Vita Vya Badr

 

Vita Vya Badr

 

Imekusanywa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Badr ni jina la mji ulio kiasi cha kilomita mia na hamsini mbali na mji wa Madiynah, na mahali hapo hapakuwa na chochote isipokuwa bonde tu na kisima kilichokuwa milki ya mtu mmoja aitwae Badr, na kwa ajili hiyo mahala hapo pakaitwa ‘Badr’. Kwa vile vita hivyo vilipiganwa mahali hapo, ndiyo maana vikaitwa vita vya Badr.

 

Vita hivyo vilitokea asubuhi ya siku ya Ijumaa, Ramadhwaan ya kumi na saba mwaka wa pili baada ya Hijrah (baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhamia Madiynah).

 

 

Sababu Za Vita

 

Chanzo cha vita hivi kilikuwa ni msafara wa biashara wa makafiri ukiongozwa na Abu Sufyan uliokuwa ukitoka nchi ya Sham ukirudi Makkah ukiwa na watu wasiozidi arobaini. Msafara huu ulikuwa umebeba mali nyingi sana ya watu wa Makkah, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaona hii ni fursa nzuri ya kuipiga dola hiyo ya kikafiri kiuchumi, kijeshi na kisiasa, na pia kulipiza kisasi. Hasa kwa vile Waislam walipohama Makkah kwenda Madiynah, Makafiri waliwalazimisha kuziacha mali zao zote huko, na kuondoka bila chochote isipokuwa nguo zao na mnyama wa kumpanda. Bali wengine walinyang’anywa hata wanyama wao, na ikawabidi kutembea kwa miguu mpaka Madiynah na wengine waliviziwa njiani na kuuliwa.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Waislam:

 

“Msafara huu wa ma-Quraysh umejaa mali zao, uendeeni, huenda Allaah akatulipa (haki zetu walizotunyang’anya) kwa kutuwezesha kuuteka.”

 

 

Nguvu Za Jeshi La Waislam

 

Si watu wengi waliojitolea kwenda, na hii ni kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutilia mkazo sana kutoka huko. Hakumlazimisha mtu kwenda naye na wala hakumlaumu yeyote yule asiyetoka pamoja naye. Bali alimwacha kila mmoja ajiamulie mwenyewe ikiwa anataka kwenda au hataki. Na kwa ajili hiyo Swahaba wachache tu walimfuata.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka akiwa na watu wapatao mia tatu na kidogo tu hivi. Inasemekana walikuwa mia tatu na kumi na tatu au kumi na nne na riwaya nyengine zinasema kuwa walikuwa mia tatu na kumi na saba. Themanini na sita kati yao ni Muhajiriyn (watu wa Makkah waliohamia Madiynah) na mia mbili thelathini na moja ni watu wa pale pale Madiynah.

 

Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hawakujuwa kuwa msafara huu utakuja geuka kuwa ni moja katika mapambano makubwa baina ya Haki na Baatwil. Walidhania kuwa yatakuwa yale mapambano ya kawaida baina ya makundi ya wapiganaji wa Kiislam na misafara midogo midogo ya makafiri. Hawakujua kuwa Allaah amekwisha panga atimize jambo lililokuwa lazima litendeke.

 

Waliondoka wakiwa na farasi wawili tu, mmoja wa Zubair bin Awaam na mwengine wa Mikidaad bin Al-Aswad Al-Kindy (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Walikuwa pia na ngamia sabiini wakipokezana katika kuwapanda.

 

 

Jeshi La Waislam Linaondoka Kuelekea Badr

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka Madiynah pamoja na Swahaba zake hao (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuufuatia msafara huo wa Abu Sufyan. Akamchaguwa Ibni Ummi Makhtuum (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni mkuu wa Madiynah badala yake, lakini alipofika nje kidogo ya Madiynah, mahali panapoitwa Ar-Rawha, akamrudisha Swahaba mmoja anayeitwa Aba Lubaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na kumtaka yeye awe khalifa wake pale Madiynah badala ya Ibni Ummi Makhtuum (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Katika msafara huo, Nabiya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamchagua Mas-‘ab bin ‘Umair (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni mshika bendera, na bendera yenyewe ilikuwa ya rangi nyeupe.

 

Akaligawa jeshi makundi mawili:

 

1.     Kikosi cha Muhajiriyn (watu wa Makkah) na akampa bendera yao ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

2.     Kikosi cha watu wa Madiynah, na akampa bendera yao Sa’ad bin Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka na jeshi lake hilo akiifuata njia ya Makkah, na alipofika mji uanoitwa Ar-Rawha akapumzika, na baada ya kupumzika mahala hapo akaondoka kuelekea mji wa Badr akiiacha njia ya Makkah kushotoni kwake na kuendelea na safari yake mpaka akalifikia bonde la Rahiyqan na baada ya kuendelea mbele kidogo, akawatuma Swahaba Basis bin ‘Umar na Uday bin Azzaghaabah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) watangulie na kupeleleza habari za msafara waliokusudia kuuteka.

 

 

Msafara Wa Abu Sufyan

 

Ama Abu Sufyan aliyekuwa kiongozi wa msafara wa biashara ya makafiri wa Makkah, alikuwa ni mtu mwenye kuchukua hadhari sana, alijuwa kuwa njia ya Makkah ina hatari nyingi, na kwa ajili hiyo, kila mara alikuwa akitanguliza wapelelezi ili wamletee habari za mbele ya safari, wakati huo huo alikuwa akimuuliza kila anayekutana naye, iwapo huko alikotoka ameona chochote kile kisichokuwa cha kawaida.

