Tukio la Israa Na Mi'iraaj

 

Tukio la Israa Na Mi'iraaj

 

Imekusanywa na Ummu ‘Abdillaah

 

Kutoka katika Vitabu "Zaad Al-Ma’ad" na "Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm"

 

Bismillahi Rahmani Rahim

 

 

Kutokana na umuhimu wa tukio hili ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Kalielezea katika Kitabu Chake Kitukufu pale Aliposema:

 

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake; ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu. Hakika Yeye (Allaah) ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Al-Israa : 1]

 

Ni Mu’ujizah mkubwa kabisa wa Nabii yetu kipenzi (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya Mu’ujizah wa Qur-aan Tukufu, kuna haja ya kukieleza tena japo kimekwishaelezwa na kuandikwa na wengi.

 

Tukio hili adhimu, limeelezwa na wanahistoria kwa kauli mbalimbali wakati hasa lilipotokea:

 

1. Inasemekana Israa ilikuwa katika ule mwaka ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimkirimu ndani yake Utume, Ameichagua kauli hii Atw-Twabariy.

 

2.    Inasemekana Israa ilikuwa baada ya kupewa Utume kwa miaka mitano, Kauli hii imepewa nguvu na Al-Nawawiy na Al-Qurtwubiy.

 

3.    Inasemekana Israa ilikuwa usiku wa ishirini na saba katika mwezi wa Rajab, Mwaka wa kumi wa Utume, Kauli hii imepewa nguvu na mwanachuoni mkubwa Al-Mansuur Forty.

 

4.    Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa miezi kumi na sita yaani katika mwezi wa Ramadhwaan mnamo mwaka wa kumi na mbili wa Utume.

 

5.   Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja na miezi miwili yaani Muharram mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.

 

6.    Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijrah kwa mwaka mmoja yaani Rabiy’uth Thaaniy mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.

 

Kauli tatu za mwanzo zimepingwa kwa sababu Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alifariki mwezi wa Ramadhwaan mwaka wa kumi wa Utume na kifo chake kilitokea kabla ya kufaradhishwa kwa Swalaah tano na hakuna tofauti kuwa Swalaah tano zilifaridhishwa katika usiku wa Israa.

 

Ama kuhusu kauli tatu zilizobaki hakikupatikana kile ambacho kingetumika kutia nguvu moja katika kauli hizo isipokuwa mtiririko wa Suwrah Al-Israa, Ambao unafahamisha kuwa Israa ilichelewa sana. Wanachuoni wa Hadiyth wamepokea ufafanuzi wa tukio hili na hapa chini tunauleta kwa ufupi katika maneno yafuatayo:

  

Ibn Al-Qayyim amesema; “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kauli sahihi, alipelekwa kimwili akiwa amempanda Buraaq, akifuatana na Jibriyl (‘Alayhis-salaam) kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Baytul Al-Maqdis, akamfunga Buraaq katika kikuku cha mlango wa Msikiti, Na kisha kuswali pamoja na Rusuli, Yeye akiwa Imaam. Baada ya hapo, usiku huo huo kutoka Baytul Al-Maqdis akapandishwa katika uwingu wa Dunia akifuatana na Jibriyl (‘Alayhis-salaam) aliyekuwa akibisha hodi kwa ajili yake, akafunguliwa na huko akamuona Aadam (‘Alayhis-salaam) baba wa watu wote, akamsalimia, akamkaribisha na akamjibu salaam yake na akaukubali Utume wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamuonyesha roho za watu wema zikiwa upande wake wa kuume na roho za watu waovu zikiwa upande wake wa kushoto. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa pili, Jibriyl (‘Alayhis-salaam) akaomba kuingia, akafunguliwa na hapo akamuona Yahya bin Zakariya na ‘Iysa bin Maryam (‘Alayhimaa-salaam), akakutana nao, akawasalimia, na wao wakamjibu salaam yake, Wakamkaribisha na kisha wakaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa mpaka uwingu wa tatu, hapo akamuona Yuwsuf (‘Alayhis-salaam), akamsalimia, naye akamjibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa nne ambako alimkuta Idriys (‘Alayhis-salaam), akamsalimia, naye akamjibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa uwingu wa tano, Na hapo akamuona Haaruun bin ‘Imraan (‘Alayhis-salaam), akamsalimia, naye akajibu salaam yake na kumkaribisha na kuukubali Utume wake.

