Taraawiyh: Maswali Mbali Mbali Kuhusu Swalaah Ya Taraawiyh, Witr Na Du'aa Ya Laylatul-Qadr
Maswali Mbali Mbali Kuhusu Swalaah Ya Taraawiyh, Witr Na Du'aa Ya Laylatul-Qadr
SWALI:
Assalaam 'Alaykum Warahmatullah,
Inshalla Allah atuwezeshe kuifunga Ramadhwaan kwa Iman na Ikhlas na wingi wa Rehma zake, Amin.
1) Nilikua na maswali kidogo tu kuhusu dua hii: "ALLAHUMMA INNAKA 'AFUWUN TUHIBUL-'AFUA...... Jee ina wakati maalum wa kuiomba dua hii au wakati wowote??
2) Na vipi katika taraawiyh kama ilivyozoeleka husomwa kila baada ya salam ni sunna au haina neno au sio pahala pake.
3) Jee kuna dua yeyote iliyosunniwa katika tareweh au.
4) Ikitokezea kuswali Witri mara tu baada tareweh, bahati ukaamka usiku kusali kuna ubaya wowote? Ukizingatia kwamba witri ni kama kifungio cha sala za usiku.
5) Mwisho naomba unifahamishe sala za usiku kisunna ni rakaa ngapi, unatoa salam kila baada muda gani na sura gani inazopendekezwa kissuna kusomwa.
Inshallah Allah atatuwafikisha kwa haya.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
SWALI LA KWANZA:
Nilikua na maswali kidogo tu kuhusu dua hii:"ALLAHUMMA INNAKA 'AFUWUN TUHIBUL-'AFUA...... Jee ina wakati maalum wa kuiomba dua hii au wakati wowote??
JIBU:
Kuhusu Du'aa uliyoitaja 'Allahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbbul-'afwa Fa'fu 'Anniy'
Dua hii unaweza kuomba wakati wowote ule unaopenda kwani ni dua'a mojawapo ya kuomba msamaha kutoka kwa Mola Mtukufu, na khaswa kuiomba siku za Laylatul-Qadr kwani ndivyo ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
Imetoka ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba alisema "Ee Rasuli wa Allaah, je, nitakaposimama usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema, ((Sema Ee Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi nisamehe)) Ibn Maajah na kaisahihisha Albaniy
SWALI LA PILI:
Na vipi katika taraawiyh kama ilivyozoeleka husomwa kila baada ya salam ni sunna au haina neno au sio pahala pake
JIBU:
Kuombwa Du'aa hiyo na kuifanya mahsusi katika Taraawiyh kila baada ya salaam au kuifanya mahsusi wakati ma'aalum sio Sunnah, bali kama tulivyosema kuwa wakati wowote mtu anaweza kuiomba na wakati wake maaluum ni katika Usiku wa Laylatul-Qadr kama ilivyothibitika katika Hadiythi hiyo ya juu.
SWALI LA TATU:
Jee kuna dua yeyote iliyosunniwa katika tareweh au?
JIBU:
Hakuna Du'aa iliyokuwa Sunnah kuomba wakati wa Taraawiyh kama wanavyofanya baadhi ya watu katika kila mapumziko ya Raka'ah nne husoma tasbiihi fulani na kuzifanya mahsusi za Taraawiyh. Hili ni jambo lisilokuwa na dalili katika Sunnah, kwa hiyo inapasa Muislamu kujiepusha nalo.
Ama katika Swalaah ya Witr ikiwa ni katika Taraawiyh ya Ramadhwaan au miezi mingine, dua zilizothibiti katika Sunnah ni du'aa zinazosomwa katika Qunuwt, ambayo ni katika Raka'ah ya mwisho ya Witr, nazo utazipata katika kiungo hiki kifuatacho ambazo zote zimo katika Kitabu cha Hisnul-Muslim kilichokuweko katika AL HIDAAYA katika 'Duaa na Adhkaar'
Bonyeza hapa :
SWALI LA NNE
Ikitokezea kuswali Witri mara tu baada tareweh, bahati ukaamka usiku kusali kuna ubaya wowote? Ukizingatia kwamba witri ni kama kifungio cha sala za usiku
JIBU:
Hakuna ubaya wowote kuswali Swalaah za baada ya kuamka usiku (Tahajjud) hata kama ulikuwa umeshaswali Witr kabla ya kulala. Lakini ukimaliza kuswali Swalaah mbili mbili utakazojaaliwa, basi haikupasi tena uswali Witr kutokana na kauli ya Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم
((لا وتران في ليلة)) رواه الترمذي
((Hakuna Witri mbili katika usiku)) [At-Tirmidhiy]
‘Ulamaa wanasema kuwa unaweza kuswali witr tena au Qiyaamul-Layl baada ya Taraawiyh (ingawa pia Taraawiyh ni Qiyaamul-Layl vilevile) usiku zaidi karibu na alfajiri kwa anayetaka lakini kwanza aswali raka’ah moja kuivunja ile witr aliyoswali na Imaam kisha ndipo aswali tena mwisho witr ya kufungia.
