Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Hatetewi Kwa Dhulma Na Ujinga

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Hatetewi Kwa Dhulma Na Ujinga

 

Imefasiriwa Na: Abuu Suhayl

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Himdi Anastahiki Allaah, Rahmah na amani zimuendee Rasuli wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na aali zake na Swahaba zake na Waislamu wote. Ama baada ya hayo.

 

 

Hakuna Muislamu ambaye anaweza kukubaliana na kutukanwa, kudhalilishwa, kudhauruliwa na kusingiziwa mambo mabaya Rasuli wetu mpendwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imaamu wa Ahlus-Sunnah kama Imam Maalik, Al-Layth, Ahmad, na Ash-Shaafi’iy, wamekubaliana kwa pamoja kwamba yeyote atakayemvunjia heshima, kumtukana au kumdhalilisha au kumtia ila Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa amekufuru, na adhabu inayomstahili kwa yule anayeishi katika dola ya Kiislamu na akafanya hivyo ni kifo, adhabu ambayo itakuwa katika mikono ya mtawala wa Kiislamu.

 

 

Hapana shaka kwamba mashambulizi ya aina hii kwa Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yatasababisha hasira na kukata matumbo ya kila Muislamu kutokana na mapenzi yao kwa Allaah, Rasuli wake na Dini yake. Lakini Muislamu aliye mkweli, muadilifu na muaminifu hawezi kuruhusu kuchukuliwa na hasira na jazba na kujibu mashambulizi haya kwa matendo ya kihuni ambayo yanakusanya matendo ambayo Allaah na Nabiy wake wameyakataza. Zaidi atakuwa kama katika matendo mengine na subra, kisha anayarejesha mambo hayo katika Qur-aan na Sunnah na ufahamu wa Swahaba na ‘Ulamaa walioshikana barabara na elimu. Hivyo Muislamu anakuwa na subira na anaithibitisha miguu yake kwa elimu na anajisalimisha kwa hukumu za Allaah na Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa : 59].

 

 

Al-Haafidhw Ibin Kathiyr ametaja kuwa maana ya

 

وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ

 

 “wenye madaraka katika nyinyi.”

 

kwa mujibu wa Ibn ‘Abbaas, Mujaahid na ‘Atwaa na wengine katika Salaf, inakusudiwa “ ‘Ulamaa”. Na Ibn Kathiyr amesema inakusudiwa ’Ulamaa na watawala na hapa inakusudiwa ’Ulamaa wa Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah.

 

 

Ambacho kimetokea siku chache zilizopita katika ardhi za Waislamu na sehemu nyingine kama hatua za kupinga filamu inayoshambulia Uislamu na kumtukana Rasuli wetu mpendwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanapingana na muongozo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tunatakiwa tukumbuke kuwa mashambulizi haya si mapya. Allaah Ametaja katika Qur-aan kuwa Rusuli Wake (‘Alayhim-salaam) walishambuliwa na kutukanwa, watu wao waliwaita vichaaa, wendawazimu na hata kuwaita wachawi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ ﴿٥٢﴾

Ndio kama hivyo, hawakuwafikia wale wa kabla yao Rasuli yeyote isipokuwa walisema: Mchawi au majnuni. [Adh-Dhaariyaat : 52].

 

 

Na haya yametokea kwa Rusuli kuanzia Nuwh (‘Alayhis-salaam) mpaka kwa Nabiy wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Katika kipindi cha maisha ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuna ambao walikuwa wakimtusi na kumkashfu hadharani. Ka’ab bin Ashraf Al-Yahuwdiy aliyekuwa Madiynah alikuwa akiimba mashairi ya kumkashifu Nabiy na kuimba mashairi mabaya kuhusu wanawake wa Kiislamu. Na Makkah alikuwepo ‘Abdullaah bin Khatal ambaye alikuwa na waimbaji wawili wa kike ambao walikuwa wakiimba mashairi ya kumkejeli Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Aliporudi toka safari ya Makkah kuja Madiynah Ka’ab bin Al-Ashraf akaanza kuimba mashairi ya kumtukana. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwauliza Swahaba zake, ‘Nani atakayemdhibiti Ka’ab bin Al-Ashraf? Kwani amemdhuru Allaah na Rasuli Wake.’ Na hapa ni pale Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika dola yake na yeye alikuwa ndiye kiongozi na Al-Ka’abah alikuwa akiishi chini ya mamlaka yake hapo Madiynah. Lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaambia Swahaba zake kwenda kuwaadhibu majirani zake, rafiki zake au familia yake kwa yale aliyokuwa akifanya Al-Ka’abah bin Al-Ashraf. Wala hakuuadhibu ukoo wake wa Banu Nadhwiyr au kuwaadhibu Mayahudi wengine wa Madiynah.

