Mume Ananionea, Hanipendi Ananiadhiri Mbele Za Watu, Anajuta Kunioa Nami Naumia Sana Na Mateso Haya Nifanyeje?

SWALI:

 

Asalam aleikum. Ndugu zangu wa alhidaaya nina swali langu nataka uniffahamishe, mimi niko na mume wangu twaishi pamoja lakini hatuelewani kabisaa. Na tangu niishi nae sasa nina miaka 7 nimezaa nae watoto. Na tabiya yake nimkali sana nakila akiniona hana raha na mimi na mimi sijamfanya jambo lolote kubwa na mungu ndio shahidi yangu ndio anayaona. Na pia hapendi mimi nione raha ama nifurahike mpaka kwenye roho yangu hua yaniuma nakumuogopa na pia hua yuwaniambia mambo mabaya nakunionesha viimbi ndani ya nyumba yake bila kosa lolote. Ikiwa nimefanya kosa dogo hua hata hajali kuni azirisha kwa watu kuambia mke wangu hivi vile mpaka hii roho yangu yaniuma.na mimi nimtu siwezi vita na yeye ni mtu wa vita hataki hata kitu chochote niseme hata kama nichaukweli na yuwapenda kuniambia wewe mwanamke gani? Mimi sikukupenda nakuowa tu. Na kama kitu pengine sijapendelea hua ataka nipiga. Na mimi niko nchi zaulaya sina mama wala baba niko peke yangu, sasa sijui ndugu zangu naomba wenu ushauri tafadhali.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kunyanyaswa na mumeo.

Mateso kwa wanawake dada zetu yamekithiri kwa kiasi cha kustaajabisha sana. Na tatizo hili linatokana na kuwa wanawake na wazazi hawatazami muongozo wa Kiislamu katika mas-ala ya ndoa ndio matatizo haya yanayotokea baadaye. Uislamu umetuwekea muongozo mzuri lakini sisi tumekataa kabisa kufuata hayo hivyo kuingia katika matatizo kama hayo. Mara nyingi akija mume kutoka Arabuni au Ulaya huwa anapewa msichana bila ya maswali yoyote yale. Mwanamme huyo huwa hachunguzwi tabia zake wala mambo yake mengine. Lau tungekuwa tunafuata yaliyowekwa na Shari’ah kwa mfano:

 

1.     Kutazama Dini ya mwanamme/ mwanamke.

2.     Maadili na tabia zake.

3.     Mahusiano na wenzake.

 

Basi ndoa zetu zingekuwa ni nzuri na maelewano na masikilizano ya hali ya juu. Kwa hakika hayo unayofanyiwa si mambo mazuri kabisa ya kufanyiwa licha mwanadamu hata mnyama pia haifai kuteswa hivyo. Kwa hiyo, mambo unayoweza kufanya ni kama yafuatayo:

 

1.     Jaribu mwanzo kuzungumza naye yale unayokabiliana nayo kutoka kwake hata kama umesema ni mkali. Ni muhimu ujaribu na utafute wakati ambao unaona anaweza kukusikiliza. Ikishindikana basi;

2.     Wapigie wazazi wako uwaeleze yanayokusibu uwasikilize nasaha zao. Kwa kuwa wawakilishi wako (wazazi) hawawezi kufika huko itabidi baada ya kuwaeleza uwaeleze na wazazi wake kwa yale yanayokukumba. Ikiwa wazazi wake wapo huko mnakoishi itabidi uitishe kikao na wao kuhusu hilo. Ikiwa hakukupatikana suluhisho itabidi uchukue njia ya mwisho. Nayo ni;

3.     Kwenda kwa Qaadhi kama yupo, na kama hayupo basi itabidi uende kwa Imaam au Shaykh wa mji unaoishi ili umueleze unayokumbana nayo ili mpate suluhisho muafaka kabisa.

 

Twataraji kuwa kutapatikana suluhisho muafaka kabisa kwa tatizo lako hilo inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share