027-Kutoa Zakaah: Swadaqah

 

Kutoa Zakaah: Swadaqah

 

Alhidaaya.com

 

Swadaqah

Muislam anaipa mali yake mtazamo wa aina nyingine kabisa tofauti na asiyekuwa Muislam, kwani dini ya Kiislam inampa kila mtu haki ya kutafuta mali na kufanya biashara ya halali na kuwa tajiri anayeweza kumiliki mali nyingi. Isipokuwa baada ya kuimiliki mali hiyo, analazimika kuwapa maskini Zakaah, ambayo ni haki yao maalum waliyopangiwa na Mola wao Subhanaahu wa Ta’aalaa.

 

Wakati huo huo Muislam anatakiwa ajipatie thawabu nyingi zaidi na ajiepushe na shari nyingi pamoja na kuwasaidia ndugu na jamaa zake, na masikini waislamu wenzake wenye kuhitaji, kwa kutoa kiasi kingine katika mali zao kwa hiari yao wenyewe na kwa kiasi anachokitaka mwenyewe, na hii inaitwa 'Swadaqah'.

 

Kinyume na njia inayotumika katika nchi za Kikoministi za kuwanyang'anya matajiri mali zao kwa nguvu na kuwapa masikini, kitendo cha dhulma na cha ufisadi, kwa sababu binaadamu kwa kawaida wanakhitalifiana katika ujuzi na katika jitihada zao, na kwa ajili hiyo lazima wahitalifiane katika ujira na mapato yao, kwani katika kuwafanya watu wote wawe sawa katika mapato, utakuwa unamweka katika daraja moja mvivu na mwenye kujitahidi, hodari na asiyekuwa hodari, mtaalamu na asiyekuwa mtaalamu.

 

Hii ikiwa mali hiyo wanayonyang'anywa matajiri wanapewa kweli masikini na wale wanaostahiki, na ikiwa watu wote watakuwa sawa kweli, lakini uhakika wa mambo umethithibitisha kuwa yanayotendeka ni kinyume kabisa na maneno yao, kwani wao huwanyang'anya mali matajiri na kuwapa viongozi wa vyama vyao pamoja na vibaraka wao.

 

Allaah Anasema:

مَّا أَفَاء اللَّهُ عَلَى رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَى فَلِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاء مِنكُمْ

Ngawira Aliyotoa Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Allaah na Rasuli na kwa ajili ya  jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na msafiri aliyeharibikiwa, ili isiwe mzunguko wa zamu baina ya matajiri tu miongoni mwenu.

[Al-Hashr: 7]

 

Allaah katika Aayah hii anatujulisha kuwa jamaa na mayatima na masikini na wasafiri walioharibikiwa wana haki zao katika mali zetu, na anawakataza matajiri wasiifanye mali ikawa kinyang'anyiro baina yao tu na kusahau haki za wengine.

 

Muislam pia anatakiwa aitumie mali yake katika kuijenga akhera yake na kujitayarishia Jannah yake.

 

Allaah Anasema:

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الاخِرَةَ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الاَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ

Na tafuta katika yale Aliyokupa Allaah makazi ya Aakhirah. Na wala usisahau fungu lako katika dunia. Na fanya ihsaan kama Alivyokufanyia Allaah ihsaan, na wala usitake ufisadi ardhini. Hakika Allaah Hapendi mafisadi. [Al-Qaswasw: 77]

 

Haya ndiyo mafundisho ya Kiislam yaliyo kinyume kabisa na mafundisho ya mafisadi wanaojishughulisha na kukusanya mali tu na kurimbika, na wakati huo huo yanatufundisha kuwa Musilam hatakiwi abaki msikitini tu akifanya ‘Ibaadah bila kujishughulisha na elimu pamoja na kufanya biashara, na kuwaachia makafiri peke yao katika uwanja wa elimu na biashara na viwanda, na kwa ajili hiyo wanapata nguvu ya kututawala kiuchumi na kielimu, bali Muislam anatakiwa asiisahau pia sehemu yake ya dunia.

 

Allaah Anasema:

وَلا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ

Na tafuta katika yale Aliyokupa Allaah makazi ya Aakhirah. Na wala usisahau fungu lako katika dunia. Na fanya ihsaan kama Alivyokufanyia Allaah ihsaan, [Al-Qaswasw: 77]

 

Dini ya Kiislam inatutaka tuwe msitari wa mbele katika kutoa, na Allaah amewaahidi khayr nyingi wale wanaotoa katika njia Yake.

