Kwa Nini Wanaume Wamepewa Cheo/Fadhila/Mamlaka Zaidi Kuliko Wanawake?

 

Kwa Nini Wanaume Wamepewa Cheo/Fadhila/Mamlaka Zaidi Kuliko Wanawake?

 

Alhidaaya.com 

 

 

SWALI:

 

Assalamu alayum warahmatu llahi taala wabarakatu.

 

Naomba kuuliza maswali: ambayo yananiumiza kichwa changu na kila ninaemuuliza naona sijafaidika bado na majibu ninayoyapata. Kwa nini mwanamme ana cheo kikubwa kuliko mwanamke katika uislam wakati mwanamke ana kazi kubwa kuliko mwanamme? Mwanamke anazaa, anashughulikia nyumba na watoto, anamshughulikia mume kama mtoto mchanga, mwanamke ni mtu mwenye kazi masaa ishirini na nne hapumziki, mwanamme kazi anayoifanya ni kutafuta kijio. Lakini tunaambiwa kwamba kama kuna kusujudu baada ya Allaah tungeambiwa tusujudie waume zetu, na mirathi wao wamepewa mingi kuliko wanawake, lazima ukitoka uage wao si lazima, wao wamepewa uwezo wa kuoa mke mwengine, wamepewa uwezo wa kutoa talaka, na mambo mengi ambayo mwanamke hakupewa, swali langu liko hapo.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika hili ni suala ambalo linaonekana hivyo na watu hasa kwa ajili ya kasumba ambazo zinatiwa na wasiokuwa Waislamu wasiouelewa Uislamu na haki inayompatia kila mmoja.

 

 

Awali ya yote inatakiwa tufahamu kuwa aliyempatia haki kila mmoja wetu ni Allaah Mtukufu ambaye Anamjua kila mmoja wetu na kila analostahiki. Hakika ukichambua haki zilizoko kwa kila mmoja wetu utakuta kuwa mwanamke amepatiwa haki zaidi na Uislamu kuliko mwanamme. Tutajaribu katika jibu letu kuangazia yote yaliyoulizwa na ndugu yetu.

 

 

Kabla ya kuendelea na kuangazia haki na wajibu wa mwanamke na fadhila zake, tuangalie mwanamke alivyokuwa akifanywa kabla ya kukamilishwa Uislamu kwa kuja kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mfano:

 

1.    Katika Bara Arabu mwanamke alikuwa hana hadhi, akiuliwa pindi anapozaliwa (An-Nahl [16]: 58 – 59), kurithiwa na hata watoto wake wa kambo pindi alipokuwa mumewe, kunyimwa urithi kabisa na mengineo mengi.

 

2.    Mwanamke katika ustaarabu wa Kigiriki alikuwa ni chombo cha kuondolea matamanio ya kiwiliwili cha mwanamme; hivyo alikuwa akiuzwa kama machungwa sokoni. Socrates alisema: “Mwanamke ni chanzo cha machafuko yote duniani, yeye ni kama mti wa dafali ambao sura ya nje ni ya kuvutia mno lakini iwapo ndege ataula basi ni wazi atakufa”

 

3.    Ama mwanamke katika Ukristo hana thamani kabisa.  Kulingana na Biblia, mwanamke hana utukufu kwa sababu ameumbwa kwa ajili ya mwanamme (1 Wakorintho 11: 7 – 10). Vile vile yeye ni najisi (Ayubu 14: 1 – 4), ndiye asili ya dhambi (Mwanzo 3: 12) na kadhalika.

  

4.   Mwanamke katika Ubaniyani alikuwa akichomwa hadi kufa na mumewe iwapo mume atakufa kabla yake na kutokuwa na uhuru kabisa wa aina yoyote.

 

5.    Mwanamke wa Kirumi alikuwa ni pambo kwa mwanamme na kwa kuwafurahisha wafalme alikuwa anaimbishwa akiwa uchi. Na tabia hii ya kishenzi imebakia hadi leo.