 

Katika kuuliza uliza kwake akamuuliza mtu mmoja anayeitwa Majdi bin ‘Amru iwapo ameona jeshi kutoka mji wa Madiynah, akasema:

 

“Mimi sikuona majeshi, lakini niliona kundi kubwa la watu waliopumzisha ngamia wao mahali hapa”.

 

Abu Sufyan akaenda kupafanyia uchunguzi mahali pale alipoambiwa kuwa watu walipumzisha ngamia wao. Baada ya kuchambua kinyesi cha ngamia waliopumzishwa mahali hapo na kuona kokwa za tende ndani yake, akasema:

 

“Madamu choo chao kimejaa kokwa za tende, hapana shaka yoyote kuwa hawa ni ngamia wa watu wa Madiynah”.

 

Alipotambua hayo, akajua kuwa anaviziwa, na hapo hapo akageuza njia yake na kumtuma mtu mmoja aitwae Dhamdham bin ‘Amru Al-Ghafaariy atangulie mbio sana. Aende kuwazindua watu wa Makkah juu ya hatari inayoukabili msafara wao wenye vitu vya thamani kubwa sana.

 

Watu wa Makkah waliposikia hayo, wakasema:

 

“Muhammad anadhania kuwa atauteka msafara huu kwa urahisi kama alivyouteka msafara wa ‘Amru bin Al-Hadhramiy?” (Kisa cha kutekwa kwa msafara wa ‘Amru nimekielezea katika makala ya ‘Miezi Mitukufu’).

 

Makafiri wakaendela kusema:

 

“Haitokuwa hivyo kabisa! Wa-Allaahi atakiona chake Muhammad safari hii”.

 

 

Jeshi La Makafiri Wa Makkah

 

Ma-Quraysh mara baada ya kujuulishwa juu ya hatari hiyo, wakakusanya jeshi la watu wapatao alfu moja na mia tatu, farasi wapatao mia moja na ngamia wengi sana. Wakaondoka hapo wakiongozwa na Abu Jahal bin Hishaam pamoja na vigogo vya ma-Quraysh.

 

Walisafiri kwa kasi kubwa sana kuelekea kaskazini mahali uliopo mji wa Badr. Walipoufikia mji uitwao Al-Juhufa, wakapata salamu kutoka kwa Abu Sufyan kuwa; msafara wake umekwishasalimika na hatari ya kutekwa, na akawataka warudi Makkah.

 

Kwa sababu mara Abu Sufyan alipotambua kuwa anafuatwa, akabadilisha njia na kupita njia ya pwani pwani badala ya kupitia njia ya mji wa Badr. Na kwa ajili hiyo akaokoka na kuwapelekea habari hizo wenzake.

 

Abu Jahal akasema:

 

“Wa-Allaahi haturudi, mpaka tufike Badr, tukae hapo siku tatu, tuchinje wanyama wetu, tunywe pombe yetu na waimbaji waimbe mpaka habari zetu ziwafikie Waarabu wote ili wapate kutujuwa ni nani sisi na ili watuogope”.

 

 

Tatizo La Jeshi La Waislam

 

Waislam walipata habari za kuwaponyoka kwa msafara wa Abu Sufyan na wakati huo huo wakapata habari za jeshi kubwa la watu wa Makkah lililowakabili lililoazimia kwenda mji wa Badr, na kwa ajili hiyo wakaingia katika tatizo kubwa sana.

 

Baadhi yao wakaingiwa na hofu, na wengine wakatoa wazo la kurudi Madiynah, na hii ni kwa sababu walikuwa wachache, hawana silaha za kutosha na hawakutoka kivita. Lakini ikawabidi kulikabili tatizo hilo kwa ushujaa mkubwa kabisa kwani iwapo watakimbia kupambana na jeshi la makafiri na kuliacha litambe hapo Badr, mji ulio katika eneo la karibu na mji wa Madiynah, huko kutawapa nguvu na kichwa kikubwa makafiri na watapata moyo zaidi, jambo ambalo halitakuwa na mwisho mwema. Wakati huo huo haiba ya jeshi la Waislam itaondoka.

 

Mwanachuoni mkubwa Al-Mubaarak Fury anasema katika kitabu chake Ar-Rahiyqul Makhtuum:

 

“Jeshi la Waislam lingekuwa mfano wa mwili bila ya roho, na makafiri wangepata moyo wa kujaribu kuushambulia mji wao wa Madiynah bila ya hofu yoyote ile”.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِن بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ﴿٥﴾يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ﴿٦﴾وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّـهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ﴿٧﴾لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ﴿٨﴾

 

Kama Alivyokutoa Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi miongoni mwa Waumini linachukia. Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika, kama kwamba wanasukumwa katika mauti nao huku wanatazama. Na pindi Allaah Alipokuahidini moja kati ya makundi mawili (la msafara au la jeshi) kwamba ni lenu; nanyi mkatamani kwamba lisilo na silaha liwe lenu, na Allaah Anataka Athibitishe haki kwa maneno Yake, na Akate mizizi ya makafiri. Ili Athibitishe haki na Abatilishe ubatilifu japokuwa wakhalifu wamekirihika. [Al-Anfaal: 5-8]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Anashauriana Na Sahaba Zake (Radhwiya Allaahu ‘Anhum)

 

Kutokana na mabadiliko haya ya ghafla na ya hatari, ilimbidi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aitishe mkutano wa mashauriano na wakuu wa jeshi la Waislam ili kuwajuulisha juu ya hali ya mambo ilivyo na kutaka ushauri wao.