 

Baada ya hapo akapandishwa katika uwingu wa sita na akamkuta hapo Muwsaa bin ‘Imraan (‘Alayhis-salaam), akamsalimia, naye akajibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Alipompita, Muwsaa (‘Alayhis-salaam) alilia na alipoulizwa ni jambo gani linalimliza? Akajibu, “Ninalia kwa sababu kijana amepewa Utume baada yangu, Na katika Ummah wake wataingia peponi kuliko watakaoingia peponi kutoka katika Ummah wangu.” Kisha akapandishwa kwenye uwingu wa saba, ambako alikutana na Ibraahiym (‘Alayhis-salaam), akamsalimia naye akajibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo ndipo akanyanyuliwa Swidratul-Muntahaa, Kisha akanyanyuliwa Baytul Ma’amuur, naye akapandishwa kupelekwa kwa Allaah Mwingi wa Utukufu, Akasogea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka umbali wa kiasi cha masafa ya Qawsayn (pinde mbili) au karibu zaidi kuliko hivyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akayafunua kwa Mja Wake yale Aliyoyafunua, Na Akamfaradhishia Swalaah Khamsini. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akazipokea na kuanza kurejea mpaka alipofika mahali alipo Muwsaa (‘Alayhis-salaam) ambaye alimuuliza; “Umepewa amri ya jambo gani? Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamueleza, “Ameniamrisha Swalaah Khamsini”, Muwsaa (‘Alayhis-salaam) akamwambia, “Kwa hakika Ummah wako hawataweza kutekeleza jambo hilo, Rejea kwa Rabb wako na umuombe Akupunguzie iwe takhfifu kwa Ummah wako”. Akageuza uso na kumuangalia Jibriyl (‘Alayhis-salaam) kwa jicho la kumtaka ushauri katika jambo hilo, naye akampa ishara ndio kama ukitaka. Akapanda naye Jibriyl (‘Alayhis-salaam) mpaka akafika kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na hali ya kuwa Yeye Yu Mahali Pake; [hili ni la Al-Bukhaariy]. Katika mapokezi mengine, Akampunguzia Swalaah kumi kisha akateremshwa mpaka mahali alipokuwa Muwsaa (‘Alayhis-salaam) na akamueleza idadi ya Swalaah zilizopunguzwa. Muwsaa ('Alayhis-salaam) akamwambia, “Rejea kwa Rabb wako na umuombe Akupunguzie tena. “Inasemekana kuwa hakuacha kwenda na kurudi kwa Muwsaa (‘Alayhis-salaam) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mpaka Swalaah zikabaki tano. Muwsaa (‘Alayhis-salaam) akamtaka arejee kwa Allaah tena na kuomba kupunguziwa, Hapo Nabiy akajibu; “Kwa hakika ninamuonea hayaa Rabb wangu na sasa mimi ninaridhia na ninakubali Swalaah nilizopewa.” Alipokwenda umbali kidogo, Alilingania mlinganiaji; “Nimezipitisha faradhi Zangu na nimewapunguzia waja Wangu.”  

 

Ibnul Qayyim amejadili kuhusu suala hili la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuona Rabb wake, Allaah Aliyetukuka mwenye Utukufu na kisha akayataja maneno ya Ibn Taymiyyah kuhusu suala hili. Matokeo ya utafiti ni kuwa, “Kumuona Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa macho duniani ni jambo ambalo halikuthibiti kabisa. Hiyo ni kauli ambayo haikusemwa na yeyote katika Swahaba. Na kile tunachokisema kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) moja kwa moja (katika safari ya Mi'raaj). Ni kuwa alimuona kwa moyo si kwa macho, Kauli ya kwanza haipingani na ya pili.” Kisha akasema: “Ama kuhusu kauli yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Suwrah An-Najm (53: 8).