  

6.    Mwanamke wa Kichina alikuwa hana haki yoyote katika jamii, na mumewe alikuwa ana haki ya kuuza mwili wa mkewe kwa wanaume wengine. Naye alirithiwa kama mali na jamaa za mumewe pindi anapoaga dunia.

  

7.   Ama mwanamke wa kisasa katika tamaduni mbali mbali amekuwa ni chombo cha kuridhisha wanaume kwa njia moja au nyingine. Hakuna bidhaa yoyote inayouzwa bila kuonyesha mwanamke kwenye matangazo.

 

Tukija katika Uislamu Allaah Aliyetukuka Amempatia kila mmoja kati ya mwanamme na mwanamke majukumu, haki na wajibu wake kulingana na maumbile yake. Hata hivyo, mwanamme amepatiwa daraja ya juu kuliko mwanamke. Anasema Aliyetukuka:

 

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ

Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. [An-Nisaa: 34]

 

 

Ama majukumu yao yanakuwa ni wenye kusaidiana ili kuleta mabadilko mazuri katika jamii. Utapata kwa suala lingine mwanamke yuko juu ya mwanamme na kwa jambo jingine ni mwanamme mwenye jukumu kubwa zaidi.

 

Uislamu umetangaza kabisa kuwa asili ya mwanamke na mwanamme ni moja:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ 

Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi.  [An-Nisaa: 1].

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

Hakika wanawake ni ndugu wa wanaume” [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy].

 

Ama katika Uislamu hakuna kosa la asili ambalo analaumiwa mwanamke bali wote wanalaumiwa kwa kushawishiwa na Shaytwaan:

 

فَأَزَلَّهُمَا الشَّيْطَانُ عَنْهَا فَأَخْرَجَهُمَا مِمَّا كَانَا فِيهِ ۖ 

Shaytwaan akawatelezesha wote wawili kwayo, Akawatoa kutoka katika hali waliyokuwa nayo. [Al-Baqarah: 36].

 

Na pia:

قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾

Wakasema: Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu; bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Al-A‘raaf: 23].

 

 

Hivyo, wote walikosa na wakasamehewa, kwa hiyo kutokuwa na makosa baada ya hapo.

 

 

Mwanamme na mwanamke wapo sawa katika malipo lau mmoja wao atatenda mema. Anasema Aliyetukuka:

 

قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾

Wakasema: Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu; bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Al-A'raaf: 23].

 

Na pia,

أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ ۖ 

Hakika Mimi Sipotezi ‘amali za mtendaji yeyote yule miongoni mwenu akiwa mwanamume au mwanamke,... [Aal-‘Imraan: 195].

 

Pia waweza kutazama kuhusu haya katika Suwrah Al- Nahl: 97 na pia Suwrah Al- Ahzaab: 35.

 

 

Na mwenye kufanya uhalifu ima wa kuiba au kuzini, akiwa mwanamke au mwanamme atapata adhabu hiyo hiyo. Tazama adhabu ya wizi katika Suwrah Al-Maaidah: 38 na uzinzi katika Suwrah Al-Nuwr: 2.

 

 

Pia Uislamu umempatia kila mmoja wao usawa wa kiuchumi na kumiliki mali, kufanya biashara baina ya jinsia hizo mbili. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَلَا تَتَمَنَّوْا مَا فَضَّلَ اللَّـهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُوا ۖ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ ۚ وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٣٢﴾

Wala msitamani ambayo Allaah Amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu katika waliyoyachuma, na wanawake wana sehemu katika waliyoyachuma. Na muombeni Allaah fadhila Zake. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu. [An-Nisaa: 32].

 

 

Na kwa ajili hii tunaona vipi wanawake katika enzi tofauti waliweza kuusaidia Uislamu na Waislamu kwa pesa zao, mfano mmoja ni Mama wa Waumini Khadijah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).

