Wanawake Wasio Waislamu Wanavaa Hijaab Shuleni Je, Wakatazwe?

SWALI:

 

Assalaam alaykum warahmatullaahi wabarakaatu. Mimi ni mwanachuo katika chuo kimoja cha mchanganyiko, katika chuo hiki wasichana wameruhusiwa kuvaa hijabu, lakini wapo wasiokuwa waislamu wanavaa vazi hili bila utaratibu, sasa tunashindwa kuwachukulia hatua. Je inaswihi kuwazuia au tuwaache?


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu wanawake wasio Waislamu kuvaa Hijaab.

 

Huu ni mwanzo mwema kwa hao wanawake wanaofanya hivyo. Linalotakiwa ni nyinyi kufanya mikakati ya kuweza kuwasiliana na wanawake hao na kuwaelezea Uislamu na hekima ya vazi hilo ambalo ni la heshima na zuri. Inatakiwa mtumie njia nzuri ima kwa kufanya nyinyi wenyewe au kuwatumia wanawake wa Kiislamu walio katika chuo hicho.

 

Kinachotakiwa nyinyi kufanya ni kutumia busara na mawaidha mazuri katika ulinganizi wenu kama alivyosema Aliyetukuka:

"Lingania watu katika njia ya Mola wako Mlezi kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora" (16: 125).

 

Hamuwezi kutumia nguvu, kwani hata mkitumia nguvu na hawataki basi haitokuwa na faida zaidi ya kujenga uadui au kuuzidisha. Pia mnaweza kuwa na orodha yao hao ili kunapotokea jambo ambalo limefanywa na wao na likahusishwa na Uislam, basi tayari mnao ushahidi kuwa hao waliotenda sio Waislam bali wanatumia alama za Kiislamu kuuharibia Uislamu jina na kuuchafua. Hilo pia linaweza kusaidia wakati wa matatizo.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share