Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi'raaj Na Mafunzo Yake

 

 

Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi'raaj Na Mafunzo Yake

 

Imekusanywa Na: Alhidaaya.com

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

 Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake; ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu. Hakika Yeye (Allaah) ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Al-Israa 17: 1]

 

 

Utangulizi:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaelezea Utukufu Wake, Ukubwa Wake na Uwezo Wake, kuwa Yeye ni Mweza wa kila kitu na Anafanya kila kitu Anachotaka kukifanya. Yeye pekee Ndiye Mwabudiwa wa kweli na Yeye pekee Yake Ndiye Rabb (Muumba, Mtoaji wa Riziki na Mwenye kutoa ukimu wa kila kiumbe). Alimchukua mja Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka Makkah na kumpeleka katika Masjid Al-Aqswaa (Msikiti wa mbali) huko Jerusalem katika usiku mmoja. [Tafsiyr ya Ibn Kathiyr].

 

 

 

Baadhi Ya Miujiza Ya Rasuli Wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam):

 

 

Qur-aan:

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa miujiza mingi na Rabb wake. Muujiza wake mkubwa ni Qur-aan; Kitabu ambacho kiliteremshwa miaka 1400 iliyopita na hakuna hata mtu mmoja ambaye ameweza kubadilisha hata herufi moja au kuleta kitabu cha mfano wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema: 

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijr 15: 9]

 

 

Aayah hii ni changamoto dhidi kwa makafiri waliojaribu kuandaa mifano ya Qur-aan wakashindwa na kufedheheka.

 

 

Vitabu vingine vitokavyo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Tawraat na Injiyl ambavyo viliharibiwa ima kwa kuongeza maneno au kupunguzwa maneno.    Ama Qur-aan Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametoa ahadi kuwa “Atailinda” na kweli Ameilinda na Ataendelea Kuilinda.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila Nabiy aliyekuja kabla yangu alipewa muujiza na miujiza hiyo ilibakia kuwa miujiza wakati wa uhai wao hao Manabii:  Mfano ‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) alikuwa na muujiza wa kutibu watu wagonjwa na kufufua wafu Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) alipewa fimbo ya miujiza na mambo mengine, nami nimepewa muujiza wa milele, Qur-aan itabakia kuwa muujiza hadi kusimama Qiyaamah. Hivyo natarajia kuwa wafuasi wangu watakuwa ni wengi katika idadi zaidi ya wafuasi wa Manabii wengine kwa kuwa muujiza wangu utabakia na utakuwepo hadi Siku ya Qiyaamah ambao ni Qur-aan. Kila anayekisoma Kitabu hiki hata kama ni mpagani basi yeye huvutika na kuona ukweli uliomo ndani yake na kuona hakuna aliyekiandika isipokuwa Rabb wa Mbingu na Ardhi.”  [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

Kupasuka Kwa Mwezi:

 

Muujiza mwingine wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ulikuwa ni kupasuka kwa mwezi. Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) anasema katika riwaayah yake, kuwa watu wa Makkah walimtaka Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaonyeshe muujiza na akawaonesha kupasuka kwa mwezi. [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu ya 4 Namba 831].

 

 

Kutoka Maji Kutoka Vidole Vya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Imepokewa kutoka kwa Jaabir ibn Abdillaah akisema: “Nilikuwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na muda wa kuswali Swalaah ya Al-‘Aswr ukafika. Tulikuwa hatuna maji isipokuwa maji kidogo tu ambayo yalikuwa ndani ya chombo ambayo yaliletwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) . Basi aliweka mkono wake ndani ya maji hayo na kutandaza vidole vyake na huku akisema, “Njooni Haraka watu wote ambao wanataka kutawadha Hii ni baraka kutoka kwa Allaah.” Nikaona maji yakibubujika kutoka katika vidole vyake. Hivyo watu walitawadha na wengine wakawa wanakunywa maji hayo na mie nilitaka kunywa maji mengi kupita kiasi (kwa sababu nilijua kuwa ilikuwa ni baraka). Mpokeaji wa Hadiyth hii kutoka kwa Jaabir alisema: “Nilimwuliza Jaabir Je, mlikuwa watu wangapi wakati huo?” Akajibu, “Tulikuwa watu elfu moja na mia nne.” [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 7 namba 543 na Swahiyh Muslim, Juzuu 4 namba 779].

