Tofauti Ya Miezi Ya Kiislamu (Hijriyyah) Na Ya Miladi Zipi Sifa Zake?
Tofauti Ya Miezi Ya Kiislamu (Hijriyyah) Na Ya Miladi Zipi Sifa Zake?
SWALI:
Ni kwa nini miezi ya kiislamu inakuwa sanjari na miezi ya kimagharibi lakini inakuwa tofauti katika muda.
Naomba nakala ya kalenda iliyo na mchanganyiko wa miezi ya pande zote. Zipi sababu za kuitwa mwezi fulani na kisa cha kila mwezi au siku katika mwezi fulani, mfano: siku ya 9 na 10 mfungo nne nilipata kusimuliwa kuwa ndiyo Bani Israil waliangamizwa kwa kumuasi allah (Subhanahu wa Ta'ala).
Kwa nini kila mwezi una sifa zake na hakuna mfanano wa sifa na kama zipo ni zipi?
ALLAH (Subhanahu wa Taala) awalipe kwa yote myatendayo na wajaze kheri. In shaa Allah.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tutajaribu kufafanua kwa kadiri tulivyolifahamu swali lako.
Mwanzo inatafaa tuelewe kuwa kuna tofauti ya msingi baina ya miezi ya Kiislamu na mingine. Miezi ya Kiislamu inafuatana na mwandamo wa mwezi ambao kila mwezi unakuwa na siku 29 au 30 ilhali miezi ya Kimagharibi inafuata jua, hivyo kufanya siku zake kuwa 28, 29 kwa Februari na kawaida ni 30 au 31. Kwa ajili hiyo, mwaka wa Kiislamu unakuwa na takriban siku 11 kidogo kuliko mwaka wa Kimagharibi.
Ama kuhusu miezi ya Kiislamu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Aliyeifanya kuwa kumi na mbili, minne ikiwa ni mitukufu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ ۚ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ﴿٣٦﴾
Hakika idadi ya miezi mbele ya Allaah ni kumi na mbili katika hukmu ya makadirio ya Allaah, (tangu) siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo, (iko miezi) minne mitukufu. Hivyo ndiyo Dini iliyo nyoofu. Basi msijidhulumu humo nafsi zenu (kwa kufanya maasi), na piganeni vita na washirikina wote kama wao wanavyokupigeni vita nyote. Na jueni kwamba Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa. [At-Tawbah: 36]
Ama kuhusu nakala za kalenda kukutumia kwa njia ya mtandao inakuwa si wepesi kwani hizo zinachapishwa na kuuzwa katika miji na nchi tofauti. Kinachotakiwa ni wewe kwenda katika maduka yanayouza vitabu vya Kiislamu na kununua moja ili uweze kuwa nayo na kutazama unayoyahitaji. Au unaweza kuipata katika mitandao.
Ama kuhusu sababu ya kuitwa majina ya miezi ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Mwenye kujua zaidi kwani Yeye haulizwi Anayofanya, sisi ndio wenye kuulizwa.
Ama kuhusu siku zina tarehe na majina yake zilizopatiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano ni:
1-Tarehe 10 wala sio tisa ya Mfungo Nne (yaani Al-Muharram). Siku hiyo inaitwa ‘Aashuraa nayo ni kwa ajili ya Bani Israaiyl wakati wa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) waliokolewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) sio kuangamizwa kama ulivyo sema. Kwa ajili ya kuokolewa huko, wakawa wanafunga siku hiyo kama kutoa shukran kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akatuongezea tarehe tisa ambayo inayojulikana kama Taasuaa’ ili tufunge siku hizo mbili tutofautiane na Mayahudi.
2-Tarehe 9 ya Dhul-Hijjah inajulikana kama siku ya ‘Arafah, kwani katika siku hiyo Mahujaji wanasimama katika wangwa wa ‘Arafah ili kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kutimizia nguzo ya Hajj.
Miezi ya Kiislamu ina sifa tofauti kwa kupatiwa sifa hizo na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake, ima kwa sababu ya kufanywa ‘Ibaadah miongoni mwa ‘Ibaadah kwa sababu nyingine yoyote ile.
Na Allaah Anajua zaidi