Qiyaamah Kitatufikia Tu Lakini Tumeghafilika Nacho

Qiyaamah Kitatufikia Tu Lakini Tumeghafilika Nacho

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مُّعْرِضُونَ ﴿١﴾ مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ ﴿٢﴾

 

Imewakaribia watu hesabu yao, nao wamo katika mghafala wanakengeuka (na wanapuuza).  Hauwafikii Ukumbusho wowote ule mpya kutoka kwa Rabb wao isipokuwa huusikiliza kwa makini na huku wao wanacheza. [Al-Anbiyaa: 1 – 2]

 

 

Hili ni onyo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa watu kuhusu kukaribia kwa Qiyaamah lakini watu wameghafilika nacho, kwa maana kwamba hawajitahidi kuifanyia kazi au hawajitayarishi nacho.

 

Abu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) amesikia kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu:

 

فِي غَفْلَةٍ مُّعْرِضُونَ ﴿١﴾

katika mghafala wanakengeuka (na wanapuuza).

 

Kwamba ni: Katika dunia.  [Imaam An-Nasaaiy]  

 

 

Mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sauti kubwa alipokuwa naye katika msafara:

 

 " يا محمد" و فقال له النبي صلى الله عليه وسلم نحوا من صوته ((هاؤم)). فقال:  "متى الساعة؟"  فقال له رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ويحك, إنها كائنة، فما أعددت لها؟)) فقال: "حُب الله ورسوله" . فقال: ((أنت مع من أحببت))

 

"Ee Muhammad!" Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu naye kwa sauti: ((Niko hapa!)). Yule Mtu akasema: "Lini Saa (Qiyaamah) itafika"? Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ole kwako, itafika tu. Je, umefanya nini kujitayarisha nacho?)) Akasema: "Mapenzi ya Allaah na Rasuli Wake." Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Wewe utakuwa pamoja na wale unaowapenda)) [Fat-h Al-Baariy 10: 573, Muslim 4: 2033]

 

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

أَتَىٰ أَمْرُ اللَّـهِ فَلَا تَسْتَعْجِلُوهُ ۚ  

Amri ya Allaah (ya Qiyaamah) itafika tu basi msiihimize.  [An-Nahl: 1]

 

Inamaanisha: kilichokuwa mbali sasa kiko karibu kwa hiyo msihimize.

 

Wasioamini hukiulizia kwa kejeli na kuhimiza kifike. Ama walioamini wao wanakhofu nacho kwani wanajua kwamba ni haki na kwamba kitatokea tu bila shaka. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

اللَّـهُ الَّذِي أَنزَلَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ وَالْمِيزَانَ ۗ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ قَرِيبٌ﴿١٧﴾ يَسْتَعْجِلُ بِهَا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِهَا ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا مُشْفِقُونَ مِنْهَا وَيَعْلَمُونَ أَنَّهَا الْحَقُّ ۗ أَلَا إِنَّ الَّذِينَ يُمَارُونَ فِي السَّاعَةِ لَفِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ﴿١٨﴾

Allaah Ambaye Ameteremsha Kitabu hiki kwa haki na mizani. Na nini kitakachokujulisha pengine Saa (Qiyaamah) iko karibu? Wanaihimiza wale wasioiamini; na wale walioamini wanaiogopa na wanaitambua kwamba hiyo ni haki. Tanabahi!  Hakika wale wanaotilia shaka kuhusu Saa; bila shaka wamo katika upotofu wa mbali. [Ash-Shuwraa: 17 – 18]

 

Na wengine wanaona kuwa hiyo adhabu itakayowafikia Siku ya Qiyaamah iko mbali lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa iko karibu kabisa:

 

إِنَّهُمْ يَرَوْنَهُ بَعِيدًا﴿٦﴾ وَنَرَاهُ قَرِيبًا﴿٧﴾

 

Hakika wao wanaiona (adhabu, Qiyaamah) iko mbali. Nasi Tunaiona  ikaribu. [Al-Ma'aarij: 6 - 7]

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akitaka, ni Mwenye uwezo wa kukileta haraka zaidi kuliko upepeso wa macho kama Anavyosema:

 

  وَمَا أَمْرُ السَّاعَةِ إِلَّا كَلَمْحِ الْبَصَرِ أَوْ هُوَ أَقْرَبُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٧٧﴾

Na wala haikuwa amri ya Saa isipokuwa kama upepeso wa jicho au karibu zaidi. Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Muweza. [An-Nahl:77]

 

 

Hivyo inatupasa Waislamu tujitayarishe nacho Qiyaamah kwa kutenda mema mengi na kujiepusha na maovu ili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atulipe Jannah (Pepo) kwani Jannah haipati mtu kwa wepesi ila kwa kuifanyia kazi kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿٥٨﴾

 

Na wale walioamini na wakatenda mema, bila shaka Tutawawekea makazi ya ghorofa katika Jannah, yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje ujira wa watendao. [Al-‘Ankabuwt: 58]

 

 

*******

 

 

 

 

 

Share