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amepewa miujiza mingine mingi. Muujiza mwingine mkuu ni ule wa Israa na Mi’raaj au “Safari ya Usiku.”

 

Makala hii ni kujaribu kuonesha faida zinazopatikana katika safari hii na mafunzo yanayopatikana katika muujiza huu mkubwa.

 

 

Tukio la Israa na Mi’raaj lina hekima na mafunzo makubwa mno. Funzo lake kubwa ni kuwa mja hapaswi kukata tamaa, lazima awe daima anamtegemea Rabb wake kuwa atamletea faraja hata kama kutakuwa na mambo mazito yanamkabili. Zaidi ya hapo mwana Aadam anapaswa kuwa daima karibu na Rabb wake hasa wakati anapokuwa anakabiliwa na mambo mazito na vitendo vya kuhuzunisha au mikasa mizito, kwani matatizo hayo hupotea kama vile yalikuwa hayajatokea.

 

 

 

 

Baadhi Ya Matukio Yaliyotokea:

 

 

1- Kifo cha Abuu Twaalib.

 

 

Abuu Twaalib alikuwa ni mlinzi na mlezi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati Waislamu wakiwa Makkah na yeye alimkinga dhidi ya mashambulizi ya makafiri wa Makkah. Watu wa Makkah walipopinga kwa nguvu risala ya Muhammad na kuanza kumshambulia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na kuwashambulia Waislamu, Abuu Twaalib alikinga kifua chake na kumhami mtoto wa nduguye. Alisema, “Tunapenda kusaidia tunakubali ushauri wako na tunayakubali maneno yako. Hawa ni watu wa jamii yako ambao umewakusanya na mimi ni miongoni mwao, lakini mimi ni mwepesi kuliko wote kufanya kile ukitakacho. Fanya kila lile uliloamriwa kufanya. Nitakulinda na kukuhami, lakini siwezi kuiacha dini yangu.” Abuu Lahab akapayuka na kusema: “Wa-Allaahi jambo hili ni jambo ovu na wewe lazima umkataze hayo ayafanyayo kabla ya watu wengine hawajamkanya.” Abuu Twaalib akasema: “Naapa nitaendelea kumlinda na kumhami katika maisha yangu yote.” [Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm].

 

 

Al-‘Abbaas bin Abdil-Mutwalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kuwa alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hukuwa mwenye kumsaidia ‘Ami yako, Abuu Twaalib, japo kuwa yeye alikuwa ni mtu mwenye kukuhami sana na alikuwa anachukizwa sana kwa mambo uliyokuwa unatendewa na Makureshi.” Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Yuko katika moto mwepesi, kama si mimi angelikuwa kwenye moto wa tabaka la chini kabisa huko Jahanam.” [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 5 Namba 222].

 

 

Hivyo licha ya kuwa Abuu Twaalib ni kafiri, lakini alimuunga mkono Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nguvu zake na mali yake dhidi ya makafiri. Wakati Abuu Twaalib alipokuwa hai makafiri walikuwa hawawezi kumdhuru Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, kifo cha Abuu Twaalib kilikuwa ni mwanya kwa makafiri wa kuendeleza vitimbi vyao dhidi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na dhidi ya Waislamu kwa ujumla. Tabia yao ya ukatili ilimfanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aone maisha mjini Makkah ni magumu. Kusilimu kwa Maswahaba mjini Makkah ilikuwa ni njia ya kujitangazia uadui wa wazi wazi na wakawa wanapata madhila na kuadhibiwa vibaya. Kila aliyesilimu aliambiwa afanye moja kati ya mambo mawili: aritadi au aondoke hapo nchini au sivyo basi roho yake itafariki dunia; makafiri hawakutaka njia nyingine zaidi ya hiyo. Lakini Maswahaba licha ya kuwa hiki kilikuwa ni kipindi kigumu sana na chenye taabu kubwa sana katika maisha yao kutokana na adhabu na madhila waliyoyapata, waliendelea kusimama imara juu ya imani ya Uislamu na walisonga mbele na Rasuli wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika msimamo huo.

