Anampenda Sana Mume Wake Lakini Hawana Raha Katika Tendo La Ndoa, Wafanyeje?

SWALI:

 

A'laykum.

 

Mimi nina matatizo katika ndoa yangu hatuna hamu ya kufanya tendo ila tunafanya kwa ada tu ya ndoa. Hatusisimkwi katika tendo huwa hakuna raha ya aina yoyote kati yetu. Mimi huwa sijawahi kusikia raha hata mara moja na pia mume wangu amenithibitishia hilo. Na kuoa mke mwengine hana uwezo wa kifedha wala kumtimizia mahitaji yake ya lazima ni mgonjwa, anachoumwa huwa hakijulikani na pia kuniacha anasema hawezi nahofia atavunja msikiti na kujenga kanisa. Na pia anahofia watoto wake.  Ni kiwa kwetu hunipenda sana na kunitamani.

 

Naomba kwa ajili ya allah munieleweshe nini nifanye kwa huyu mume mimi nampenda mume wangu sana

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumpenda sana mume lakini kutokuwa na raha katika tendo la ndoa.

Furaha ni kwetu kwa kutuelezea kwa uwazi bila kuficha tatizo mlilo nalo. Matatizo kama hayo hutokea katika maisha ya ndoa baina ya wanandoa. Zipo sababu nyingi ambazo hupelekea hilo:

 

1.     Huenda mume aliingia katika ndoa bila kuwa tayari au kutayarishwa katika hilo.

 

2.     Huenda kuwa alichaguliwa bila mwanzo kuwa alikuwa na hamu ya kukuoa.

 

3.     Huenda ya kuwa mume na mke hawajafahamu cha kufanya katika tendo la ndoa.

 

4.     Kukifanya kitendo hicho kuwa ni ada na sio Ibaadah.

 

5.     Huenda mume ana ugonjwa ambao unamfanya asiwe na raghba ya kitendo hicho.

 

6.     Huenda mume amefanyiwa sihri na hivyo kutakiwa kufarakanishwa na mkewe kwa sababu moja au nyingine. Au huenda ikawa ni hasad.

 

Yale yanayotakiwa kufanywa kuhusu matatizo yanayowakumbwa ni kujaribu kwa kiasi kikubwa kufanya yafuatayo:

 

 

1.     Ikiwa aliingia katika ndoa bila kuwa tayari au alichaguliwa bila kupenda ajitayarishe na akuridhie kwa Niyah safi kama mke wako na aache yote mengine nyumbani. Aanze kuganga yajayo. Na kubadilisha kwake kwa Niyah kutawapatia fursa ya kutengeneza hayo msiyosikia kwayo raha.

 

2.     Huenda ikawa hampati starehe kwa kuwa hamjajaribu kupata maelekezo ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu raha hiyo. Kinachotakiwa ni kujitayarisha kwa kitendo hicho kila mmoja kwa mwenziwe. Na huko ni kuoga mkawa safi, kila mmoja kujirembesha kwa mwenziwe kwa kujipaka manukato ili yafumuke mahaba baina yenu. Na inatakiwa mume na mke wapeane mazungumzo matamu yanayohusiana na kitendo ambacho mnataka kukifanya. Na kabla ya kuanza kitendo chenyewe inatakiwa muanze na kushikana sehemu nyeti, kupigana busu na mengineo ambayo yataongeza ashiki ya kila mmoja wenu. Ikiwa mnahisi karibu ya kufikia kilele hapo ndio mnaweza kukamilisha kwa jimai.

 

3.     Mnatakiwa mfahamu kuwa kitendo hicho si ada bali ni ‘Ibaadah kama Swalah, Zakah au Hijjah. Kwa kuwa shughuli hiyo ni ‘Ibaadah ifanywe kwa hamu na kwa ukamilifu.

 

4.     Muwe mnasoma Qur-aan kwa wingi na huku katika nyakati za kujibiwa muwe mnamuomba Allaah Aliyetukuka Awaondolee tatizo hilo. Kwa mfano kuomba mnapofunga kama Jumatatu na Alkhamiys, mnapoinuka usiku wa manane kwa ajili ya Tahajjud na kadhalika

.

5.     Aende mume akasomewe na Shaykh ambaye ni mchaji Mungu na kisomo cha kishari’ah ili ibainike kama amefanyiwa sihri au la.

 

Kwa kufanya hayo tunaamini kuwa kwa uwezo wa Allaah Aliyetukuka atakuwa ni mwenye kupona na kuwa katika hali njema na nzuri inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share