026-Kutoa Zakaah: Zakaatul Fitwr
Kutoa Zakaah: Zakaatul Fitwr
Imefaridhishwa katika mwezi wa Sha'abani mwaka wa 2 baada ya Hijrah (baada ya kuhamia Madiynah). Rasuli wa wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaridhisha Zakaatul Fitwr ili iitakase saumu kutokana na dhambi ndogo ndogo zilizopatikana ndani ya mazungumzo na matendo. Na wakati huo huo Zakaah hiyo iwe msaada kwa mafakiri na wasiojiweza katika kuisherehekea Sikukuu.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaridhisha Zakaah ya Fitwr kwa ajili ya kumtakasa aliyefunga kutokana na dhambi ndogo ndogo za mazungumzo na matendo, na ili wafaidike masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalaah (ya 'Iyd) inakubaliwa kama Zakaah ya Fitwr na atakayeitoa baada ya Swalaah inakubaliwa kama Swadaqah ya kawaida." [Abuu Daawuwd – Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy]
Alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akitoa Zakaah ya Fitwr siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhwaan kabla ya Swalaah ya Idi kuswaliwa. [Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na Al-Hakim]
Kila aliyefunga Mwezi wa Ramadhwaan mwenye kumiliki chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaatul Fitwr, nayo ni pishi ya tende au pishi ya ngano au pishi ya shaiyri. Anatakiwa atowe kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile wanawe, wakeze nk. na kuwapa masikini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.
Kwa vipimo vya kisasa, pishi moja ya mbao iliyokuwa ikitumika wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kiasi cha kilo 2.
Zakaah hii ni wajibu kwa kila Muislam mdogo na mkubwa, mwanamume au mwanamke.
Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha kwa kila mtu kutoa Zakaatul Fitwr katika mwezi wa Ramadhwaan, pishi ya tende (au) pishi ya shaiyri, ikiwa yeye ni mtumwa au mtu aliye huru, mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislam". [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hikmah Yake
Zakaatul Fitwr ilifaridhishwa katika mwezi wa Sha'baan mwaka wa pili baada ya Hijrah kwa ajili ya kumtwahirisha aliyefunga kutokana na makosa yoyote yale aliyotenda katika mwezi wa Ramadhwaan pale alipokuwa amefunga, kama vile mazungumzo ya upuuzi au madhambi, na wakati huo huo Zakaah hiyo itawafaa masikini na wahitaji ili nao wapate kufurahi pamoja na Waislam wenzao siku ya Sikukuu.
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha Zakaatul Fitwr kwa ajili ya kumtahirisha aliyefunga kutokana na maneno ya upuuzi au madhambi madogo madogo na ili masikini nao wapate chakula. Atakayeitoa (Zakaah hiyo) kabla ya Swalaah (ya 'Iyd) inakubaliwa Zakaah yake, ama atakayeitoa baada ya Swalaah (ya 'Iyd), itahesabiwa kama ni Swadaqah ya kawaida tu". [Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy]
Mwenye Kuitoa
Anayeitoa Zakaah hiyo ni mtu aliyefunga. Anajitolea yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wanaomtegemea na anawatolea pia wote wale wanaomtegemea wakiwemo watumishi wake.
Kiasi Chake
Iliyowajibishwa katika Zakaatul Fitwr ni pishi ya ngano au ya shaiyri au ya tende au zabibu au mchele au mahindi na vinginevyo vilivyo na mfano huo katika vyakula.
Imaam Abuu Haniyfah peke yake amejuzisha kutoa pesa zenye thamani hiyo badala ya kutoa nafaka panapo udhuru
Wakati Wa Kuitoa
Wanachuoni wengi wamekubalina kuwa Zakaatul Fitwr itolewe katika Ramadhwaan ya mwisho, lakini wamekhitalifiana juu ya wakati maalum unaowajibika kuitoa.
Wapo waliosema kuwa wakati unaowajibika kuitoa ni pale jua la Ramadhwaan ya mwisho linapozama, na wengine wakasema kuwa wakati wake ni kuanzia baada ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu.
Kutokana na hitilafu hii tunapata faida ya kuwajibika kumtolea Zakaah hiyo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu na baada ya jua kuzama, je mtoto huyo anatolewa Zakaah?
Kwa wale wenye kufuata rai kuwa wakati wa kuitoa Zakaah hiyo ni pale jua la siku ya Ramadhwaan ya mwisho kuzama, mtoto huyo hatolewi Zakaah kwa sababu amezaliwa baada ya kumalizika wakati wa kuwajibika, na kwa wenye kufuata rai ya pili, kwa sababu amezaliwa kabla ya wakati unaomwajibika.
Kuitanguliza
Wanachuoni wengi wanakubali kuwa Zakaatul Fitwr inaweza kutangulizwa na kutolewa kabla ya wakati wake kwa siku moja au mbili.
Hadiythi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) inasema:
"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamrisha kuitoa Zakaatul Fitwr kabla ya watu kutoka msikitini (katika Swalaah ya ‘Iyd)".
Anasema Naafi’ (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Ibn ‘'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiitoa kwa siku moja au siku mbili kabla ya Siku ya Sikukuu".
Ama zaidi ya hapo, Wanachuoni wamekhitalifiana.
Imaam Abuu Haniyfah amesema:
"Inaweza kutolewa wakati wowote ule katika mwezi wa Ramadhwaan".
Imaam Ash-Shaafi’iy amesema:
"Inajuzu kuitoa (hata) katika siku za mwanzo za mwezi wa Ramadhwaan".
Imaam Maalik amesema:
"Inajuzu kutanguliza kwa siku moja au mbili kabla ya Sikukuu".
Lakini Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa haijuzu kuiahirisha na kuitoa baada ya ‘Iyd.