 

 

Kupanuka kwa Uislamu kuliwaudhi sana makafiri na wakajaribu kila njia ili kuzuia na kukinga Uislamu usiwepo katika nchi yao. Ulinganiaji wa Dini hii ukawa mzito kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hata kuishi mjini Makkah ikawa ni hali ngumu sana kwake na kwa Waislamu.

 

 

2- Kifo cha Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 

Ni miezi miwili tu baada ya kifo cha Abuu Twaalib. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipata tatizo lingine zito lililomhusu yeye binafsi. Mke wake na Mama ya Waumini, Sayyidah Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alifariki. Mama wa Waumini Khadiyjah, alikuwa ni rehma kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Alikuwa daima na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati akipata madhila na maudhi ya Makureshi na alikuwa naye siku zote wakati wa mitihani mizito ilipokuwa inamfikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa mahasimu wake wa Kikureshi na walikuwa pamoja katika hali hiyo kwa muda wa miaka 25. Na kwa yote hayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukaribu huo aliokuwa nao Mama wa Waumini Khadiyjah alisikitika sana kwa kifo cha mkewe mpenzi na kuna wakati alisikika akisema juu ya Sayyidah Khadiyjah: “Aliniamini wakati wengine hawakufanya hivyo, Alijiunga na Uislamu wakati watu walikuwa hawataki kufanya hivyo. Pia alinisaida na kuniliwaza mwenyewe na na kwa mali zake wakati kulikuwa hakuna hata mtu wa kuniunga mkono. Pia nilipata watoto kutoka kwake.’’ [Musnad Ahmad 6/118].

 

 

Matukio haya mawili yalitokea mfululizo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amefikia hali ya kubabaika namna gani awaongoze Makureshi wa Makkah, basi aliangalia upande wa Twaaif mji ambao kwa wakati huo ulikuwa unahitajia msaada na uongozi. Lakini hata huko pia hakupokelewa na hali hiyo kuongeza machungu moyoni mwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata akaona kipindi hicho kuwa ni “Mwaka wa Huzuni”.

 

 

Baada ya mitihani hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimchukua mja Wake katika muujiza mkubwa wa Israa na Mi’raaj ili amwoneshe Aayah Zake na kumpatia msaada na himaya. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ  

Ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu.  [Al-Israa (17: 1)]

 

 

Kwa muujiza wa Israa na Mi’raaj, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliweka msingi kwa waja Wake kuwa hata kama makafiri wangelifunga mlango wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah Ndiye Mwenye Kumhami na ndio Mlezi Wake na milango ya Peponi iko wazi kwa ajili ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakuna nguvu ambayo inaweza kumteza au kumdhuru yule ambaye yuko chini ya ulinzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Israa na Mi’raaj ilikuwa ni dalili ya kuonesha kufanikiwa kwa Da’wah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ushindi wake juu ya maadui zake pamoja na kuwepo kwa mitihani hiyo.

 

 

Safari ya Israa:

 

Lini kilikuwa kipindi cha Israa na Mi’raaj?

 

Tarehe hasa ya tukio la Israa na Mi’raaj haifahamiki kwa uhakika.  Ibn Kathiyr amenukuu kutoka kwa ‘Ulamaa mbali mbali katika kitabu chake Al-Bidaayah wan-Nihaayah (3/108) juu ya terehe ya tukio hilo. ‘Ulamaa wengi wanaona kuwa tarehe hiyo ilikuwa kati ya miezi 12 na 16 kabla ya Hijrah yake kwenda Madiynah. Na wa zaidi ya hapo wamekhitilafiana juu ya siku na hata huo mwezi.

 

Kabla ya Safari:

 

