Kubandika Jina La Allaah Na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Sambamba Ukutani Au Msikitini

 

SWALI:

 

Jee kuweka saa au majina Allaah subhana wa taala au ya rasululaa salalahu alayhi wasalam mbele ya msikiti inafaa.

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Miongoni mwa vitu ambavyo Shari’ah ya Kiislamu inashinikiza ni kuwekwa pamoja na kuunganishwa kwa Shahada ya Upweke wa Allaah na Shahada ya Ujumbe wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mifano wa miunganisho hii inaonekana katika Adhana ya Swalah na katika Iqaamah. Kwa uzaidi, pia katika Hadiyth ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: kushuhudia kwamba hapana Mola [Anayestahiki kuaabudiwa kwa haki] isipokuwa Allaah, na ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mjumbe wa Allaah…”

 

Hii inawakilisha yale ambayo Mukallaf anapaswa kuamini. Mukallaf ni mtu ambaye Kishari’ah ana uwezo, ana jukumu juu ya vitendo vyake anavyovifanya, na anahitajika kutekeleza yale aliyoamrishwa, ambayo katika Shari’ah ya Kiislamu, yanaanza pindi anapobaleghe. Lazima [hizi Shahada mbili] zifahamike kwa pamoja, na kutamkwa kwa pamoja kama ni ushahidi wa imani.

 

Ama kuhusiana na swali lako kwa kuziandika katika maandishi yaliyoungana ima Msikitini, majumbani na penginepo, hakuna chochote katika haya ambayo yanaweza kupatikana katika Kitabu cha Allaah au katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na natija yake ni kwamba kuna hatari kubwa ndani ya jambo hili [kwa sababu haliko katika Qur-aan wala katika Sunnah]. Kwani haya yanafanana na kanuni ya kiongo ya utatu (trinity) ambayo iko katika Ukristo, dhana ambayo inadai kuwa; baba, mwana, na roho mtakatifu ni mungu mmoja. Zaidi ya hayo, tabia hii ya kuunganisha jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kimaandishi, inaweza kuchukuliwa kuwa kama nembo inayowakilisha dini ya kiongo ya umoja wa kuwepo. Kwa ujumla, inaweza kutumiwa vilevile kutetea uvukaji wa mipaka juu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuabudu yeye pamoja na Allaah.

 

Kwa hiyo, kuandika jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na jina la Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hali kama hii (ya kufanya maandishi ya majina yao yaungane na kuyapandisha maandishi ya majina yao moja juu ya mwenzie, au moja pembeni ya jingine), lazima ikatazwe. Hairuhisiwi hata kuandika (Allaah - Muhammad) katika mlango wa Msikiti, au katika sehemu nyingine yoyote, hii ni kwa sababu ya utata, mawakilisho yasio ya kweli, na mashaka mazito yaliyokwishafafanuliwa na kuonywa juu ya jambo hilo hapo nyuma.

Soma makala ifuatayo kwa faida zaidi:

Je, Umenilinganisha Mimi Kuwa Sawa Na Allaah?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share