 

 

Yeyote mwenye akili iliyosalimika hawezi kukubaliana na hili kwani halikubaliani na mantiki achilia mbali maandiko ya Kitabu na Sunnah.

 

 

Alichofanya kama mtawala Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuadhibu Al-Ka’abah ambaye ndiye aliyekuwa anafanya kosa hilo.

 

 

‘Abdullaah bin Khatal alikuwa Makkah na alikuwa na waimbaji wawili wa kike aliowafundisha kuimba nyimbo za kumkejeli na kumkashifu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na wakati huo Nabiy alikuwa ni kiongozi na hakuwahi kamwe kuwashambulia makafiri wa Madiynah au miji au vijijiji vingine kama malipo ya matusi ya ‘Abdullaah bin Khatal kwake yeye. Pia hakuwaamrisha Swahaba zake kuishambulia Makkah au watu wa Makkah kwa sababu ya ‘Abdullaah bin Khatal.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na subira na hakuwakandamiza watu au kuchupa mipaka. Alikuwa na subira na alikuwa muadilifu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoiteka Makkah na jeshi lake, akaamrisha asidhuriwe yeyote ambaye hatopigana nao, isipokuwa kikundi kidogo cha watu ambao aliwataja kwa majina.

 

 

Hapa Nabiy alikuwa na nguvu, ameiteka Makkah na alikuwa na nguvu na miongoni mwa aliowataja ni ‘Abdullaah bin Khatal na waimbaji wake wawili wa kike. Hakuamrisha majirani zake wala familia yake kuadhibiwa. Hakuamrisha mali za ukoo wake kuharibiwa. Alichoamrisha ni kuuawa ‘Abdullaah bin Khatal na waimbaji wake wawili wa kike.

 

 

Hii ni mifano miwili tu ya jinsi Nabiy alivyofanya na watu waliomtukana akiwa hai. Alikuwa ni muadilifu na subira. Hakumkandamiza mtu wala kumdhulumu na hawa watu walimlaani, wakamtukana, wakamdhalilisha na kumkashifu akiwa hai (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Sasa matendo haya ya haya makundi na wajinga wengine walioathiriwa na hayo makundi wameyapata wapi kwa kutazama mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

 

Mmeona wapi kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake walikwenda katika miji mingine na kuandamana, na kuua watu wasiokuwa na hatia, kuharibu mali zao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya Ibn al-Ashraf na Ibn Al-Khatal wakiwa Makkah na Madiynah?

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na subira na uadilifu. Na uadilifu ni kukiweka kila kitu mahali pake. Na haya tunayayona toka kwa watu Misr, Yemen, Libya na nchi zingine katika mashariki ya kati ni ukandamizaji, dhulma na kuvunja Sunnah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 ۚ فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr : 63].

 

 

Kinachofafanua zaidi tofauti katika muongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wale Waislamu ambao wanachukuliwa na jazba na upotevu ni Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambayo imesimuliwa na [Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad] na wengineo, walipokuja kundi la Mayahudi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia “As-Saamu ‘Alaykum” (kifo kiwe juu yako). ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) alielewa walichosema hivyo akawajibu “Wa ‘alaykum As-Saam wa la‘ana.” (Na kifo na laana ziwe juu yenu). Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Taratibu ee ‘Aaishah, bila shaka Allaah Anapenda upole katika mambo yote.” ‘Aaishah akasema “Ee Rasuli wa Allaah! Hukuwasikia waliyoyasema?” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Nimeshawajibu (kwa kusema) “Wa ‘Alaykum.”Na juu yenu pia.” Na Dini yetu haiendi kwa hisia na jazba. Muislamu ambaye anampenda kiukweli Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atafuata muongozo na Sunnah zake.

 

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-‘Imraan : 31].

 

 

Tuzizingatie Nukta Zifuatazo:

 

 

-Maandamano haya ambayo yameenea katika ardhi za Waislamu na yameeingia mpaka Kuwait ni bida’a kama walivyosema wanachuoni wa Ahlus Sunnah Waljama’a kama Shaykh Ibn Baaz, Shaykh Al-Albaani, Shaykh Ibn ‘Uthaymini na walivyoyafafanua. Ni matendo ya kuwapinga na kupambana na viongozi wa Kiislamu na ni katika njia za Makhawaariji. Makundi ya kisiasa wanayaruhusu na kuyatetea kwani ni njia ya kupambana na watawala wa Kiislamu na ndio njia ya kuchukua madaraka.

 

Tumeona jinsi vijana waliojawa na hamasa walivyochukua hatua kuingia mitaani katika maandamano haya na kupambana na polisi na kusababisha uharibifu kwa mali na si mali za balozi - ambacho pia kitendo hichi ni ukandamizaji lakini mali za Waislamu pia!! Na hii ndio inaitwa kumlinda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Haiwezekani kwa Muislamu kumtetea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukandamizaji wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuamrisha kuwa waadilifu:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّـهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾

Enyi walioamini!  Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Maaidah : 8].