Malaika Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alifungua kifua cha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akatoa moyo wake na kuuosha kwa maji ya Zam Zam. Anasema Anas Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa katika Israa na Mi’raaj kutoka Masjid Al-Haraam (Msikiti Mtukufu Makkah). Watu watatu walimjia (ndotoni) akiwa amelala ndani ya Masjid Al-Haraam kabla hakufunuliwa Wahyi kwake. Mmoja wao akasema: “Ni yupi kati ya hawa watu?” Malaika wa kati akasema: “Yule ambaye ni mbora kuliko wote.” Na Malaika wa Mwisho akasema: “Chukueni aliye mbora wao.” Mambo haya yalitokea katika usiku huo huo. Usiku huo hakuwaona, lakini aliwaona usiku mwingine ambapo tayari Wahyi ulikuwa umefunuliwa kwake na alikuwa macho amelala lakini alikuwa hadhiri (Ni kawaida ya Manabii wote kulala macho wakati wako hadhiri). Wale Malaika hawakumsemesha bali walimbeba hadi wakamfikisha katika kisima cha Zam Zam. Miongoni mwao ni Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alikuwa akiongoza na kuelekeza kifanyike nini. Alipasua sehemu kati ya koo na kati ya kifua na akatoa vyote vilivyokuwemo kifuani na kuviosha kwa maji ya Zam Zam kwa mikono yake mwenyewe na pia kusuuza sehemu za ndani za mwili na kisha kikaletwa chano cha dhahabu kikiwa na bakuli la dhahabu kililetwa ndani ya bakuli mkiwa mkajazwa iymaan na busara. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akachukua vitu hivyo kutoka ndani ya bakuli na kuvijaza kifuani mwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kisha akachukua viungo vya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na mishipa ya damu akavijaza kifuani kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kukifunga kifua.” [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608, na Juzuu 5 Namba 227].

 

 

Israa maana yake ni safari ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yeye akiwa ni mwili wake na akili zake na roho yake kutoka Ka’bah huko Makkah mpaka Masjid Al-Aqswaa (Msikiti wa Mbali) huko Quds (Jerusalem) akiwa amebebwa na mnyama wa ajabu mwenye kuvutia umbo lake anayeitwa Buraaq na kisha safari ya kurejea kwake Makkah.

 

 

Al-Buraaq:

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa kutoka Masjid Al-Haraam, Makkah mpaka Masjid Al-Aqswaa mjini Quds juu ya mnyama aitwaye Al-Buraaq akiwa ameambatana na Malaika Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwelezea Al-Buraaq kuwa: “Nililetewa Al-Buraaq, mnyama mrefu wa umbo na mweupe, ni mkubwa kiasi zaidi ya punda  lakini ni mdogo kuliko nyumba, ambaye anapokwenda mbio hatua yake ni upeo wa macho yake. Nilimpanda mnyama huyo mpaka nikafika Masjid Al-Aqswaa huko Al-Quds (Jerusalem). Hapo nilimfunga pale mahali ambapo Manabii wengine walikuwa wakifunga wanyama wao.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

Anas Bin Maalik alisema: “Katika usiku ambao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipelekwa mbinguni, Al-Buraaq aliletwa kwake akiwa amefungwa vikuku na ana matandiko, lakini alifanya ugumu kidogo, na ndipo Jibriyl alipomwambia Al-Buraaq: “Je unafanya haya kwa Muhammad? Hakuna mtu mtukufu aliyewahi kukupanda ambaye ni mtukufu zaidi ya huyu mbele ya Macho ya Allaah.” Kisha akatoa jasho.”  [At- Tirmidhiy na Musnad Ahmad].

 

 

Maana Ya Al-Buraaq Kwa Kiarabu Ni Mwale Unaotoka Katika Mwanga:

 

 

Leo hii, Wanasayansi wanatuambia kuwa mwanga una mwendo kasi zaidi ya vitu vyote duniani. Huenda masafa ya maili 700 milioni kwa saa moja. Miaka 1400 iliyopita wakati ambapo kulikuwa hapajatokea utafiti na uvumbuzi palikuwa hakuna mtu ambaye aliweza hata kukisia mwendo kasi wa mwanga wala ukweli wake ukoje. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walimwita mnyama huyo kama Al-Buraaq kwa msingi wa mwendo wake ulivyo na kasi kali. Huu ni ukweli ambao unthibitisha ukweli wa Uislamu na ukweli wa Unabiy wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Alivyosema Allaah ndani ya Qur-aan:

 

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٥٣﴾

Tutawaonyesha Aayaat (ishara, dalili) Zetu katika peo za mbali na katika nafsi zao, mpaka iwabainike kwamba hiyo ni haki! Je, haitoshelezi Rabb wako kuwa Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu? [Fusswilat 41: 53].

 

 

 

Hapo kale watu walipinga na kusema: “Mnyama huyo katokea wapi tena ambaye alimchukua Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka sehemu moja ya dunia mpaka nyingine na kisha kapita naye katika anga za mbingu na tena katika usiku mmoja?”

