Alimuoa Mwanamke Bila Ya Kumpenda Ila Ameshika Dini Sana, Sasa Hana Raha Naye, Ana Khofu Kumuacha

SWALI:

 

Assalaam aleikum.

 

Mimi ni kijana wa miaka 32, miezi michache iliyopita nilioa binti ambaye kwa hakika mi sijampenda sana, na nilimuoa hasa kutokana na ushawishi nilioupata kutoka kwa watu wangu wa karibu na huruma niliyokuwa nae baada ya kutaka kumwacha nisimuoe nae alihuzunika sana, ila kusema ukweli binti ameshika dini kisawasawa hata kunizidi mimi. Sasa bahati mbaya kwa sasa sina raha kabisa kuwa nae na hata wakati tunakutana kama mke na mume mi hamu zote sina na najihisi karaha, nafikiria kumwacha ila nakosa hoja ya kushika, nahisi kama nitamwacha kwa sababu hiyo watu watasema kwa nini umemuoa mtu usiyempenda. Naomba mnisaidie nifanye nini?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuoa mwanamke usiyempenda.

Hakika mwanaadamu huenda akachukia jambo na likawa na kheri ndani yake kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kadhalika mwanamke mwenye sifa kama hiyo uliyoitaja ndio sifa ambazo Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizipendekeza na akatusisitiza tuolee kwazo. Na wewe umebahatika kulipata hilo lakini inasikitisha kuona kuwa hujaridhika na unapata karaha! Je, karaha ni za nini? Maumbile? Chumbani? Au ni nini zaidi?

 

 

Jambo la pekee ambalo unaweza kufanya ni kumuomba Allaah Aliyetukuka katika Swawm zako na Swalah za usiku akupatie mahaba kwa mke aliyeshika Dini kama huyo.

 

Na kwa kuwa ana mazuri mengi inafaa ujipatie moyo kuwa karaha hiyo itaondoka. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah Ametia kheri nyingi ndani yake” (An-Nisaa’ [4]: 19).

Au njia nyingine ni wewe ukiwa umeshindwa kabisa kuishi naye na unaona utafanya dhuluma kwake na kwa Diyn yako, basi litakalofuatia ni kumpatia talaka, kwani hiyo ndio njia iliyowekwa na Allaah Aliyetukuka ikiwa wanandoa hawapendani. Na kwa kuwa wewe humpendi na ndiye mwenye talaka inafaa umtaliki na si lazima katika kumuacha utoe sababu bali ni riziki ya kuishi pamoja imeisha. Na ikiwa mtafanya hivyo, basi Allaah Aliyetukuka Atampatia kila mmoja wenu wapili wake watakaoridhiana.

 

Tunakuombea kila la kheri katika kuchagua lenye busara na jema. Na ikiwa imepita talaka basi usiingie katika dhulma nyingine kwa kuoa mke kwa kushawishiwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share