Watu Wepi Watakaoingia Peponi Bila Ya Hesabu?

SWALI:

Je ni watu gani wataingiya peponi bila hesabu.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu watu watakaoingia Peponi bila hesabu.

 

 

Ama kuhusu watu hao wapo wale walio karibu sana na Allaah Aliyetukuka nao ni Manabii na Mitume (‘Alayhimus Salaam). Ama wengine ni wale elfu sabini waliotajwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Je, tunaweza kuwajua hawa ni kina nani au wana sifa gani?

 

Watu hao na sifa zao zimetajwa katika Hadiyth ya kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

Nilionyeshwa mataifa (watu), na nikamuona Nabiy mmoja akiwa na watu kidogo; Nabiy mwengine akifuatwa na mtu mmoja au wawili; na mwingine hana mfuasi hata mmoja. Mara nikaona kundi kubwa, nami nikadhania kuwa hao ni wafuasi wangu, lakini nikaambiwa: Huyo ni Muwsaa na wafuasi wake’. Lakini tazama upande mwingine. Nilitazama nami nikaona kundi kubwa sana. Kisha nikaambiwa tena tazama na upande mwingine wa mbingu, nako kulikuwa na kundi kubwa. Hapo nikaambiwa: Huu ni Ummah wangu, kati yao kutakuwa na elfu sabini watakaoingia Peponi pasi na hesabu au adhabu. Baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia nyumbani mwake. Watu walianza kujadiliana kuhusu watakaoingia Peponi bila hesabu wala adhabu. Baadhi yao walisema kuwa hao ni Maswahaba wa Mtume. Na wengine wakasema kuwa huenda hao wakawa wale waliozaliwa katika Uislamu, hivyo kutomshirikisha Allaah na chochote. Ilhali wengine wakasema mambo mengine. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka nyumbani kwake na kuwauliza: ‘Je, mnajadiliana kuhusu nini?’ Walimwambia waliyokuwa wakijadiliana, naye akasema: Ni wale ambao wasiotafuta kufanyiwa ruqyah, wala kujichoma chuma cha moto, wala hawaamini mkosi, bali wanamtegemea Mola wao na kutawakali Kwake (Pekee)’. Akasimama ‘Ukkaashah bin Mihswan akauliza, ‘Hivi mimi ni miongoni mwa hao, ewe Mtume wa Allaah?’ Akamjibu, ‘Ndiyo’. Akasimama mwingine, naye akauliza, ‘Hivi mimi pia ni miongoni mwao?’ Akamjibu, ‘Amekutangulia kwa hilo ‘Ukkaashah’.” [Al-Bukhaariy na Muslim].  

 

Na pia zipo Hadiyth zinazotueleza kuwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) ataingia Peponi bila hesabu.

 

Na Allaahu Anajua zaidi

 

 

Share