 

Leo hii tunaona vipando ambavyo vimeundwa na wana Aadam; roketi na misali vikikata maelfu ya maili kwa muda dakika chache tu. Basi iweje Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ashindwe kuumba mnyama mwenye uwezo wa kukata masafa ya mamilioni ya maili kwa muda mfupi, ilhali Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Muumba wa ulimwengu na Wana Aadam hao na Ndiye Yeye Aliyewajaalia uwezo wa kuunda hivyo vitu?

 

 

Kituo cha kwanza cha Safari ni Al-Aqswaa: 

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Kisha niliingia Masjdi Al-Aqswaa, nikaswali Raka’ah mbili.” [Swahiyh Muslim]. 

 

 

Riwaayah nyingine ambazo zinaeleza kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali na Manabii wengine hapo Msikiti wa Al-Aqswaa na yeye akiwa Imaam.

 

 

Msikiti wa Al-Aqswaa umekuwa na sifa ya kuwa ni kituo cha Manabii wote, toka siku ya Al-Khaliyl Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam). Hivyo Manabii wote walikusanyika hapo na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa Imaam wao. Hii ni dalili ya nafasi kubwa aliyo nayo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni Nabiy wa mwisho miongoni mwa Manabii wengine (‘Alayhimus- Salaam). [Tafsiyr Ibn Kathiyr].

                       

                      

Kisa cha Israa na Mi’raaj kimeelezwa ndani ya Qur-aan [Al-Israa 17:1]

 

 

Aayah inayofuatia inaeleza matendo ya aibu na makosa ya Mayahudi na kufuatia juu ya hayo makemeo makali ya Qur-aan. Mpangilio huo si kwa bahati tu, Al-Quds ilikuwa ni kituo cha kwanza cha safari hii ya Usiku na hapa kuna ujumbe ambao unaelekezwa kwa Mayahudi na kupewa ujumbe kuwa hadhi waliyokuwa nayo ya kuongoza dunia na bin Aadam kwa ujumla imetanguliwa. Utenguzi wa uongozi kwa Mayahudi ulitokana na mabaya yao waliyokuwa wakiyafanya na yale ambayo wanaendelea kuyafanya.

 

Ujumbe huo unathibitisha wazi wazi kuwa uongozi huo umehamia kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) achukue uongozi wa makao makuu ya ‘Aqiydah ya Baba Ibraahiym na pia kuwa makao hayo sasa ni Makkah na Masjdi Al-Aqswaa (Msikiti wa mbali) huko Al-Quds. Hivyo mamlaka hayo yalihamishwa kwenda kwenye taifa ambalo ni la wenye taqwa na lenye utii kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na Nabiy ambaye amependelewa kubeba Qur-aan ambayo inaongoza watu kuelekea kwenye ukweli. [Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm].

 

 

Uchaguzi wa Asili (Fitwrah):

 

 

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:

 

“Vyombo viwili vya dhahabu vililetwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kimoja kikiwa kimejazwa maziwa na kingine kikiwa kimejazwa mvinyo (pombe). Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) achague kinywaji kati ya hivyo vinywaji viwili. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichagua maziwa na akainua kile chombo na kuyanywa. Jibriyl alisema, “Umeongozwa katika fitwrah na umefikia daraja ya fitwrah. Kama ungelichagua mvinyo, watu wako wangelipotea.” [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 6 Namba 232].

 

 

Neno fitwrah lina maana ya silika asili ambayo imo kwa kila mtoto anapozaliwa.  Silika hiyo inamtambua Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); kama silika hiyo haikufisidiwa humpeleka mja katika iymaan ya Tawhiyd ya Allaah.

 

Imaam An-Nawawiy alisema kuwa kauli ya Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Umechagua fitwrah” maana yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amechagua Dini ya Islaam, yaani: “Umechagua nembo ya Islaam na Istiqaamah (kuwa imara katika Njia Iliyonyooka). Maziwa yalikuwa ni alama tu kwa sababu ni rahisi kuyanywa wakati mvinyo ni “mama wa maasi na maovu” na chanzo cha matendo ya kikatili.”

