023-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mazao

 

Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mazao

 

Alhidaaya.com

 

Allaah Amewajibisha kuyatolea Zakaah mazao Aliposema:

 

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

Naye (Allaah) Ndiye Ambaye Aliyezalisha mabustani yanayotambaa na yasiyotambaa. Na mitende na mimea yakitofautiana kwa ladha yake, na zaytuni na makomamanga yanayoshabihiana na yasiyoshabihiana. Kuleni katika matunda yake yanapotoa mazao na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake. [Al-An’aam: 141]

 

Katika kuifasiri Aayah hii amesema Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

'Haki yake, ni Zakaah yake iliyofaradhishwa".

 

Wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Zakaah ya mazao ilikuwa ikitolewa katika Mahindi, Ngano, Mtama, Tende na Zabibu na wengine wakaongeza 'Mchele' na wengine wakasema kuwa Zakaah ya mazao inatolewa katika chakula chochote kile kinachoweza kubaki muda mrefu kama vile mwaka au zaidi bila kuharibika.

 

Matunda, hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa Tende na Zabibu. Matunda mengine hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa kama matunda hayo ni kwa ajili ya biashara, basi hapo itatolewa Zakaah ya biashara na si Zakaah ya Mazao. Zakaah ya Mazao inatolewa siku ya kuvuna na kabla ya kuuzwa wala kuliwa na si lazima itimie mwaka.

 

Niswaab Ya Mazao

 

Mazao hayatolewi Zakaah mpaka yatimie Wiski tano yakiwa safi bila magamba. Kama hayajasafishwa, basi lazima yatimie wiski kumi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Chini ya Wiski tano haitolewi Zakaah". [Imaam Ahmad na Al-Bayhaqiy]

 

Wiski 5 ni sawa na pishi 300, kwa sababu wiski moja ni sawa na pishi sitini kwa pishi iliyokuwa ikitumika wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na pishi sitini mara tano ni sawa na pishi mia tatu.

 

Kwa vipimo vya kisasa:

 

"Niswaab ya mazao ni Wisqi 5. Moja ni kilo 60 yaani kilo 300. Kilo moja ni ratili 13/4 (ratili mbili kasorobo) (300 mara 13/4 = ratili 525).

Kilo karibu ni sawa na pishi ya mbao (vibaba vinne)."

 

Kwa hivyo mazao yakifikia pishi 300 au ratili 525 yanakuwa yamefikia Niswaab yake (kiwango chake) na yatatolewa Zakaah yake ambayo ni moja juu ya kumi (one tenth), hii ikiwa mazao hayo yanapata maji yake bila kuyahangaikia, yaani kama vile kunyeshewa na mvua au maji ya mito au chemchem n.k.

 

Ama ikiwa mkulima anayatilia maji yeye mwenyewe kwa kuyahangaikia maji hayo, basi Zakaah yake itapungua na itakuwa ni nusu ya moja juu ya kumi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kilichonyeshewa na mvua au maji yanayopita (waadi) au yaliyotwama (Zakaah yake ni) moja katika kumi na kilichomiminiwa maji nusu ya moja katika kumi". [Al-Bukhaariy na wengineo].

 

Allaah Ameamrisha kuitoa Zakaah ya mazao; "Siku ya kuvuna kwake", na maana yake ni; kabla hakijaliwa wala kugawiwa chochote kile ndani yake, na ikiwa mtu amekwishafanya hivyo kwa kusahau, basi itambidi akisie kile alichotoa au alichouza na akitolee Zakaah yake.

 

Ama kile alichokula mkulima kabla ya kuvuna, hakimo katika hesabu. Alipoulizwa Imaam Ahmad juu ya wanachokula wenye ardhi kabla ya mavuno alisema:

 

"Hapana neno ikiwa atakula katika mazao yake kiasi anachohitajia".

 

Anasema Shaykh Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:

 

"Kauli hii pia imetamkwa na Imaam Ash-Shaafi’iy na Al-Layth na Ibn Hazm'.

Ama Imaam Malik na Imaam Abuu Haniyfah wanasema:

"Anachokula mtu katika mazao yake kabla ya mavuno atahesabiwa katika Niswaab" [Mwisho wa maneno ya Sayyid Saabiq].

 

Toeni Katika Vizuri

 

Baadhi ya wenye kumiliki mitende walikuwa wakitoa Zakaah yao ya mazao katika tende au zabibu au mazao yasiyokuwa mazuri. Walikuwa wakichagua mazao yasiyokuwa mazuri na kuyatolea Zakaah, na yale mazuri walikuwa wakichukua wenyewe.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَنفِقُواْ مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الأَرْضِ وَلاَ تَيَمَّمُواْ الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلاَّ أَن تُغْمِضُواْ فِيهِ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ

Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi. Na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa na hali nyinyi wenyewe si wenye kuvichukuwa isipokuwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba hakika Allaah ni Mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa. [Al-Baqarah: 267]

 

Anasema Imaam Ash-Shawkaaniy:

 

"Hii ni dalili kuwa, haijuzu mtu kuwapa watu Zakaah katika yale mazao mabovu na yasiyokuwa mazuri."

 

Share