 

 ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ ﴿٨﴾

Kisha akakurubia na akashuka. [An-Najm : 8]

 

Huko siko kule kukaribia ambako kumetajwa katika kisa cha Al-Israa, Kwani kukaribia ambako kumo katika Suwrah An-Najm, “Ni kukaribia kwa Jibriyl (‘Alayhis-salaam) na kusogea zaidi kama alivyosema Mama wa Waumini ‘Aaishah(Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Mtiririko wa maneno unafahamisha juu ya maana haya; “Amekukaribia na kusogea sana.” Katika Hadiyth ya Al-Israa, Kuna maana kuwa kukaribia huko ni kukaribia kwa Rabb Mtukufu Aliyetukuka na kuwa karibu kwake zaidi. Hakuna kupingana katika Suwrah An-Najm. Lakini kutajwa huko ndani yake ni kuwa yeye alimuona mara nyingine mbele ya Swidratul-Muntahaa, Na huyo ni Jibriyl (‘Alayhis-salaam).

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Jibriyl (‘Alayhis-salaam) katika sura yake halisi mara mbili; ya kwanza hapa duniani na mara nyingine katika Sidratul-Muntahaa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Mjuzi zaidi.

 

Lilitokea lile tukio la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupasuliwa tena kifua chake kwa mara ya pili. Kwa ujumla katika safari hii aliona mambo mengi; miongoni mwa hayo ni kule kuletewa maziwa na pombe na kuchagua maziwa badala ya pombe, Na pakasemwa, “Umeongozwa katika fitrah na umechagua na kupata fitrah, Ama kwa hakika laiti ungechukua pombe Ummah wako wote ungepotea, “Katika safari hiyo alionyeshwa mito minne huko Jannah, Mito miwili iko nje na mito miwili iko ndani. Mito miwili iliyo nje ni mito ya Nail (Nile) na Furaat (Euphrates), Na maana ya mambo hayo ni kuwa ujumbe wake utafanya makazi yake katika majanga yenye rutuba katika Nail na Furaat na  watu wake ndio watakaokuwa wasimamizi wa da’awah ya Kiislaam, Kizazi baada ya kizazi, na si kuwa maji ya mito miwili hiyo yanachimbuka kutoka Jannah.

  

Alionyeshwa Malaika muangalizi wa moto wa Jahannam ambaye hacheki, mwenye uso usio na furaha wala bashasha. Alionyeshwa Jannah na moto. Alionyeshwa walaji wa mali za yatima kwa dhulma, Waliokuwa na midomo kama ya ngamia, Wanatupiwa midomoni mwao vipande vya moto kama mawe na kisha kutolewa katika tupu zao za nyuma.

 

Alionyeshwa walaji wa ribaa waliokuwa na matumbo makubwa yaliyowafanya wasiweze hata kuondoka mahala walipokuwepo. Alipita na kuwaona watu wa Fir’awn wakionyeshwa moto na hali wakipita wakiukanyaga.

 

Alionyeshwa wazinifu, mbele yao kulikuwa na nyama iliyonona vizuri na pembeni mwao kulikuwa na nyama duni iliyooza yenye uvundo. Wakawa wanakula ile nyama duni iliyooza yenye uvundo, na wanaiacha ile nzuri iliyonona. Alionyeshwa wanawake wanaonasibisha waume zao watoto ambao si wao (watoto wa zinaa) hawa walikuwa wametundikwa kwa matiti yao. Na aliona msafara wa kibiashara wa watu wa Makkah wakati wa kwenda na wakati wa kurudi kwake, Na aliwafahamisha watu hao juu ya ngamia aliyewatoroka na alikunywa maji yao yaliyokuwa yamefunikwa na hali ya kuwa wao wamelala na kisha akakiacha chombo kikiwa kimefunikwa na jambo hilo ndilo likaja kuwa dalili (hoja) ukweli wa madai yake asubuhi ya usiku wa Israa.

