukatubu madhambi yetu? Toba ambayo itatufanya kuacha kuwaona Makafiri ni bora na badala yake tukausimamisha Uislamu ndani ya majumba yetu, ukasimama mtaani na ukaenea nchini na duniani kote.

 

 

Share