Kusujudu Mara Tu Unapomkumbuka Allaah

SWALI:

 

Asalamu alaikum

Napenda kuuliza hivi je inafaa kama mtu yu watembea kisha ukamkumbuka Allaah s.w kisha ukasujudu palepale kwa ajili yake. wabilah taufiq

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kusujudu baada ya tu kumkumbuka Allaah Aliyetukuka.

 

Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisujudu alipowasomea makafiri Quraysh Suratun Najm na alipofika mwisho wa Surah alisujudu pamoja na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) na Maquraysh wote wakasujudu juu ya mchanga mpaka wengine kwa kukosa nafasi wakasujudu juu ya migongo ya wenziwao. Na hivyo ndivyo ipasavyo unaposoma Aayah zenye sajda.  Ama kusujudu unapomkumbuka tu Allaah Subhaanah wa Ta’ala hatukupata mafunzo ya haya, hivyo ni vyema kutokusujudu. Bali kumbuka Allaah ni aina ya ibaada ya kutafakari, na ina thawabu nyingi, hivyo inatosha kujipatia thawabu kila unapomdhukuru Allaah.

 

 

Na hali nyengine ya kusujudu ni ile hali ya kuwa mtu yu juu ya kipando kinachokwenda kama walipokuwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Katika hali hiyo unatoa ishara ya kusujudu kwa kuinamisha kichwa na huko kutakuwa sawa kabisa.

 

Kadhalika pindi upatapo habari ya furaha au habari njema unaweza kusujudu kama alivyofanya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma). Na kusujudu huko  waweza kusujudu popote bora pawe hapana najisi juu yake ikiwa unasujudu barabarani au kiwanjani au ofisini.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share