Wanandoa Wanapoendeana Kinyume Au Kufanya Maasi Wasameheane Au Waachane?

 

Wanandoa Wanapoendeana Kinyume Au Kufanya Maasi Wasameheane Au Waachane?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalam aleykum.

 

Shukrani za dhati kwa ndugu zetu katika imani ya kiislam ambao mmejitolea kwa hali na mali katika kutuelimisha na In Shaa Allaah akulipeni kheri sisi na nyinyi hapa duniani na aakhirah. Amma ba'ad. suali langu ni hili:  je kama mke wa mtu au mume wa mtu amezini nje ya ndoa na baadae akatanabahi kosa alilofanya  na akamkabili mkewe au mumewe kumuomba samahani, je huyu mume au mke aloombwa samahani ni lipi bora kwake kumsamehe wakarejeana? Au kutomsamehe wakaachana? Na sio zinaa tu bali pia suala langu linakwenda kwa madhambi makubwa mengine kama shirki, kuuwa, kufitinisha n.k. Wassalam aleykum.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Uislamu ni Dini iliyokamilika katika mambo yake yote ya hapa duniani. Toba inatakiwa ifanywe kwa kila dhambi inayofanywa na Muislamu kubwa au dogo. Na mtu yeyote akiomba msamaha hata kwa dhambi kubwa Allaah Aliyetukuka Humsamehe. Hii ni kwa mujibu wa kauli Yake:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az-Zumar: 53].

 

 

Ili kusamehewa aliyefanya dhambi anahitajika kufanya yafuatayo katika masharti:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya hayo.

2.     Ajute sana katika kufanya kosa hilo.

3.     Aazimie kutolirudia tena kosa hilo.

4.   Na kwa kuwa amemdhulumu mwenziwe katika haki yake basi aombe msamaha kutoka kwake.

 

 

Ikiwa mke au mume aliyefanya kosa amerudi nyuma akajirekebisha na kuomba msamaha basi ni bora kusameheana na kuendelea kuishi pamoja. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

خُذِ الْعَفْوَ وَأْمُرْ بِالْعُرْفِ وَأَعْرِضْ عَنِ الْجَاهِلِينَ ﴿١٩٩﴾

Shikamana na usamehevu, na amrisha mema na jiepushe na majahili. [Al-A’raaf: 199].

 

Na katika Aayah nyingine, Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

 

"Na kusamehe ni karibu na uchaji wa Allaah".

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share