 

Allaah Anasema:

مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّئَةُ حَبَّةٍ وَاللّهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاء وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja ya mbegu iliyotoa mashuke saba, katika kila shuke kuna punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye; na Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah: 261]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Hakika ya Swadaqah inazima ghadhabu ya Rabb na inamuondolea maiti adhabu" [At-Tirmidhiy]

 

Na akasema:

 

"Haipiti asubuhi wanayoiamkia watu, ila Malaika wawili wanateremka. Mmoja wao anasema: "Allaah muongezee mtoaji badala ya kile anachokitoa". Na mwengine anasema: "Allaah mharibie mali yake (usiite baraka) aliyeacha kutoa ".  [Muslim]

 

Aina Za Swadaqah

Swadaqah haina maana ya kutoa pesa tu au kumsaidia mtu, bali Swadaqah ziko aina nyingi sana.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Kila Muislam anatakiwa atoe Swadaqah".

Wakasema:

"Ee Rasuli wa Allaah, asiyekuwa na mali (je)?"

Akasema:

"Afanye kazi kwa mikono yake, ajisaidie nafsi yake kisha atoe Swadaqah".

Wakasema:

"Ikiwa hajapata?"

Akasema:

"Amsaidie mwenye shida".

Wakasema:

"Asipompata?"

Akasema:

"Afanye mema na aache shari, kwani akifanya hivyo anaandikiwa (thawabu ya) Swadaqah".

[Al-Bukhaariy na wengineo]

 

Na katika riwaya nyingine amesema:

"Kila siku jua linapochomoza nafsi inaandikiwa juu ya kila inachotenda (katika thawabu ya) Swadaqah. Katika hayo ni kuwapatanisha wawili wanaogombana (anaandikiwa mtu thawabu ya kutoa) Swadaqah. Akimsaidia mtu kumnyanyua ili aweze kumpanda mnyama wake, anaandikiwa Swadaqah, akimnyanyulia mzigo wake, Swadaqah, kuondoa udhia barabarani, Swadaqah, neno jema, Swadaqah, na kila hatua anayokwenda msikitini Swadaqah". [Ahmad na wengineo]

 

Na akasema:

"Kati yenu kama yupo mwenye kuuogopa moto, basi atoe Swadaqah walau kwa nusu ya tende, na asiyepata, basi kwa neno jema”. [Ahmad na Muslim]

 

Na akasema:

"Siku ya Qiyaamah Allaah Atasema:

"Ee mwana Aadam, niliumwa (kwa nini) hukunitembelea?"

Atasema (mwana Aadam):

"Ee Rabb, vipi nitakutembelea na wewe ni Mola wa Ulimwengu?"

Atasema:

"Hukujua kuwa mja wangu fulani alikuwa akiumwa na hukumtembelea? Ama ungelimtembelea, ungelinikuta kwake. Ee mwanaadamu nimekuomba chakula na wewe hukunilisha?"

Atasema:

"Ee Rabb wangu, vipi nitakulisha na wewe ni Rabb wa ulimwengu wote?"

Atasema:

"Hukujuwa kuwa fulani alikuomba chakula na hukumpa. Huelewe kuwa ungelimpa chakula, ungelikikuta kwangu?

Ee mwanaadamu, nilikuomba maji hukunipa".

Atasema:

"Ee Rabb wangu, vipi nitakunywesha nawe ni Rabb wa Ulimwengu wote?"

Atasema:

"Mtu fulani alikuomba maji, na wewe hukumpa. Ama ungelimpa ungeyakuta hayo kwangu".

[Muslim]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema pia:

"Mtu hapandi kitu au halimi kitu kisha mwana Aadam akala katika mazao hayo au mnyama au chochote ila ataandikiwa kwa ajili yake Swadaqah". [Ahmad na At-Tirmidhiy]

 

Na akasema:

"Kila wema ni Swadaqah, na katika wema ni kumkabili mwenzio kwa uso wa bashasha… (uso mkunjufu)." [Ahmad na At-Tirmidhiy]

 

Wenye Kustahiki Zaidi

Watu wako, mkeo na watoto wako pamoja na ndugu zako wa nasaba ndio wanaoistahiki zaidi Swadaqah yako.

 

Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mmoja wenu akiwa fakiri, basi ajitosheleze nafsi yake, kinachozidi awape watoto wake, kinachozidi, awape ndugu zake wa nasaba, na kikizidi basi atoe huku na kule". [Ahmad na Muslim]

 

Hukumu ya Swadaqah inahitilafiana na ya Zakaah, kwani mali ya Zakaah haijuzu kupewa asiyekuwa Muislam, lakini Swadaqah anaweza kupewa asiyekuwa Muislam.