 

Ama wale aliowashauri katika wakubwa wa jeshi lake, kwanza aliinuka Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akatoa hutoba nzuri ya kumuunga mkono Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu kulazimika kwao kupigana na makafiri. Kisha akainuka ‘Umar bin Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kutoa hotuba nzuri vile vile. Kisha akainuka Al-Mikdaad bin ‘Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

“Ee Rasuli wa Allaah, nenda kama atakavyokuonyesha Allaah, na sisi tuko nyuma yako. Wa-Allaahi hatukuambii kama walivyomuambia wana wa Israili Nabiy wao Muwsaa: 

فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ ﴿٢٤﴾

Basi nenda wewe na Rabb wako mkapigane, hakika sisi tunakaa hapa hapa. [Al-Maaidah: 24]

 

Bali tunakwambia: “Nenda wewe na Rabb wako ukapigane na sisi pamoja nanyi tutapigana ” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Vyema” Kisha akamuombea du’ah.

 

Hawa watatu wote walikuwa katika Muhajiriyn (Watu wa Makkah), ambao ni wachache katika jeshi hilo, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapenda kujua rai ya viongozi wa watu wa Madiynah waliokuwa wengi katika jeshi hilo, akasema:  “Nipeni shauri lenu enyi watu”.

 

Akikusudia watu wa Madiynah. Sa’ad bin Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mmoja wa viongozi wa watu wa Madiynah akatambua hayo, akasema: “Wa-Allaahi kama kwamba unatukusudia sisi ee Rasuli wa Allaah?”Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ndiyo” Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

“Sisi tumekuamini na kukusadiki, na tukashuhudia kuwa uliyokuja nayo ndiyo haki, na tukakupa ahadi zetu na neno letu kuwa tutakusikiliza na kukutii, kwa hivyo endelea tu kama unavyotaka kwani Wa-Allaahi kama utatutaka tuivuke bahari hii, ukaivuka, basi tutaivuka pamoja nawe na hapana hata mmoja kati yetu atakayebaki nyuma, sisi hatuogopi kupambana na adui kesho, sisi ni watu wenye kusubiri katika vita na wakweli katika mapambano na In Sha Allaah Allaah atakuonyesha ndani yetu yale yatakayokufurahisha macho yako, kwa hivyo tuongoze kwa baraka za Allaah”.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafurahishwa sana na maneno ya Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu), akasema:

 

“Nendeni na nakupeni bishara njema, Allaah ameniahidi moja wapo ya makundi mawili. Wa-Allaahi kama kwamba ninaona wapi wataanguka kila mmoja kati ya maadui.”

 

 

Majeshi Ya Kiislam Yanafanya Upelelezi

 

Walipowasili mahali panapoitwa Addiya, karibu na Badr, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Sahibu yake wa pangoni Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu), wakatoka na kuanza kufanya uchunguzi nje ya kambi yao, na katika kutembea kwao, wakakutana na mzee mmoja wa Kiarabu na kumuuliza juu ya habari za jeshi la ma-Quraysh na juu ya habari za jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ili asiweze kutambua ni katika kundi gani wao.

 

Yule mtu akawaambia: “Kabla sijakujibuni, nambieni kwanza nyinyi mnatokea wapi?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Ukituambia na sisi tutakuambia…?”

 Yule mtu akasema:

“Nimesikia kuwa jeshi la Muhammad na Sahibu zake lilitoka siku kadhaa wa kadhaa, ikiwa habari hizo ni sahihi, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa.”

Akapataja mahali lilipo jeshi la watu wa Madiynah.

“Na nimesikia kuwa ma-Quraysh wametoka siku kadhaa wa kadhaa, na ikiwa maneno niliyoambiwa ni kweli, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa wa kadhaa.”

Akapataja mahali lilipo jeshi la ma-Quraysh.

Baada ya kumaliza kusema, akawauliza:

“Nyinyi mnatokea wapi?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:

“Sisi tunatokana na maji.”

Kisha akaondoka.

Yule mtu akawa anajiuliza:

“Hawa wanatoka katika maji ya Iraaq au maji gani?”

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema uongo, kwani viumbe vyote vinatokana na maji. Allaah anasema:

وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ

 

Na Tukajaalia kutokana na maji kila kitu kilicho hai. [Al-Anbiyaa: 30]

 

 

Waislam Wanapata Habari Muhimu Kuhusu Jeshi La Ma-Quraysh:

 

Mchana wake siku hiyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma watu watatu kwenda kupeleleza juu ya habari za jeshi la ma-Quraysh, nao ni: ‘Aliy bin Abi Twaalib, Az-Zubayr bin ‘Awaam na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Walipokwenda penye kisima cha Badr wakawakuta watoto watatu wanachota maji kwa ajili ya kuwapelekea jeshi la ma-Quraysh, wakawateka na kwenda nao kambini ili kuwauliza masuali.

 

Walipofika nao kambini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali, kwa hivyo wao wakaanza kuwauliza mateka wao.

 

Vijana hao wakasema kuwa wametumwa na ma-Quraysh ili kuwachotea maji. Swahaba walikasirishwa na jibu hilo, kwani walitamani wawe watu wa msafara wa Abu Sufyan. Wakawapiga sana mpaka wakasema kuwa wao ni watu wa Abu Sufyan na si watu wa jeshi la ma-Quraysh. Baada ya kutamka hayo, wakawaachilia.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kusali akawaambia:

“Waliposema kweli mliwapiga, na walipokudanganyeni mkawachilia. Walisema kweli Wa-Allaahi, kwani wao ni watu wa jeshi la ma-Quraysh”

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawuliza wale vijana:

“Nipeni habari za ma-Quraysh.”

Wakasema:

“Wapo katika ng’ambo ya bonde lile la mbali”.

Akawauliza:

“Wako wangapi?”

Wakasema:

“Wengi”

Akawauliza:

“Idadi yao ngapi?”

Wakasema:

“Hatujuwi”

Akawauliza:

“Wanachinja wanyama wangapi kila siku?”

