Mzazi Kumuuzia Nyumba Mtoto Mmoja

 

Mzazi Kumuuzia Nyumba Mtoto Mmoja

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

assalam aleikum.

swali langu ni:   Tuna nyumba ya familia kubwa kwa majina yetu yaani ndugu sote isipokua jina la baba na mama.  na ikiwa baba ama mama ana nyumba yake mwenyewe  na anataka kumuuziya mmoja wa watoto wao kisheria inawezekana? Ama atakuwa amewadhulumu watoto wengine kwa kuwa hakuwagawiya? tafadhali naomba jibu. 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika ni kuwa mas-ala ya kuuza na kununua yamo katika Dini yetu tukufu. Kuuza na kununua ni kazi na biashara ambayo hutiliwa baraka na Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا ۗ وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ  

Hivyo kwa sababu wao wamesema: “Hakika biashara ni kama ribaa.” Na Allaah Amehalalisha biashara na Ameharamisha ribaa.  [Al-Baqarah: 275]

 

Biashara katika Uislamu kama kazi nyenginezo ina kanuni zake. Mambo kama kughushi, kuficha, kuongeza bei na haja yoyote ile, utovu wa uaminifu, uongo na kadhalika. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msihusudiane, wala msiongezeane bei pasi na kuwa na haja ya kununua wala msichukiane wala msipeane nyongo wala wasinunue baadhi yenu kilichokwisha kuuziwa wenzenu, lakini kuweni enyi waja wa Allaah ndugu” [Al-Bukhaariy, Muslim na Abuu Daawuwd]

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ مِّنكُمْ ۚ وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٢٩﴾

  Enyi walioamini! Msiliane mali zenu kwa ubatilifu, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Allaah ni Mwenye kuwarehemuni. [Al-Maaidah: 29]

 

Aayah tuliyoinukuu hapo juu (Al-Maaidah 4: 29) inatuweka sisi wazi katika mas-ala ya kuuza (au biashara) kwa kuridhiana. Kwa hiyo, msingi mkubwa na mahusiano ya kidamu baina ya wanaouziana bali ni maelewano. Katika Uislamu inajuzu mzazi kumuuzia kitu kilicho miliki yake mtu yeyote hata akiwa mtoto wake. Vile vile inajuzu kwa mtoto kuuza bidhaa yake kwa mtu yeyote hata akiwa ni mzazi wake. Hii nyumba aliyonayo baba bado ni yake na kwa hiyo ana uhuru wa kumuuzia mtoto wake aliye tayari kuinunua kutoka kwake kwa pesa watakazokubaliana.

 

Jambo ambalo halifai ni kwa baba kumrithisha mmoja na kuwaacha wengine. Mas-ala haya yamekatazwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Jambo la urithi tayari Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) keshagawa na mtu kaachiwa thuluthi ya kumtunikia anayemtaka ambaye kisheria si yule mwenye kurithi. Kwa hivyo, baba kumuuzia nyumba mtoto wake inawezekana na hakuna dhulma yoyote kwani yeye yuko huru.

 

Sentensi ya kwanza katika swali lako hatukuifahamu pale uliposema, “Tuna nyumba ya familia kubwa kwa majina yetu yaani ndugu sote isipokuwa jina la baba na mama”. Je, hii nyumba ambayo mzazi ameiuza kwa mmoja wenu ni hii yenu au vipi? Ikiwa jibu ndio, je, ilikuwaje kwa majina yenu, mlinunua au mlikabidhiwa au vipi? Ikiwa mmeimiliki tayari basi itakuwa haifai kwa mama au baba kuiuza nyumba hiyo kwani yeye hayumo katika shirika ya nyumba hiyo. Na ikiwa yumo katika shirika pia hatoweza kuiuza peke yake mpaka washirika wote wawe ni wenye kukubali.

 

Na Allaah Anajua zaidi  

 

 

Share