 

 

Mwanamke naye ana haki sawa katika kurithi kile ambacho kimeachwa na jamaa wa karibu. Kwa hilo, Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ ۚ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿٧﴾

Wanaume wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu. Na wanawake wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu, ikiwa ni kidogo au kingi; ni mgao uliofaridhishwa. [An-Nisaa: 7].

 

 

Hata hivyo, Uislamu umempatia mwanamme sehemu mbili kwa moja anayopata mwanamke. Huenda hilo likaonekana ni dhuluma kwa mwanamke, lakini tukiona hekima kwa mgao huo tunaweza kugundua kuwa pengine mwanamme amepata sehemu ndogo zaidi kwa mgao huo. Kwa muhtasari mwanamme amepatiwa sehemu kubwa zaidi katika urithi kuliko mwanamke katika shari’ah ya Kiislamu. Na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:

 

1. Mwanamme amelazimishwa kutoa mahitaji kwa mkewe, wanawe, jamaa zake wa karibu, tofauti na mwanamke ambaye hakukalifishwa kishari’ah kutoa mahitaji yoyote. Kwa hiyo, mali anayopata mwanamme inatumika kwa watu wengi ilhali ya mkewe itakuwa ni yake anaweza kuweka akiba, wala hatolazimika kutoa senti moja katika mali aliyorithi kwa ajili ya watu wengine.

  

2.  Mwanamme anawajibika kutoa mahari kumpa mwanamke wakati akioa ilhali mwanamke yeye hatoi mahari bali ndiye anayepatiwa mahari tena anayotaka yeye.

 

3.  Wajibu wa kuwaelimisha watoto, kuwatibu wenye kumtegemea na kuwatunza ni wa mume. Kwa hivyo, urithi wake wote utatumika kwa mambo kama hayo, ilhali urithi wa mwanamke ni wake naye hana wajibu kama huo.

 

 

Labda tuchukue mfano wa mzazi aliyekufa akaacha mvulana na msichana na akiwa amebakisha 30,000. Kwa mgao wa Kiislamu ikiwa hakuna mrithi mwengine, mvulana atapata 20,000 na msichana 10,000. Na endapo wote wawili wamefikisha umri wa kuoa na kuolewa, na kila mmoja atalipa au kulipwa elfu kumi (10,000). Kwa minajili hiyo, mvulana atatoa 10,000 na kubakisha 10,000, ilhali msichana akipata 10,000 atakuwa na pesa taslimu 20,000. Hizi pesa za msichana ni zake na anaweza kuzitumia kwa njia yoyote atakayo ilhali mvulana pesa alizobaki nazo itabidi azitumie kumtazama mkewe na watoto atakaporuzukiwa. Msichana hata akizaa jukumu la kumtazama yeye pamoja na mtoto/ watoto ni la mumewe. Na lau ikitokea sinto fahamu (su-u tafaahum) baina ya mume na mkewe, na kutokea talaka msichana huyo atarudi kwa kaka yake na ni jukumu la kaka kumtazama katika hali zote zile.

 

 

Pia Uislamu umeweka nidhamu kuwa wazazi wanatakiwa wawalee watoto wote bila ya kuwabagua kati yao kulingana na jinsia zao. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ 

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe;... [At-Tahriym: 6].

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye watoto wa kike watatu au dada watatu au watoto wa kike wawili au dada wawili akawalea vyema na akamcha Allaah kwa ajili yao basi atapata Pepo" [At-Tirmidhiy].

 

 

Na hivyo, hapa tunapata msisitizo wa umuhimu wa kuwalea watoto wa kike kwa wema na njia nzuri.

 

 

Uislamu umempatia haki mwanamke kwa kumuelimisha sawa na mwanamme na umesisitiza sana kupewa elimu wanawake tangu awali ya risala yake kupitia kwa Nabiy wa mwisho (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Ametujulisha kwamba wenye kumuogopa yeye kikweli ni watu wenye elimu bila kubagua jinsia, 

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ 

Na kwa hakika wanaomuogopa Allaah katika viumbe Vyake ni wenye elimu.[Al-Faatwir : 28].