  

Ibnul Qayyim alisema. “Kulipopambazuka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa kwa jamaa zake aliwaeleza yote Aliyoonyeshwa na Allaah Mtukufu Mwenye Kushinda, Miongoni mwa miujiza Yake mikubwa. Maquraysh walipinga na hawakutaka kabisa kuamini khabari hizo. Katika kutafuta ukweli wa maelezo yake walimtaka awaeleze ulivyo Msikiti wa Baytul Al-Maqdis. Kwa uwezo wake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)Akamdhihirishia hiyo Baytul Al-Maqdis machoni mwake, akawa anawaelezea alama zake moja baada ya nyingine na wakashindwa kukanusha kwa vile alikuwa akiwaambia ukweli. Mwisho akawaeleza kuhusu ule msafara wa wafanyabiashara aliokutana nao wakati wa kwenda na kurudi; akawaeleza ni lini msafara huo unategemea kufika; akawaeleza kuhusu ngamia aliyeuongoza msafara huo, Na mambo yakatokea kama alivyowaeleza. Hata baada ya kujulishwa yote hayo Ma-Quraysh walizidi kukanusha na kukufuru. Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ameitwa “Swiddiyq” ‘Msadikishaji’ kwa sababu ya kulisadikisha tukio hili.

 

Yapo maelezo mafupi na marefu yaliyokuja katika kueleza sababu ya safari hii. Ipo pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Mwenyewe inatosha kabisa kueleza sababu ya safari hii, Pale Aliposema:

 

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

Ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu.  [Al-Israa : 1]

 

Na huu ni utaratibu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Rusuli, Pahala pengine ndani ya Qur-aan Anasema:

وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ ﴿٧٥﴾

Na hivyo ndivyo Tulivyomwonyesha Ibraahiym ufalme wa mbingu na ardhi na ili awe miongoni mwa wenye yakini. [Al-An’aam : 75]

 

Na Alisema kumwambia Muwsaa (‘Alayhis-salaam):

 لِنُرِيَكَ مِنْ آيَاتِنَا الْكُبْرَى ﴿٢٣﴾

Ili Tukuonyeshe baadhi ya Aayaat (ishara, dalili) Zetu kubwa kabisa. [Twaahaa : 23]

 

Na ameweka wazi makusudi ya huko kuoneshwa, “Ili awe ni miongoni mwa wenye yaqini.” Kwa hivyo ni wazi basi kuwa elimu ya Rusuli katika kumjua Rabb wao inatokana na kuiona kwa macho miujiza Yake na kwa njia hiyo kuwa na yaqini na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kiasi kisichokuwa na mfano. Ni ukweli ulio wazi kuwa jambo la kujionea si sawa na la kusikia, Na hii ndio sababu Rusuli (‘Alayhim-salaam) walivumilia mengi katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mambo ambayo si rahisi kuvumiliwa na watu wa kawaida. Nguvu zote za kidunia mbele ya Rusuli ni kama ubawa wa mbu hawatishiki nazo hata chembe, Hata wanapofanyiwa vitimbi na wakati mwingine kuteswa.

 

Bila shaka msomaji ataona kuwa katika Suwrah Al-Israa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekitaja kisa cha Al-Israa katika Aayah moja tu, Kisha Akaingia katika kutaja fedheha za Mayahudi na maovu yao, Na kisha Akawazindua kwa kuwaeleza kuwa hii Qur-aan inaongoza kwenye mambo yanayohitaji misimamo madhubuti kabisa. Inawezekana msomaji akadhania hizi Aayah mbili hazina uhusiano wowote, Jambo hili si kweli, maana kwa maneno haya Allaah Mtukufu Anaashiria kuwa kwa hakika Israa ni tukio lilitokea Baytul Al-Maqdis na kuwa Mayahudi watanyang'anywa cheo cha kuwaongoza wanaadamu kutokana na matendo yao maovu ambayo wameyafanya. Matendo ambayo hayakubakisha nafasi ya wao kubakia katika cheo hicho na kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atakihamisha cheo hicho kwa vitendo na kumkabidhi Rasuli Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye atamkusanyia vituo viwili vikuu vya Da’awah ya Ibraahiym (‘Alayhis-salaam).

