Amwache Mumewe Nchi Za Ki-Magharibi Ili Arudi Tanzania Kumsomesha Mwanawe Qur-aan?

 

SWALI:

 

ASSALAM ALAYKUM WARAHMATULLAHI TAALA WABARAKATU.MIMI NIKO UENGEREZA NA HUKU WATOO HAWASOMI QUR~ANI KWA JUHUDI KAMA NYUMBANI [ZANZIBAR] NA KUTOKANA NA MASOMO MAPYA YATAKAYOANZA MASKULINI TUNAOGOPA MBELE YA ALLAH KUHUSU UCHUNGAJI WA WATOO, KWA HIVYO NIMEAMUA NIENDE ZANZIBAR KWA AJILI YA MTOTO WANGU NAOMBA MUNIJULISHE ISLAMIC INTERNATIONAL SCHOOL ILIYOBORA. JEE NIKO SAWA MUME WANGU KUMUACHA HUKU IKIWA TUMEKUBALIANA HIVYO.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuacha Mume Uingereza nawe kwenda Zanzibar na mtoto. Na dada yangu mwanzo inatakiwa tufahamu kuwa katika kila nchi haswa za Uzunguni na Afrika Mashariki zina matatizo ikiwa umemtia mtoto wako shule kwani masomo yanayojaliwa huko ni kufuata mtaala wa serikali wa masomo.

 

Kisha, inatakiwa tufahamu kuwa malezi ya mtoto yanahitaji ushirikiano wa baba mzazi na mama. Bila ya hao wawili kutakuwa na kasoro nyingi katika ukuaji wa mtoto mwenyewe. Naona ushauri mwema ni nyinyi wazazi mfanye juhudi ya kumtafutia mtoto wenu shule ya Kiislamu ambayo imefanya indimaj (integration) kwa kusomesha mitaala yote miwili katika jingo moja. Na nadhani huko zipo. Lau si hivyo basi muhame nyote wewe na mumeo muende Zanzibar kwa ajili ya kuishi na kumsomesha kijana wenu.

 

Sijui kama kwa sasa Zanzibar imekuwa na Islamic International school au la kwani mara hapo miaka ya nyuma kulikuwa hakuna. Itabidi kama kuna jamaa zako huko uwasiliane nao kuhusu suala hilo la shule. Na mara nyingine shule zinaitwa kwa jina Islamic lakini hakuna Uislamu ndani yake bali ni kuwavutia Waislamu na kupata pesa zao mbali na kuwa waanzilishaji ni Waislamu.

 

Ikiwa mumeelewana kuwa wewe uende Zanzibar kwa lengo la mtoto kupata mafunzo ya Dini hakuna taabu kisheria lakini itabidi muwe wavumilivu kwani kuna changa moto nyingi. Kuna changa moto ya matamanio kwa mume na mke ndio Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaweka kuwa mujahidina wasikae zaidi ya miezi minne ila warudi wakutane na ahli zao, baadaye warudi tena vitani. Kuna changa moto ya maneno baina ya watu wa mke au mume kupeleka kwa wapili wako na hapo kutoka vurugu. Kuna pia changa moto ya upweke kwa nyote wawili.

 

Hata hivyo, uamuzi ni wenu lakini mnatakiwa mufikirie kwa kina suala hilo kabla kutoa uamuzi wa mwisho. Kwa hiyo, ni muhimu sana mutake ushauri kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuswali Swalah ya Istikhaarah.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share