Swawm Ya Nabiy Daawuwd; Akishindwa Kutimiza Anaweza Kufunga Siku Nyinginezo Pasi Jumatatu Na Alkhamiys?

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum Warrahmatulah Wabarrakatuh,

 

Kwa kweli sifa njema zote anastahiki Allah Subahannahu Wataa'ala.

Nashahidilia kuwa hakuna Mola apasae kuabuduwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kuwa Muhamad ni mja wake na ni mtume wake kwa walimwengu wote. Kazi hii mnayoifanya ni kazi safi na hakuna kusita malipo yapo kabisa ni kwa Allah Subahanahu Wataa'ala.

 

Swali langu la kwanza ni hili: Mtu akijaribu kufata na kufanya sunnah ya ibada aliyokuwa akifanya Dawuud hata kama asifanye kila siku kama alivyokuwa anafanya Dawuud je inakubaliwa? Tuseme nikifunga kama jinsi alikuwa akifunga na kuswali kama jinsi ambavyo alikuwa akiswali lakini nikafika wakati napumzika kidogo ama nikashindwa kuendelea itakuwa vipi?

 

Swali la Pili: Je kufunga na siku ambazo si jumatatu ama Alkhamys inajuzu? Wassalam aleikum warrahmatulah wabarrakatuh.

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Swawm ya Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) na Swalah yake.

Mwanzo inatakiwa tuelewe kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza Waislamu kufunga kila siku. Swawm ya Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) ilikuwa ni ya kufunga siku moja na kuacha siku moja, yaani siku baada ya siku. Na hii ndiyo aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ndio Sunnah bora zaidi ya funga (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa ‘amali iliyo bora zaidi ni ile inayodumu japokuwa ni ndogo au kidogo. Kwa hiyo badala ya kufunga Swawm ya Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) funga Jumatatu na Alkhamiys au funga kila mwezi wa Kiislamu siku tatu. Na Muislamu anapofunga siku tatu kila mwezi katika tarehe 13, 14, na 15 za mwezi wa Kiislam, zijulikanazo kama ‘masiku meupe’ thawabu yake ni kama kufunga mwezi mzima.

 

Ama kufunga siku ambazo si Jumatatu au Alkhamiys hasa Ijumaa, Jumamosi au Jumapili hazifai kuzifunga pekee, kwani Ijumaa ni siku kuu yetu, na Jumamosi na Jumamosi ni siku kuu za wasiokuwa sisi. Unaweza kufunga siku nyingine ikiwa tu imesibu kuwa ni siku ambazo zimesuniwa kufungwa kama siku ya Arafah, ‘Aashuraa, siku nyeupe, siku sita za Shawwal, na kadhalika. Unaweza kufunga Ijumaa ikiwa unaendelea na Swawm yako iliyoanzia Alkhamiys au kabla ya hapo, lakini si kuitenga Ijumaa kuifunga peke yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share