 

Kwa lugha nyepesi ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa vitu viwili; kimoja kinawakilisha matendo mema na kingine kinawakilisha matendo maovu na viliwekwa mbele ye Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa silika akachagua kile kilicho kizuri. Kwa leo hii mtu akiacha fitwrah na kuanza kutafuta vitu vinginevyo anaonekana jinsi anavyohangaika baada ya kuacha njia ambayo amewekewa na Rabb wake. Ni wajibu wa mwana Aadam kushikamana na Njia ambaye ameamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa sababu Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾

 “Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, na Tutamfufua Siku ya Qiyaamah hali akiwa kipofu.”

 

قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾

Atasema: “Rabb   wangu! Kwa nini Umenifufua kipofu, na hali nilikuwa naona?”

 

قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا ۖ وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾

 (Allaah) Atasema: “Hivyo ndivyo, zilikufikia Aayaat Zetu ukazisahau   na kadhaalika leo umesahauliwa.” [Twahaa 20: 124 - 126].

  

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَن كَانَ فِي هَـٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٧٢﴾

Na atakayekuwa kipofu katika hii (dunia) basi yeye Aakhirah atakuwa kipofu na atapotea zaidi njia.  [Al-Israa 17: 72].

 

 

 

 

 

Mi’raaj ni hali iliyomfikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kupaa mbinguni kutoka Masjid Al-Aqswaa na kwenda katika mbingu ya saba. 

 

Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alikuwa naye katika msafara huo wa kupaa. Ibn Kathiyr aliandika katika kitabu chake cha Al-Bidaayah wan-Nihaayah: “Safari ya kupaa haikuwa kwa kutumia Al-Buraaq kwa sababu alikuwa amefungiwa katika mlango wa Baytul-Maqdis, akisubiri Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akirejea kutoka mbinguni ili ampeleke Makkah.”

 

 

Baada ya ziara ya Masjid Al Al-Aqswaa, Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walianza safari ya kwenda mbinguni. Kila alipofika kwenye mbingu alibisha hodi na aliulizwa na walinzi wa mbingu hiyo, “Wewe nani?” na alipojibu kuwa ni “Jibriyl!” aliuliulizwa tena, “Nani umefuatana naye?” Alisema “Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)” Na aliulizwa tena, “Je ameitwa?” Na Jibriyl alijibu: “Naam, hakika ameitwa!” Na ndipo Malaika walisema: “Marhaba, anakaribishwa, safari yake ni njema kabisa.” Milango ilifunguliwa na wakamwona Aadam (‘Alayhis-Salaam). Jibriyl alisema akimwambia Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Huyu ni baba yako Aadam (‘Alayhis-Salaam). Mpe heshima zake kwa salaam.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsalimu na Aadam aliitikia na akasema: “Unakaribishwa ee mwanangu Nabiy Mtukufu.” na akamwombea du’aa njema.

 

Kisha walipanda mbingu ya pili na sawa kama hapo awali Jibriyl alibisha hodi na kuwaomba walinzi kufungua milango ya mbingu na wakamuuliza maswali kama yale aliyoulizwa hapo mbingu ya kwanza. Hali ya namna hiyo iliendelea hadi kufika mbingu ya saba. Hatima milango ilifunguliwa na wakawa wamekaribishwa kwa kauli ya “Marhaba, anakaribishwa, safari yake ni njema kabisa.”

 

Katika mbingu ya pili Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona ‘Iysaa bin Maryam (‘Alayhimas-Salaam) na Yahyaa bin Zakariyyaa (‘Alayhimas-Salaam) mtu na binamu yake. Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Nilikutana na ‘Iysaa bin Maryam. Alikuwa na umbo la wastani na uso wake ni mwekundu kama vile katoka kuoga…” [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 647]

 

 

 Jibriyl alisema: “Hawa ni Yahyaa bin Zakariyyaa na ‘Iysaa (‘Alayhimus Salaam) wasalimu.” Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasalimu na wote wawili walijibu salamu zake na kusema: “Unakaribishwa Ee ndugu yetu Nabiy Mtukufu.” Na kisha wakamwombea dua njema.

