Wanawake Wawili Wanaweza Kuswali Jama’ah? Vipi Iswalishwe? Wanaweza Kuswali Nyuma Ya Wanaume Wakiwa Shuleni?

 

SWALI:

 

ASALAM ALEYKUM WARAHMATULAH WABARAKAT, Mimi ni msichana naomba mnifahamishe kuhusu swala ya jamaa maana navyofahamu kwamba msichana aswali nyumbani, je nikiswali peke yangu si ntakuwa nimekosa swala ya jamaa? Na pia tupo wasichana wawili tunaweza tukajiswalisha swala ya jamaa na kama inaswihi inaswaliwaje? Pia nipo nchi ya ulaya shuleni kipindi cha swala huwa tunaswali darasani lkn muda hautoshi kuswali wanaume peke yao alafu na wanawake peke yao je tukiingia pamoja na wanaume tukaswali swala ya jamaa hali ya kuwa wanaume wapo mbele na sie tukiwa nyuma yao je itaswihi? ASALAM ALEYKUM WARAHMATULAH WABARAKATU.Naomba mnijibu kwenye email yangu

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Swalah ya jama’ah kwa wanawake.

Hakika ni kuwa msichana kuswali nyumbani kwake ni bora kuliko kuswali Msikitini kwa jama’ah japokuwa hawakatazwi kwenda Msikitini. Ikiwa mko wasichana nyumbani ni bora kuswali kwa jama’ah kwani kufanya hivyo mtakuwa mnahimizana katika Swalah na uvivu utaondoka baina yenu.

 

Swalah ya wanawake inakuwa tofauti na ya wanaume, kwa kuwa katika Swalah hiyo Imaam kwa wanawake hasimami peke yake mbele bali husimama safu moja, Imaam upande wa kushoto wa maamuma wake akiwa upande wa kulia wakiwa wako sawasawa.

 

Ama kuswali wanaume na wanawake pamoja, wavulana mbele na wasichana wapo nyuma katika jama’ah ni jambo ambalo linafaa kabisa kishari’ah wala halina tatizo. Inatakiwa tu maadili na muruwa za Kiislamu zihifadhiwe kabisa kusiwe na ukosefu wa adabu. Na katika hilo ikiwa kuna mlango wa kuingilia na kutokea zaidi ya mmoja, kuwe na mlango/ milango makhsusi wa wasichana na mingine kwa wavulana ili kusiwe na mchanganyiko wa kupigana kumbo wakati wa kuingia au kutoka. Ikiwa mlango ni mmoja tu, mtakuwa hamuna budi ila Swalah inapomalizika wasichana watoke mwanzo, baada yao ndio wavulana watoke.

 

Bonyeza vungo vifuatavyo  upate maelezo zaidi

 

Swalah Ya jamaa Inafaa Nyumbani?

 

Swalah Ya Jamaa Baina Ya Mume, Mke Na Mtoto Wa Kiume

 

Wanawake Lazima Waende Kuswali Ijumaa Msikitini?

 

Wanawake Kuswali Adhuhuri Nyumbani Kabla Ya Ijumaa Kuswaliwa

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share