Wakasema:

“Siku nyingine wanachinja ngamia tisa na siku nyingine kumi”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum):

“Idadi yao ni baina ya watu mia tisa na elfu.”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza tena wale vijana:

“Nani katika vigogo vya ma-Quraysh wamo miongoni mwao?”

Wakasema:

“Utbah na Shaiba watoto wa Rabia, Abu Al-Bakhtari bin Hishaam, Hakiym bin Hizaam, Naufil bin Khuwailid, Al-Haarith, Taimah, An-Nadhar bin Haarith, Zaamah bin Aswad, Abu Jahal bin Hishaam, na Umayyah bin Khalaf”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum): “Makkah imekutupieni (imekuleteeni) vipande vya maini yao [vigogo vyao na vipenzi vyao].”

 

 

Kuteremka Kwa Mvua

 

Waislam wakasogea mbele kidogo mpaka wakakaribia bonde la karibu na mahali yalipopiga kambi majeshi ya ma-Quraysh.

 

Allaah aliwateremshia Waislam utulivu wakalala vizuri, hata wengine wakaota na kuamka wakiwa na janaba. Lakini mahali hapo hapakuwa na maji ya kuogea ili wapate kujitahirisha na wala ya kunywa, na Shaytwaan akaanza kuwatia wasi wasi: “Vipi mtapigana kesho wakati miili yenu haina tohara, vipi mtapigana kesho mkiwa na kiu…?”

 

Allaah akawateremshia mvua iliyowasaidia sana. Kwa sababu kutokana na mvua hiyo waliweza:

 

  • Kujitahirisha,
  • Kuondoa uchafu wa shetani, na
  • Kuzipa nguvu nyoyo zao.

Na maji ya mvua pia yakawasaidia kuufanya mchanga chini yao uwe mgumu ili waweze kutembea vizuri bila ya kuteleza wakati wa mapambano.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ﴿١١﴾

 

Pindi Alipokufunikeni kwa usingizi kuwa ni amani kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, ili Akutwaharisheni kwayo, na Akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan, na ili Atie nguvu nyoyo zenu, na Athibitishe kwayo miguu. [Al-Anfaal: 11]

 

 

Jeshi La Waislam Linatangulia Kukamata Sehemu Muhimu

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaliamrisha jeshi lake liondoke pale walipo haraka sana ili wawahi kusogea mbele karibu na mahali yalipo maji ya mji wa Badr. Wakasogea mpaka wakafika mwanzo wa visima vya maji ya Badr na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaamrisha kupiga kambi hapo.

 

Mmoja katika Swahaba aitwaye Al-Khabaab bin Mundhir (Radhwiya Allaahu ‘anhu), akamuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Ee Rasuli wa Allaah, mahala hapa tuliposimama, Allaah amekuamrisha na hatuna haki ya kusonga mbele zaidi au ni katika hila za kivita tu na rai yako mwenyewe?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Bali ni hila za kivita na rai yangu mwenyewe.”

Akasema:

“Ee Rasuli wa Allaah, mimi naona kuwa hapa si makaazi mazuri, bora tusogee mbele mpaka mwisho wa visima vya maji ya Badr, tuvizunguke kisha tujenge mahodhi, tuyajaze maji, kisha tupambane nao, sisi tutakuwa tunakunywa na wao wasipate kunywa”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Rai uliyotowa ni nzuri.”

 

Wakaondoka hapo na kusogea sehemu ya juu ya mahali yalipo maji, na usiku wakaanza kutengeneza mahodhi na kuyajaza maji.

 

 

Makao Makuu Ya Jeshi

 

Baada ya kumaliza kazi yao hiyo, Sa’ad bin Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akatoa rai pajengwe mahali patakapokuwa makao makuu ya jeshi lao, ili waweze kujitayarisha na kuikabili hali ya hatari yoyote itakayotokea iwapo jeshi lao litashindwa katika vita hivyo.

 

Akasema:

 

“Ee Rasuli wa Allaah, unaonaje tukakujengea kipaa mfano wa hema (‘Ariish), kisha tukakuwekea tayari wanyama wa kupanda, kisha sisi tutapambana na adui, ikiwa Allaah atatujaalia tukawashinda, hayo ndiyo tunayoyapenda. Ama ikiwa kinyume na hivyo, basi wewe utapanda wanyama wako na utakwenda kujiunga na wenzetu tuliowaacha nyuma, kwani hao tuliowaacha nyuma mapenzi yao juu yako ni makubwa pia kama sisi. Wangelijuwa kuwa utapambana na adui, basi wasingerudi nyuma kabisa na wangepigana jihadi pamoja nawe.”

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea kila la khayr kwa rai yake hiyo, na Waislamu wakajenga mfano wa hema juu ya kilima, sehemu ya Kaskazini ya uwanja wa mapambano, sehemu ambayo mtu anaweza kuviona vita bila ya taabu huku vikipiganwa.

 

 

Usiku Kabla Ya Mapambano

 

Usiku kabla ya mapambano, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilipanga vizuri jeshi lake. Kisha akawa anatembea huku akiwaonyesha Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), mahali watakapokufa maadui mbali mbali, kabla hata vita havijaanza. Alikuwa akisema:

 

“Hapa ataanguka fulani, hapa atauliwa fulani …”

 

Alipokuwa akiwapanga watu wake, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipita mbele ya Sawaad bin Aziya (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamgonga kwa nguvu tumboni pake kwa bapa la mkuki na kumwambia:

 

“Simama vizuri ee Sawaad.”

 

Sawaad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:

 

“Umeniumiza ee Rasuli wa Allaah na Rabb wako amekuleta kwa ajili ya kusimamisha haki na uadilifu, kwa hivyo uniache na mimi nikulipizie katika mwili wako”.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalifunua tumbo lake na kumwambia:

“Jilipie kisasi chako.”