SWALI LA TANO:
Mwisho naomba unifahamishe sala za usiku kisunna ni rakaa ngapi, unatoa salam kila baada muda gani na sura gani inazopendekezwa kissuna kusomwa
a-Idadi ya Swalaah za Sunnah za usiku
JIBU:
a-Jumla ya Swalaah za usiku za Sunnah ni Raka'ah kumi na moja kutokana na Hadiythi ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku Raka'ah kumi na akitoa salam baada ya kila Raka'ah mbili kisha akiswali Witr Raka'ah moja) Muslim
Na akasema vile vile Hajapata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzidisha katika Ramadhwaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja, akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali tatu)) Al-Bukhariy na Muslim
b-Namna zinavyoswaliwa Swalaah za usiku
Unatoa salam kila baada ya Raka'ah mbili kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
((صلاة الليل مثنى مثنى فإذا خشيت الصبح أوتر بواحدة))" أخرجه البخاري
((Swalaah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na ukiogopa kukukuta asubuhi basi Swali Witr [Raka'ah] moja)) Al-Bukhariy
c-Sura za kusoma katika Swalaah ya usiku
Hakuna Sura Maaluum ya kusomwa katika Swala za usiku, bali ni vizuri sana kusoma sura ndefu kwani kama hadithi ya 'Aishah iliyotajwa hapo juu kuwa alisema 'wala usiniulize uzuri wake' akikusudia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah kwa utulivu kabisa kwa kusoma mara nyingine sura ndefu, Rukuu ndefu, sujuud ndefu na kadhalika.
Ifuatayo ni Hadiyth inayoonyesha fadhila za kusoma aya nyingi katika Swalaah ya usiku:
عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وسلم ((من قام بعشرِ آياتٍ لم يُكتبْ من الغافلينَ ، ومن قام بمئةِ آيةٍ كُتبَ من القانتينَ ومن قام بألفِ آيةٍ كُتبَ من المُقَنْطِرينَ)) صحيح أبي داود
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesimama usiku kuswali na akasoma Aayah kumi, hatoandikiwa kuwa miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah mia, ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah elfu, ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi (ya thawabu).’ [Abuu Daawuwd, Al-Albaaniy ameisahihisha: Swahiyh Abiy Daawuwd (1398), Swahiyh Al-Jaami’ (6439)]
(Maana ya mirundi ni wale walio na mrundi wa thawabu)
Ama katika Raka'ah tatu za mwisho imethibitika kuwa alikuwa akisoma sura hizi:
Hadiyth kutoka ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Raka'ah ya mwanzo ya (Swalaah) Witr 'Sabbihisma Rabikal-A'ala' na Raka'ah ya pili 'Qul-Yaa-Ayyuhal-Kaafiruwn' na Raka'ah ya tatu 'Qul- Huwa-Allaahu Ahad pamoja na Qul-A'udhu mbili (Al Falaq na An Naas)' At Tirmidhiy
Raka'ah hizi tatu za mwisho vile vile ziswaliwe mbili kwanza kisha umalizie na moja pekee, na katika hiyo raka’ah ya mwisho bada ya kuinuka katika ruku'u usome du'aa ya Qunuwt. Au ziswaliwe zote tatu kwa tash-shahud moja tu ya mwisho na kisha kutoa salaam, yaani bila kusoma At-Tahiyaat kwenye raka’a ya pili, na kufanya huku wanasema Ma'ulamaa ni kuitofautisha na Swalaah ya Maghrib ambayo unakaa At-Tahiyaat kwenye raka’ah ya pili.
Na Allaah Anajua zaidi