 

Al-Haafidhw Ibn Kathir amesema: “Usiache chuki zako kwa watu zikufanye ukaacha kuwafanyia uadilifu. Fanya uadilifu kwa kila mtu akiwa ni rafiki au adui.”

 

Shaykh Wa Uislamu Ibn Taymiyyah Amesema:

 

“Kwani watu hawakutofautiana kuhusiana na ukweli kwamba mwisho wa dhulma ni mbaya na una madhara na mwisho wa uadilifu ni mzuri wenye kupendeza.” Kwa ajili hiyo pamesemwa: Allaah atalisaidia taifa ambalo linafanya uadilifu hata kama watakuwa ni makafiri na hatolisaidia taifa litakalokuwa linafanya dhulma hata kama taifa hilo litakuwa limeamini.” [Majmu’u Al-Fataawaa 28/63].

 

Jua kwamba kuwaadhibu watu wengine kwa makosa ya mtu mwingine sio uadilifu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

قُلْ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِي رَبًّا وَهُوَ رَبُّ كُلِّ شَيْءٍ ۚ وَلَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ إِلَّا عَلَيْهَا ۚ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُم مَّرْجِعُكُمْ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿١٦٤﴾

Sema Je, nitake ghairi ya Allaah kuwa ni Rabb na hali Yeye ni Rabb wa kila kitu? Na wala nafsi yoyote haitochuma (khayr au shari) ila ni juu yake. Na wala habebi mbebaji, mzigo (wa dhambi) wa mwengine. Kisha kwa Rabb wenu ndio marejeo enu, Atakujulisheni kwa yale mliyokuwa mkikhitilafiana nayo. [Al-‘An’aam : 164].

 

 

Makundi ya kisiasa wanatumia maandamano haya na matukio kama haya kama jukwaa na mimbari za kuenezea mashaka na hila zao kwa watu ili watu wawageuke watawala.

 

 

- Maandamano haya ambayo ’Ulamaa wamesema ni bid’ah yametumika kama ngao kujificha kwa wale walio katika Manhaj ya Khawaarij kuua wasio na hatia. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Yeyote katika Waislamu atakayeua mtu ambaye anaishi kwa mkataba au makubaliano (na Waislamu) hatoonja harufu ya Jannah japokuwa harufu ya Jannah inasikika umbali wa mwendo wa miaka 40.” [Al-Bukhaariy].

 

Na katika Hadiyth nyingine amesema:

 

“Mkataba wa amani kwa Waislamu ni mmoja, yeyote atakayeuvunja mkataba wa amani na usalama kwa Muislamu mwengine ni juu yake laana ya Allaah, Malaika na watu wote.”

 

Al-Haafidhw Ibn Hajr (Rahimahu Allaah) amefafanua:

 

 

“Maneno mkataba wa amani kwa Waislamu ni mmoja’ ina maana kuwa kumpa mtu uhakika wa usalama wa amani ni sahihi (unakuwa mkataba umefungika). Kama mmoja wao atampa mkataba wa amani kafiri ni haramu kwa yeyote yule kuuvunja.”

 

 

Makafiri wanaoishi na kufanya kazi katika nchi za Waislamu wamepewa mkataba wa amani kwa hiyo kuwashambulia ni kupambana na kuwapinga watawala wa Kiislamu na kitendo cha usaliti na dhulma.

 

 

Shaykh Twaariq As-Subay’i amesema kwamba kama Muislamu atampa amani asiyekuwa Muislamu, hata kama huyo Muislamu atakuwa ni mwanamme au mwanamke, muungwana au mtumwa, na hata akiwa amepewa amani kwa ishara tu au kama amepewa amani kwa makubaliano ya kibalozi au kwa kumpa viza kuingia katika nchi -mtu huyo atakuwa amepewa mkataba wa amani na usalama wa maisha yake. Ni haramu kwa Waislamu kumdhuru. Na Muislamu atakayemdhuru ataangukia katika laana za Allaah, na Malaika na watu wote.

 

 

- Ukitazama wanaoongoza maandamano haya utawakuta wote ni katika viongozi wa vyama vya kisiasa. Na ushahidi kuwa hakuna katika Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah ambaye amejihusisha na haya maandamano yatosha kuwa dalili kwa mtu mwenye akili, kama ambavyo Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alivyotumia hoja kama hii dhidi ya Makhawaarij kwamba hakuna hata Swahaba mmoja aliye pamoja nao aliposema:

 

“Bila shaka nimekuja kwenu kutoka katika Swahaba wa Rasuli wa Allaah na hakuna hata Swahaba mmoja aliye pamoja nanyi.”