 

Allaah Anasema:

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka. [Ad-Dahar: 8]

 

Neno lililotumika kwa 'wafungwa', katika aya hii ni 'Asiyran', na maana yake ni mateka wa kivita ambaye bila shaka ni kafiri aliyetekwa baada ya kupigana vita dhidi ya Waislam, lakini juu ya hivyo Allaah anawasifia Waislam wanaowalisha chakula wafungwa hao.

 

Kuiharibu Swadaqah

Haijuzu kumsimbulia au kumdharau anayepokea Swadaqah kwa sababu kilichomfanya akubali kuipokea Swadaqah hiyo ni umasikini wake, na mtu kumtakabaria masikini ni dhambi kubwa sana, na anapofanya hivyo thawabu zake zinapotea bure.

Allaah Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُبْطِلُواْ صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالأذَى كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاء النَّاسِ وَلاَ يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ

Enyi walioamini! Msibatilishe swadaqah zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake kwa kujionyesha kwa watu wala hamwamini Allaah na Siku ya Mwisho.

[Al-Baqarah: 264]

 

 

Kutoa Katika Mali Ya Haramu

 

Allaah haikubali Swadaqah ikiwa inatokana na mali ya haramu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Enyi watu! Allaah ni mzuri na hakubali isipokuwa kizuri tu".

 

Imesimuliwa kuwa siku moja mtu mmoja aliiba tufaah kisha akaliuza, na pesa alizopata akawagawia masikini.

 

Habari zilipomfikia Qaadhi wa mji huo, akamwita na kumuuliza:

"Kwa nini umeiba kisha ukazigawa Swadaqah pesa za mali ya wizi?"

Yule mtu akajibu:

"Kwa sababu Allaah Anasema:

مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا

Atakayekuja kwa ‘amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo. Na Atakayekuja kwa ovu basi hatolipwa ila mfano wake... [Al-An’aam: 160]

 

Kwa hivyo, akaendekelea kusema mtu Yule aliyeiba tufaa: ‘Kutokana na aya hii, mimi nilipoiba tufaa nilifanya kitendo kibaya nikalipwa dhambi moja tu sawa na tufaa moja nililoiba, lakini nilipowagawia masikini nilifanya kitendo chema nikalipwa mara kumi, na thawabu 10 nilizozipata kwa kuligawa tufaa lile,ukitoa ile dhambi moja ya kuiba, nitabakiwa na thawabu tisa"

Qaadhi akamwambia:

"Lakini umesahau jambo moja ewe ndugu Muislam, (Allaah ni mwema, na hakubali isipokuwa chema tu).”

 

Kuwasaidia Wanyama

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwaambia Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum):

"Mtu mmoja aliyekuwa akitembea, alishikwa na kiu, akaona kisima mbele yake, akateremka na kunywa maji ndani yake kisha akatoka. Alipokuwa akitoka alimuona mbwa akihema kwa kiu. Yule mtu akasema; "Bila shaka mbwa huyu ameshikwa na kiu kama nilivyoshikwa mimi. Akateremka (tena) kisimani, akajaza maji kiatu chake, kisha akamshika kichwa chake mbwa yule na kumnywesha.

Akashukuriwa na Allaah na kughufuriwa".

Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakasema:

"Hata katika wanyama tunapata thawabu?"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Katika kila chenye uhai mna thawabu". [Al-Bukhaariy]

 

Swadaqatun Jaariyah

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mwanaadamu anapokufa, amali zake zote zinakatika isipokuwa tatu. Swadaqatun Jaariyah (Swadaqah inayoendela), au elimu yenye kunufaisha watu, au mtoto mwema anayemuombea". [Ahmad na Muslim]

 

Kushukuru

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Atakayekufanyieni wema mlipeni, na ikiwa hamna cha kumlipa, basi muombeeni dua mpaka muhisi kuwa mumemlipa". [Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

Imesimuliwa na Imaam Ahmad kutoka kwa Al-Ash’ath bin Qays kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hamshukuru Allaah yule asiyewashukuru watu." [Ahmad]

 

Na akasema:

 

"Aliyetendewa jema, akasema kumwambia aliyemtendea: “Jazaaka Allaahu khayran', (Allaah  Akujaze khayr), huyo amekwisha shukuru kama inavyotakikana".

 

Share