 

 

Pia jinsia zote mbili zina jukumu la kuamrisha mema na kukataza maovu. Hiyo ni kama Alivyosema Aliyetukuka:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ

Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari.. [At-Tawbah: 71].

 

 

Inatakiwa tufahamu kuwa kila mmoja – kati ya mwanamme na mwanamke ni mchungaji na ana jukumu kila mmoja katika Nyanja yake katika maisha. Mume na mke wanatakiwa wasaidiane katika kutengeneza jamii kwa njia iliyo nzuri zaidi.

 

 

Yapo majukumu mengine ambayo yanampasa mwanamme peke yake, miongoni mwayo ni kuitazama nyumba yake na pia kuipigania Dini ya Allaah Aliyetukuka. Mwanamke hapaswi kuitazama nyumba ila tu anapotaka kumsaidia mumewe na hiyo itakuwa ni ihsani kwa upande wake. Ama Jihadi wanawake, hawana uwajibu wa kutekeleza hilo. Na kwa ajili ya kutazama nyumba zao, wakati mmoja wanawake walimtuma msemaji wao, Asmaa’ bint Yaziyd as-Sakan (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa yupo pamoja na  Swahaba zake, ambaye alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Umetumwa kwa wanawake na wanaume, nasi tumekuamini. Hata hivyo, wanaume wanapata fadhila zote kwani wao wanahudhuria Swaalah pamoja nawe, wanapata kujifunza kwako na wanapigana katika njia ya Allaah ilhali sisi twawatazama watoto wao wakiwa hapo. Je, nasi tutapata nini?” Akasema: “Kukaa kwenu nyumbani mnashirikiana nao katika thawabu”.

 

 

Uislamu umetambua kazi kubwa ya mwanamke, hasa katika kubeba mimba, kuzaa na kumlea mtoto na kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿١٤﴾

Na Tumemuusia insani kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa katika miaka mwili; ya kwamba, unishukuru Mimi, na wazazi wako; Kwangu ndio mahali pa kuishia. [Luqmaan: 14].

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Ni nani aliye na haki wa usuhuba wangu?” Akasema: “Mama”. Kisha nani? Akasema: Mama. Kisha nani? Akasema: Mama. Kisha nani? Akasema: Baba” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa dhamana kwa mwanamke ambaye ataswali Swaalah zake tano, kufunga mwezi wa Ramadhwaan na kumtii mumewe kuwa ataingia Peponi kwa mlango wowote atakao.

 

 

Ama kuhusu talaka ameachiwa mume kwa sababu yeye ni mvumilivu zaidi na anaweza kuzuia hasira zake kwa wakati ambao alikuwa afanye jambo ambalo litaleta hasara katika jamii. Mara nyingi mwanamke hisia zake zinakwenda na yale mabadiliko ambayo anakabiliana nayo katika maisha yake na mwilini mwake mabadiliko ambayo mwanamme hana kwa kiasi cha mwanamke. Mwanamke ni mwepesi wa kuchukua hatua za haraka kisha kujuta baadaye mbali kabisa na mwanamme. Bila shaka, mwanamke pia amepatiwa aina mbili za talaka – Khul’ (kujitoa na kujivua katika ndoa) na pia kupitia kwa Qaadhi ikiwa mume ana makosa.

 

 

Ukitazama katika haya tuliyoyaeleza utakuta kuwa mwanamke amepatiwa fadhila kubwa na Uislamu kwa yale majukumu wafanyao na kazi zao nzuri.

 

 

Tunatumai majibu haya yataondosha shaka shaka ulizokuwa nazo na ambazo zinachangiwa sana na makafiri na wale Waislamu haswa wanawake wanaodai kupigania haki za wanawake wanaotumiwa na makafiri.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share