Sawaad akalikumbatia tumbo la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku akilibusu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Kipi kilichokupeleka ukafanya hivi?”

Akasema:

“Ee Rasuli wa Allaah, mambo ndiyo kama unavyoyaona na mimi nilipenda tendo langu la mwisho kabla sijafa liwe kuugusa mwili wako”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea du’ah nzuri.

 

Baada ya kuwapanga watu wake sawa na kuwataka wasianze kupigana mpaka atowe amri yake, akawaambia:

 

“Wakianza kuja, anzeni kuwarushia mishale na msitoe panga zenu mpaka wawe karibu nanyi kabisa.”

 

 

Jeshi La Watu Wa Makkah

 

Usiku ule baadhi ya ma-Quraysh walijaribu kutaka kunywa maji penye mahodhi waliyoyajenga Waislam, lakini kila aliyejaribu kuyasogelea aliuliwa, isipokuwa mtu mmoja aitwae, Haakim bin Hizaam, huyu aliachwa na alisilimu baadaye na akawa Mwislam mwema.

 

Ma-Quraysh walimtuma ‘Umair bin Wahaab Al-Jahamiy aende kuchunguza nguvu za jeshi la Waislam. Akawa anazunguka mbali na jeshi hilo akiwa juu ya farasi wake, huku na kule, kisha akarudi kwa wenzake na kuwaambia:

 

“Jeshi lao ni kiasi cha watu mia tatu na zaidi kidogo, lakini naona kesho balaa litakuwa kubwa sana, maana watu hawa hawana pa kukimbilia, na hawana cha kupoteza, wanajuwa kuwa wao watauliwa tu. Hawana isipokuwa panga zao tu, na nyuma yao jangwa tupu, kwa hivyo inaelekea watapigana kwa ushujaa na hawatokubali mmoja wao auliwe bila ya yeye naye kuuwa mtu mmoja kati yenu, kwa hivyo tizameni wenyewe”.

 

Pakatokea mzozo mkubwa baina ya ma-Quraysh, wengi wao wakamtaka Abu Jahal arudi na jeshi lake Makkah, na kwamba hapakuwa na haja ya kupigana na jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Abu Jahal kwa haraka akafanikiwa kuuzima moto huo na kumlaumu ‘Umair kwa kumwambia:

 

“Umeingiwa na hofu wewe ulipouona uso wa Muhammad, pale ulipokuwa ukiyachunguza majeshi yake ndiyo sababu ukaja na uwoga na unataka kututia na sisi uwoga huo.”

 

Akaweza kuwaingiza watu wake mori wa vita, kwa kuwakumbusha kuuliwa kwa ‘Amru bin Al-Hadhramiy na kwamba lazima walipe kisasi chake.

 

 

Majeshi Yanakabiliana

 

Asubuhi ya siku ya Ijumaa, tarehe kumi na saba, mwezi wa Ramadhwan, mwaka wa pili baada ya Hijrah, majeshi hayo mawili yakapambana. Allaah aliwafanya Waislam walione jeshi la makafiri kuwa ni wachache ili wasiwaogope na akawafanya makafiri wawaone Waislamu pia kuwa ni wachache ili wasiwaogope na kurudi nyuma, yote haya ili kitendeke kile anachokitaka Subhaanahu wa Ta’aalaa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا ۗ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ﴿٤٤﴾يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿٤٥﴾

 

Na pindi (Allaah) Alipokuonyesheni machoni mwenu, pale mlipokutana, kuwa wao ni wachache na Akakufanyeni nyinyi kuwa wachache machoni mwao; ili Allaah Akidhie jambo lilokuwa lazima litendwe. Na kwa Allaah Pekee hurejeshwa mambo yote. Enyi walioamini! Mtapokutana na kikosi (cha makafiri), basi simameni imara, na mdhukuruni Allaah kwa wingi ili mpate kufaulu. [Anfaal: 44 - 45]

 

Majeshi yalipoanza kupambana, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia ndani ya lile hema, yeye na Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yao, na hapana mwengine aliyeingia humo isipokuwa wao, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kuomba du’ah huku akisema:

 

“Rabb wangu hawa ma-Quraysh wamekuja kwa jeuri na kiburi chao, wakikupinga na kumkadhibisha Nabiy wako. Rabb wangu nitimizie yale uliyoniahidi, Rabb wangu watu hawa wakishindwa leo, basi hutaabudiwa tena…”

 

Kila vita vikipamba moto, naye huongeza kuomba du’ah.

 

Akawa anaendelea kuomba mpaka nguo yake ya begani ikamwanguka, na As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaiokota na kumvisha tena huku akimwambia:

 

“Inatosha ee Rasuli wa Allaah, ushamuomba vya kutosha Rabb wako.”

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama penye mlango wa ‘Ariish aliyojengewa akawa anaisoma aayah ya 45 ya Suwrah Al-Qamar:

 

سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ ﴿٤٥﴾

Na maana yake ni:

 

Utashindwa mjumuiko wao na watageuka nyuma. [Al-Qamar: 45]

 

 

Mubaraza (Mapigano) Kabla Ya Mapambano

 

Kwa kawaida kabla ya kuanza mapambano,

 

Waarabu walikuwa na tabia ya kuanzisha Mubaraza, na maana yake ni, mtu mmoja au wawili au watatu hutoka kutoka kila upande na kuanza kupambana wao kwanza kila mmoja na mwenzake mpaka wauwane, kisha vita ndiyo vinaanza. Mapigano haya kwa kawaida ndiyo yanayotowa picha ndogo ya mwisho wa vita.

