Meno Ya Dhahabu Ni Haramu Kubandika?

 

SWALI:

asalam alaikum, suali langu ni hili:mtu akibandika meno ya dhahabu ni haramu? Je, akisuali nayo swala itakubaliwa


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hili kuhusu mas-ala ya kutia meno ya dhahabu. Hakika ni kuwa meno ya dhahabu yanaweza kuwekwa na Muislamu kwa dharura inayokubalika kisheria. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth iliyosimuliwa na Arfajah bin As‘ad: Abdur-Rahmaan bin Tarafah alisema kuwa babu yake Arfajah ibn As‘ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikatwa pua yake katika vita vya Kilaab, hivyo akatia pua ya fedha, lakini ikaanza kunuka. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuamuru atie pua ya dhahabu (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy). Hadiyth hii inatuonyesha jinsi Sheria yetu Tukufu inavyotazama maslahi ya mwanadaamu kwa kiwango kikubwa sana ili mwanadamu kama huyo asiwe ni mwenye kudhurika kwa chochote. Kwa minajili hiyo hata kile kitu ambacho ni haramu kikapewa ruhusa ili kusaidia kuleta nafuu kwa mwanadamu.

Kwa hiyo, ikiwa ipo dharura ya kisheria kutia jino la dhahabu kutakuwa hapana shida yoyote ile.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share