 

Wakati umefika wa kuhamishwa kwa uongozi wa kiroho kutoka Ummah ulioijaza historia yake kwa udanganyifu, Khiyana, Madhambi na uadui kwenda katika ummah mwingine utakaoaminika kwa wema na kheri. Rasuli wa Ummah huo hakuacha kuwa anayesifika na wahyi wa Qur-aan inayoongoza kwenye msimamo ulio sahihi.

 

Kwa vipi utahama uongozi huu hali ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anazunguka katika majabali ya Makkah hali ya kuwa ni mwenye kufukuzwa na kupigwa na watu wa kabila lake? Suala hili linaibua ukweli mwingine ambao ni kuwa mzunguko wa kwanza katika Da’awah hii ya Kiislaam umekaribia kufika mwisho na kukamilika, Na baada ya hapo utaanza mzunguko wa kwanza katika mapito yake. Kwa sababu hiyo ndio maana tunaona kuwa baadhi Aayah zinakusanya mambo yanayohusu makhofisho ya wazi na makemeo ya kutisha dhidi ya Mushirikina.

 

 وَإِذَا أَرَدْنَا أَن نُّهْلِكَ قَرْيَةً أَمَرْنَا مُتْرَفِيهَا فَفَسَقُوا فِيهَا فَحَقَّ عَلَيْهَا الْقَوْلُ فَدَمَّرْنَاهَا تَدْمِيرًا ﴿١٦﴾وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِنَ الْقُرُونِ مِن بَعْدِ نُوحٍ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿١٧﴾

Na Tunapotaka kuangamiza mji, Tunawaamrisha wastareheshwa wake wa anasa za dunia, lakini hufanya ufasiki humo; basi hapo ikastahiki juu yake kauli (ya adhabu); kisha hapo Tunaudamirisha kwa mateketezo makubwa. Na karne ngapi Tumeziangamiza baada ya Nuwh. Na Rabb wako Anatosheleza kabisa kuwa ni Mwenye upeo wa khabari na Mwenye kuona dhambi za waja Wake.  [Al-Israa : 16-17].

 

Pamoja na Aayah hizi zipo nyingine zilizowaweka wazi Waislaamu na zinazoendelea kuwawekea misingi ya maendeleo na kanuni zake na vyanzo vyake ambavyo hujenga jamii ya Kiislaam. Kama vile tayari wamekwishafika kwenye ardhi iliyo tayari, waliyapanga vizuri mambo yao kwa pande zote na wakaunda umoja wenye mshikamano madhubuti.

 

Katika jamii yao, hali kadhalika kulikuwepo na Ishara ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atapata makimbilio na mahali pa amani ambako yatatulizana mambo yake na makimbilio hayo ndiyo yangekuwa kituo cha wito wake katika pande zote za dunia. Hii ni moja ya siri miongoni mwa siri za safari hii yenye kubarikiwa.

 

Tukio hili, ambalo kwa Muislamu mwenye Iymaan barabara, hata kama lisingelikuwepo, Iymaan yake bado ingekuwa imara vilevile, ni tukio la kihistoria lenye kuzidisha kuujua uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Utukufu Wake mkubwa usio na mithali. Ni tukio lenye mafunzo mengi ya kiimani na kiitikadi; ndani yake tumeona kumepatikana faradhi ya Swalaah, kumejulikana adhabu mbalimbali za matendo maovu ya hapa ulimwenguni, na hilo litaweza kutusaidia sana sisi kujiepusha na maovu hayo ili tusiishie kutumbukia ndani ya adhabu hizo kali.

 

Tumeona utukufu na uzito wa Swahaba kama Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na imetuzidishia heshima kubwa juu ya watukufu hao na kujua nafasi yao kubwa katika moyo wa mbora wa viumbe, kipenzi wa macho yetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tuchukue mazingatio yanayopatikana humo na kuyafanyia kazi katika maisha yetu na si tukio hili liwe la kuhadithiwa tu na watu kukusanyana kukisherehekea inapofika mwezi wa Rajab ambao kama tulivyoona mwanzoni kuna utata wa tukio hilo kuwa katika mwezi huo.

 

Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi

 

Share