 

Katika mapigano haya, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatoa upande wa Waislam, ‘Aliy bin Abi Twaalib, Ubaidah bin Haarith na Hamzah (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Kwa upande wa makafiri wakatoka, Utbah na ndugu yake Shaibah, na Al-Waliid mtoto wa Utbah – wote wakiwa watu wa aila moja. Katika mapigano hayo, Hamza (Radhwiya Allaahu ‘anhu), alimuuwa mpinzani wake Shaibah, na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), alimuuwa mpinzani wake Al-Waliid bila taabu na bila kuchukuwa muda mferu. Ama Ubaidah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), yeye na mpinzani wake, wote wawili waliumizana wakaanguka chini, lakini ‘Aliy na Hamzah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakawahi kumrukia Al-Waliid na kumuuwa kisha wakamuokoa mwenzao na kumvuta nyuma na kumrudisha katika kambi ya Waislam. Lakini hatimaye kutokana na damu nyingi iliyomwagika alifariki dunia siku nne baada ya tukio la Badr kwa homa ya manjano.

 

 

Mashambulio

 

Mapigano haya yalimaanisha mwisho mbaya wa jeshi la washirikina. Kwa sababu wamepoteza watatu katika wapiganaji wao wakubwa kwa mpigo mmoja, na kwa kawaida Waarabu walikuwa na itikadi ya kuvipima vita kutokana na mapigano ya mwanzo (Mubaraza). Kwa ajili hiyo wakawavamia Wasilam kwa ghadhabu na kwa nguvu zao zote, na Waislam wakapambana nao kwa ujasiri mkubwa kabisa.

 

Wakati huo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawatokea Waislam na kuwaambia:

 

“Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad ipo mikononi pake, yeyote atakayepigana nao leo kisha akauliwa akiwa katika hali ya subra, bila ya kurudi nyuma, basi Allaah atamuingiza Jannah.”

 

‘Umair bin Al-Hamaam (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akila tende, mara baada ya kusikia maneno hayo akasema:

 

“Hivyo baina yangu na baina ya kuingia Jannah ni kupigana na kuuliwa na watu hawa na tende hii ndiyo inanichelewesha?”

 

Akazitupa tende zake, akaingia vitani, akapigana mpaka akauliwa.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasogea mbele, akachota gao la mchanga, akawakabili ma-Quraysh kisha akasema:

 

“Zimeangamia nyuso zao.”

 

Kisha akawarushia nao.

 

Allaah Anasema:

 

فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ قَتَلَهُمْ ۚ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ رَمَىٰ ۚ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١٧﴾ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ﴿١٨﴾

 

Hamkuwaua nyinyi, lakini Allaah Ndiye Aliyewaua. Na wala hukurusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم  mchanga) pale uliporusha lakini Allaah Ndiye Aliyerusha; ili Awajaribu Waumini jaribio zuri kutoka Kwake. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. Ndivyo hivyo! Na hakika Allaah ni Mwenye kudhoofisha mbinu za makafiri. [Al-Anfaal: 17-18]

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum):

 

“Wakazieni vizuri, inukeni muifuatilie Jannah ambayo upana wake tu ni sawa na mbingu na ardhi.”

 

Kisha akaondoka na kurudi penye ‘Ariish yake ile aliyojengewa.

 

Mapambano makali yakaanza baina ya makundi mawili hayo, na ushindi ukawa wa Waislam. Wakauliwa waliouliwa katika vigogo vya ma-Quraysh na wakatekwa waliotekwa.

 

Haya ni mapambano ya pekee ambayo Malaika walishiriki, akiwemo Jibriyl ('Alayhis-salaam). Baadhi ya Swahaba walisema:

 

“Siku hiyo tulikuwa tukiona vichwa vikikatika tu na kuruka huku na kule, hatujuwi nani anayevikata”.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ﴿٩﴾وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ ۚ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿١٠﴾إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ﴿١١﴾إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ﴿١٢﴾ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ وَمَن يُشَاقِقِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿١٣﴾ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ﴿١٤﴾ 

 

Na pindi mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo. Na Allaah Hakujaalia haya isipokuwa ni bishara na ili zitumainike nyoyo zenu kwayo. Na hakuna nusura isipokuwa kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. Pindi Alipokufunikeni kwa usingizi kuwa ni amani kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, ili Akutwaharisheni kwayo, na Akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan, na ili Atie nguvu nyoyo zenu, na Athibitishe kwayo miguu. Pindi Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia): Hakika Mimi Niko pamoja nanyi; basi wathibitisheni wale walioamini. Nitavurumisha kizaazaa katika nyoyo za waliokufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kila kiungo. Hivyo kwa kuwa wao wamempinga Allaah na Rasuli Wake. Na yeyote ampingae Allaah na Rasuli Wake basi hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. Ndivyo hivyo kwenu (jazaa), basi ionjeni, na kwamba makafiri wana adhabu ya moto. [Al-Anfaal: 9-14]

 

 

Kifo Cha Abu Jahal

 

Abu Jahal alipoona majeshi yake yanaanza kurudi nyuma akawa anapiga kelele huku akisema:

“Wasikutisheni hao, msiogope kwa kuwa ‘Utbah na Al-Waliid wameuliwa, leo hatuondoki hapa mpaka turudi nao Makkah tukiwa tumewafunga kamba wote hawa”.

 

Anasema ‘Abdur-Rahmaan bin Auf kuwa nilipokuwa nimesimama vitani nikageuka kutizama kuliani kwangi na kushotoni kwangu nikidhania watakuwepo watu wazima ili tusaidiane vita vikipamba moto. Lakini nikavunjika moyo nilipowaona watoto wadogo wawili wamesimama mmoja kushotoni pangu na mwengine kuliani pangu. Nikasema moyoni mwangu: “Leo sina pa kuegemea”. Yule mtoto aliye kuliani pangu akaniomba niiname apate kuniuliza ili yule mwenzake asisikie. Akaniuliza:

 

“Ami! Yupi kati yao Abu Jahal?”

