Janaba: Kulala Na Janaba Na Kuamka Na Swawm Je, Swawm Inakubalika?
Janaba: Kulala Na Janaba Na Kuamka Na Swawm Je, Swawm Inakubalika?
SWALI:
asalam aleikum
swala langu ni ikiwa mtu amelala na janaba siku ya ramadhan akamka asubuhi je saum ina swih ama itakuwa haifai
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Asli katika mas-ala ni kuwa Swawm ya mtu mume au mke haibatiliki kama ataamka wakati wa Alfajiri na janaba iwe janaba kwa sababu ya kulala na ahli yake au kwa kutoa kama ilivyothibiti katika Hadiyth Ya Mama wa Waumini ‘Aaishah na Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) wamesema:
“Kwa hakika Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa ’ala aalihi wa sallam) alikuwa inamdiriki Alfajiri hali ya kuwa na janaba kutokana ahli zake, kisha hukoga na kufunga” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, Kitaab cha Swawm, mlango mwenye Swawm na kuamka na janaba].
Ingawa pamoja na kanuni ya ki-Uswuwl inayothibitisha kuwa kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hutangulizwa kuliko kitendo chake; yaani kauli yake ndiyo hufanyiwa kazi endapo itagongana na kitendo alichofanya yeye, na kwa sababu kuna Hadiyth kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) anayosema kuwa alisikia kuwa mwenye kuamka na janaba hana Swawm, lakini kama anavyoeleza Imaam An-Nawawiy katika sharh ya Swahiyh Muslim, kuwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipofikishiwa maelezo ya wake za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na 'Abdur-Rahmaan bin Haarith kuthibitisha kwao kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliamka na janaba na akajitwaharisha na kuendelea na Swawm, Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu kuwa wao (wake za Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni wajuzi zaidi, na akarejea na kauli yake na kuwafikiana na kauli za wake za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Imaam An-Nawawiy anasema kwa kuzilinganisha Ahaadiyth hizo zote, kuwa iliyo Swahiyh ni kuwa Swawm ya mwenye kuamka na janaba ni sahihi kabisa.
Msimamo huu vilevile ndio wamekubaliana Wanachuoni wengi. Imaam Muslim katika Swahiyh yake, kaweka mlango unaohusu Ahaadiyth hizo, na kuuita: باب صحة صوم من طلع عليه الفجر وهو جنب (Mlango wa kusihi Swawm kwa iliyomchomozea Alfajiri akiwa na janaba), kuthibitisha naye kuwa Swawm ya mwenye kuamka na janaba ni sahihi.
Hivyo basi hukumu ni kuwa Swawm haijabatilika, bali ipo na inaendelea kwa kila atakayelala usiku na kuamka na janaba, na mwenye kulala mchana na kuota ndoto ya utu uzima, awe mwanamume au mwanamke.
Kitachomlazimu ni kufanya ghuslu (kuoga josho) pindi aamkapo na kuendelea na Swawm yake na hana kulipa wala fidia kwani hana kosa lolote.
Na Allaah Anajua zaidi