 

Tunaona Waislamu wakiandamana, wakipambana na polisi wakiharibu mali na mambo mengine mabaya zaidi ya yote hayo yanafanyika kwa jina la kumtetea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na filamu iliyotengenezwa na mtu mmoja anayeishi Marekani. La kusataajabisha hakuna hata mmoja anayechukizwa na Misikiti yenye makaburi ndani ambapo asiyekuwa Allaah anaabudiwa kama Msikiti wa Badawi, Zaynab na Al-Husayn?! Dhambi kubwa kabisa mtu anayoweza kuifanya inafanyika katika ardhi za Waislamu na watu wanashambulia mali na haki za watu kwa kitu ambacho hawana mamlaka nacho au uwezo wa kufanya chochote kukizuia!

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa : 48].

 

 

Kwa hiyo Waislamu hawa na makundi haya wanataka kumtetea Nabiy kwa kufanya dhulma na na uonevu - lakini uko wapi utetezi wa Allaah na Tawhiyd yake kutokana na shirk zinazofanywa na Waislamu katik ardhi ya Waislamu wenyewe!

 

 

Jua kwamba Allaah Ametuamrisha kuwa na subira na uvumilivu na Ametukataza kufanya dhulma na uonevu. Na hakuna uadilifu katika matendo tunayoyaona toka kwa kaka zetu na dada zetu wa Misr, Yemen, Tunisia, Morocco, Sudan na nchi nyingine ambapo haya yanatokea. Matendo haya ni matendo ya ujinga, dhulma, upotevu na kuiacha Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Aliyetengeneza filamu hii chafu anaishi Marekani na Marekani ni nchi ambayo ina kanuni zake inazotumia kutawala raia wake. Jambo hili halipo katika mikono ya sisi watu wa kawaida na hatuna uwezo wa kufanya lolote kulihusu. Jambo muhimu kwetu na subira na kushikamana na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni njia bora zaidi ya kumtetea Nabiy zaidi ya haya tunayoyaona yakifanywa na makundi haya na wafuasi wao.

 

 

Na ni muhimu kuzingatia kuwa subira yetu na uvumilivu wetu na kushikamana kwetu na Sunnah wakati wa hali kama hizi wakati hatuna uwezo wa kuzikabili si alama ya udhalili au unyonge. Makundi yaliyopotea ndiyo yamewaingiza vijana katika fikra hizi kuwa ukikosa uwezo wa kuchukua hatua ni sawa na kutochukua hatua, huu ni usaliti na upotevu.

 

 

Ibn Mas’uwd amesimulia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali katika Ka’abah na alipokuwa akisujudu mmoja kati ya wafuasi wa Abu Jahl alimuwekea matumbo ya ngamia mgongoni kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati Ibn Mas’uwd akiwa anamtazama. Ibn Mas’uwd amesema: “Nilikuwa natazama lakini sikuwa na cha kufanya. Laiti ningekuwa na nguvu na uwezo (wa kumzuia).” [Al-Bukhaariy].

 

 

Hili linatuonyesha kwamba wakati hatuna uwezo kutokana na kuwa na miili dhaifu, au kukosa uwezo au kuna kitu kinakuzuia hakuna aibu kwa hilo, kama ambavyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoshindwa kuwasaidia Yaasir, ‘Ammaar na mama yake ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhum) alipowaona wakiteswa kwa sababu ya kumuamini Allaah. Hivyo akawaambia: “Fanyeni subra enyi watu wa nyumba ya Yaasir, kwani mmeahidiwa Jannah.” [Al-Mastadrak Al-Haakim (3/383), Al-Hilyah (1/140), na vingine. Tazama vilevile Swahiyh Siyrat An-Nabawiyyah cha Shaykh Al-Albaanee (uk. 154-155)].

 

 

Haya tumayoyaandika hapa si kwa ajili ya kuitetea filamu hiyo. Hiyo filamu nasi tunaiona kuwa ni matusi yenye kuudhi kama watu wengine. Lakini tunafanya hivi kama njia ya kumtetea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini yetu dhidi ya wale wenye kuchupa mipaka, na wale wanaocheza na hisia za Waislamu na vijana na kuwaita katika njia za upotevu. Huu ni wito wa kuwa na subra na kuwa na uadilifu na kushikama na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haya ndiyo yaliyokuwa yanahitajika kuelezewa na kufafanuliwa. Allaah ni mjuzi zaidi.

 

 

Rahmah na amani zimuendee Rasuli wetu Muhammad na aali zake na Swahaba zake wote. Na shukrani njema zinamstahili Allaah.

 

 

Share