 

Nikamuuliza:

 

“Ee mwana wa ndugu yangu, unamtakia nini Abu Jahal?”

 

Akanijibu:

 

“Nimesikia kuwa anamtukana Rasuli wa Allaah, Wa-Allaahi nikimuona basi sitomwacha, lazima nitamuuwa”

 

Yule mtoto aliye kushotoni pangu akaniuliza vile vile kama mwenzake, na nikamjibu kama mwenzake na akasema yale yale aliyosema mwenzake.

 

Nilipomuona Abu Jahal nikawaambia:

 

“Yule rafiki yenu mnayemtafuta”

 

Wakamkimbilia na panga zao, wakamvamia na kumpiga kwa mapanga mpaka wakamuuwa.

 

Mara baada ya kumuuwa wakakimbia mpaka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumpa habari njema hizo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

 

“Yupi kati yenu aliyemuuwa?”

Kila mmoja akasema:

“Mimi ndiye niliyemuuwa”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

“Hebu nione panga zenu.”

Baada ya kuzitizama akasema:

“Kweli, nyote mmeshirikiana katika kumuuwa.”

Kisha akasema:

“Allaahu laa ilaaha illa huwa” mara tatu.

Kisha akasema:

“Alhamdu lillaahi lladhiy swadaka wa’adahu, wa naswara ‘abdahu, wa hazama l-ahazaaba wah–dahu”.

 

Katika vita hivi waliuliwa ma-Quraysh sabiini, na wengine sabiini walitekwa, na katika waliouliwa alikuwemo Firauni wa Umma huu – Abu Jahal na ‘Utbah bin Rabia na mwanawe Al-Waliyd na nduguye Shaiba na wengi wengineo.

 

Na miongoni mwa mateka alikuwemo Al-‘Abbaas – Ami yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aqiyl bin Abi Twaalib, na Nawfal bin Al-Haarith, na Umayya bin Khalaf na wengi wengineo.

 

Hawa wote walikuwa upande wa ma-Quraysh.

 

 

Mizoga Ya Makafiri

 

Baada ya vita kumalizika, Waislam wakawazika wenzao waliokufa Mashahid na idadi yao walikuwa kumi na nne. Kisha wakaichukua mizoga ya Mushrikina na kuitupa katika kisima kisichokuwa na maji kilicho karibu na mahali palipotokea mapambano hayo.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Anawafokea Maadui Wake

 

Usiku wa manane Waislam walimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama penye kile kisima walichotupa mizoga ya Mushrikina akiwafokea huku akisema:

 

“Enyi mlio kisimani, ubaya ulioje mliokuwa nao jamaa zangu nyinyi kwa Nabiy wenu! Mlinikadhibisha wakanisadiki watu (kweli), mkanitoa katika mji wangu, wakanipokea watu (kweli), mkanipiga vita wakanisaidia watu (kweli). Je! Sasa nyinyi mmekwisha pata kweli yale aliyokuahidini Rabb wenu? Ama mimi nimepata kweli yale aliyoniahidi Rabb wangu.”

 

Swahaba wakamuuliza:

 

“Ee Nabiy wa Allaah unazungumza na watu washakuwa mizoga?”

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Wao wanasikia kuliko nyinyi haya niliyowaambia isipokuwa hawawezi kujibu.”

 

 

Bishara Njema

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma watu kwa haraka sana waende Madiynah ili kuwapa habari njema hizo za ushindi wao juu ya Makafiri.

 

Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasema:

 

“Zilitufikia habari tulipokuwa tukimzika Bibi Ruqayya (Radhwiya Allaahu ‘anha) binti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mke wa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Zayd bin Harithah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipoingia msikitini, watu walimzunguka huku akisema kwa furaha:

 

“Amekwisha uliwa ‘Utbah bin Rabia na Shaibah bin Rabia na Abu Jahal.” Akawa anawataja mmoja mmoja katika vigogo vya ma-Quraysh waliouliwa Badr.

 

Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasema:

 

“Nikamuuliza, Babangu unasema kweli?”

 

Akanijibu:

 

“Naam, kweli mwanangu”

 

 

Kuondoka Mji Wa Badr

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaondoka hapo Badr pamoja na mateka wao na ngawira zao na alipofika karibu na Madiynah alisimamisha msafara katika bonde la Safra akawagawia Waislam ngawira yao sawa sawa na kila anapoukaribia mji wa Madiynah, alikuta makundi kwa makundi ya watu waliosimama pembezoni mwa njia wakimpongeza.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

إِذْ أَنتُم بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُم بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنكُمْ ۚ وَلَوْ تَوَاعَدتُّمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ ۙ وَلَـٰكِن لِّيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ ۗ وَإِنَّ اللَّـهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿٤٢﴾إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّـهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا ۖ وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَّفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ سَلَّمَ ۗ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٤٣﴾

 

Pindi nyinyi mlipokuwa kando ya bonde la karibu na wao (Makafiri) walipokuwa kando ya bonde la mbali, na msafara (wa mali zao) ulikuwa uko chini yenu. Na lau mngeliahidiana basi mngelikhitalifiana katika miadi hiyo, lakini ili Allaah Akidhie jambo lilokuwa lazima litendwe; ili ahiliki (kwa ukafiri) yule wa kuhiliki kwa hoja bayana na ahuike (kwa iymaan) mwenye kuhuika kwa hoja bayana. Na kwamba Allaah bila shaka ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. Pindi Allaah Alipokuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache. Na lau Angelikuonyesha kuwa wao ni wengi, bila shaka mngelivunjikwa moyo, na bila shaka mngelizozana katika jambo hilo (la kupigana), lakini Allaah Amesalimisha (hayo). Hakika Yeye ni Mjuzi kwa yaliyomo vifuani. [Al-Anfaal: 42–43]

 

 

Matukio Mbali Mbali

 

Baada ya kumalizika vita, Masa-‘ab bin ‘Umair (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuona ndugu yake Abu ‘Aziiz aliyekuwa upande wa makafiri akiwa ametekwa na amefungwa kamba.

 

Akamwambia yule aliyemfunga kamba:

 

“Mfunge vizuri huyo kwa sababu mamake ana mali nyingi, anaweza kumkomboa”

 

Ndugu yake akamwambia:

 

“Huko ndiko kuwapa usia mwema ndugu yangu?”

 

Mas-‘ab akamwambia:

 

“Huyu aliyekukamata ni ndugu yangu kuliko wewe”.

 

Baada ya kutupwa maiti za makafiri kisimani, Abu Hudhaifah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwana wa ‘Utbah bin Rabia alikuwa na huzuni sana. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:

 

“Unaona vibaya juu ya babako, (kwa vile ni kafiri na ametupwa kisimani na wenzake)?”

 

Abu Hudhaifah akasema:

 

“Laa wa-Allaahi, ewe Rasuli wa Allaah, isipokuwa babangu alinifanyia fadhila nyingi sana na alikuwa akinipenda, nikadhani kwa ajili hiyo naye atasilimu, na nilipomuona kuwa amekufa kafiri, ndio nikahuzunika”.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea du’ah kumtakia kila la khayr.

 

Wale watoto wawili waliomuuwa Abu Jahal nao wana kisa chao. Walipokuja kutaka kushiriki katika vita, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkubali ndugu mkubwa na akamkataa yule mdogo.

 

Yule mdogo akasema:

 “Ee Rasuli wa Allaah, kwa nini umemkubali kaka yangu na mimi hukunikubali?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Kwa sababu umri wako ni mdogo.”

Akasema:

“Lakini sisi siku zote tukipigana mieleka, mimi namshinda kaka yangu.”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Hebu piganeni mieleka nikuoneni.”

 

Wakapigana na yule mdogo akamshinda mkubwa wake, kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkubali.

 

‘Umar bin Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuuwa siku hiyo mjomba wake Al’Aas bin Hisham, aliyekuwa upande wa makafiri.

 

 

Hitimisho

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٢٣﴾

 

Kwa yakini Alikunusuruni Allaah katika Badr na hali nyinyi mlikuwa (kikosi) dhaifu. Basi mcheni Allaah mpate kushukuru. [Al-‘Imraan: 123]

 

Allaah, hapa anatujuulisha kuwa Yeye tu ndiye wa kutegemewa, na si viumbe vyake dhaifu. Yeye tu ndiye mwenye kuleta ushindi, na anayestahiki kukimbiliwa wakati wa dhiki, badala ya kuwakimbilia viumbe vyake dhaifu.

 

Na hili ni somo kwa wale ndugu zetu ambao mara wanapokumbwa na tatizo dogo, wanaikimbilia ile du’ah ya Hal-Badiri (Ahlul-Badr) ambayo ndani yake mna majina ya Swahaba walioshiriki katika vita hivyo, na kuomba msaada kutoka kwao.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٢٣﴾

 

Kwa yakini Alikunusuruni Allaah katika Badr na hali nyinyi mlikuwa (kikosi) dhaifu. Basi mcheni Allaah mpate kushukuru. [Aal-‘Imraan: 123]

 

Allaah aliwapa ushindi Waislamu katika vita hivi juu ya uchache wao, wakati katika vita vya Hunain, kwa mara ya mwanzo Waislamu walipigana vita idadi yao ikiwa kubwa zaidi kuliko ya makafiri lakini waliendeshwa mbio na makafiri mpaka Allaah alipowateremshia utulivu wake. Hakupata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka na jeshi kubwa kuliko la siku hiyo, alitoka na watu elfu kumi na mbili, hata Waislamu wakawa wanasema:

 

“Hatutoshindwa leo kwa vile tuko wengi.”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

لَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٍ ۙ وَيَوْمَ حُنَيْنٍ ۙ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُم مُّدْبِرِينَ﴿٢٥﴾

 

Kwa yakini Amekunusuruni Allaah katika maeneo mengi, na Siku ya (vita vya) Hunayn (pia); ulipokupendezeni wingi wenu (kwa kujigamba), lakini haukukufaeni chochote; na ardhi ikawa dhiki juu yenu juu ya upana wake, kisha mkageuka na kurudi nyuma kukimbia. [At-Tawbah: 25]

 

Anasema Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) kuwa:

 

“Katika vita vya Yarmuuk, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwaambia Waislamu:

 

“Mtakapotaka msaada katika vita hivi, basi muandikieni Abu ‘Ubaidah”.

 

Vita vilipoanza, wakamuandikia Abu ‘Ubaidah aje kuwasaidia, na kwamba wako katika hatari. Abu ‘Ubaidah akawaandikia hivi:

 

“Imenifikia barua yenu ikitaka msaada kutoka kwangu, lakini mimi nitakujulisheni yule atakayeweza kukusaidieni mkapata ushindi kuliko nitakavyoweza kukusaidieni mimi; - Allaahu ‘Azza wa Jallah – ombeni msaada kutoka kwake mkitaka kupata ushindi. Kwa sababu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa ushindi na Allaah siku ya Badr akiwa na watu wachache kuliko nyinyi. Itakapokufikieni barua yangu hii, piganeni nao na wala msiniandikie mimi.”

 

Anasema Iyaadh Al-‘Ash-ary (Radhwiya Allaahu ‘anhu), mwenye kuisimulia Hadiyth hii:

 

“Tukapambana nao na tukawashinda, na tukapata ngawira nyingi siku hiyo”.

 

 

 

Share