 

 

Baada ya hapo walipanda mbingu ya tatu ambako walimkuta Yuwsuf (‘Alayhis-Salaam) ambaye amejaliwa uzuri wa sura wa nusu ya dunia. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsalimu naye akajibu salamu hiyo na akamkaribisha na akaondoka nao wakaenda mbingu ya nne pamoja. Milango ya mbingu ya nne ilifunguliwa na Idriys (‘Alayhis-Salaam) alikuwa hapo. Qur-aan inasema juu yake: 

 

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِدْرِيسَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا ﴿٥٦﴾

Na mtaje katika Kitabu Idriys. Hakika yeye alikuwa mkweli wa dhati na Nabiy. [Maryam 19: 56-57].

 

 

Idriys (‘Alayhis-Salaam) alimkaribisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakasalimiana. Kisha Idriys (‘Alayhis-Salaam) aliondoka nao wakaenda mbingu ya tano ambako walimkuta Haaruwn (‘Alayhis-Salaam). Nabiy Haaruwn (‘Alayhis-Salaam) aliwapokea na akajibu salamu zao na kumwombea dua njema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kisha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipelekwa mbingu ya sita ambako alimkuta Muwsaa (‘Alayhis-Salaam). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Nilikutana na Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) nilipokwenda Mi’raaj. Alikuwa ni mtu mrefu akiwa na nywele ndefu kama vile ni mtu wa kabila la Shamu. [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 4 Namba 647].

 

 

Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) alimkaribisha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam), na wakasalimiana na walipoondoka kuendelea na safari yao, Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) alilia. Aliulizwa kwa nini analia basi Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) alijibu: “Nalia kwa sababu amepelekwa Nabiy duniani baada yangu, kijana ambaye wafuasi wake wataingia Peponi kwa makundi makundi zaidi ya watu wangu.”

 

Kisha waliendelea na safari yao kuelekea mbingu ya saba na huko wakamkuta Ibarahiym (‘Alayhis-Salaam) akiwa ameegemea Baytul-Ma’amuwr (Nyumba ambayo inatembelewa mara kwa mara). Ndani ya nyumba hii kila siku wanaingia Malaika 70,000 na wala hawarudi tena … na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Nilimwona Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) ambaye mimi nafanana naye sana kuliko watoto wake wote.” [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 4 Namba 647].

 

 

Ibraahiym alimkaribisha Muhammad na wakasalimiana na Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) akamwombea dua njema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 5 Namba 227 na Swahiyh Muslim]

 

 

Ameeleza ‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alisema: “Ndani ya usiku wa Mi’raaj nilikutana na Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) ambaye aliniambia, “Muhammad wapelekee Salaam zangu watu wako na waambie kuwa Jannah ni uwanda mpana ambao umeenea udongo safi, maji safi na miti yake hutoa sauti; “Subhaana Allaah, AlhamduliLLaah, laa ilaha illa Allaah, Allaahu Akbar. [At-Tirmidhiy namba 1445]

 

 

Kituo Cha Mwisho Cha Safari - Sidratul-Muntahaa

 

 

Amesema ‘Abdullaah bin Mas’uwd, “Wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipochukuliwa safari yake kwenda mbinguni alifikishwa mpaka Sidratul-Muntahaa ambapo kila kitu kinachopanda kutoka ardhini hukomea na na kile kinachoshuka kutoka juu hukomea hapo…” [Muslim 329].

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Kisha nilichukuliwa hadi Sidratul-Muntahaa mti ambao majani yake ni kama masikio ya tembo na matunda yake makubwa kama mitungi. Na mti huu ulipogubikwa na amri za Allaah, basi ulibadilika kuwa katika hali ambayo hakuna kiumbe ambaye anaweza kumsabihi Allaah kwa uzuri wake.” [Muslim].

 

Kisha katika riwaayah nyingine: “Kisha nilipandishwa mbinguni hadi kufikia Sidratul-Muntahaa. Matunda yake yalikuwa makubwa kama magudulia ya Hajr (sehemu ambayo ni karibu na Madiynah) na majani yake yalikuwa makubwa kama masikio ya tembo. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema: “Huu ni mkunazi wa mbali kabisa.” Kulikuwa na mito minne karibu yake miwili ikiwa haionekani na miwili ikiwa wazi inaonekana. Nikauliza: “Hii mito miwili ni mito gani ee Jibriyl?” Basi akajibu: “Ama kwa mito miwili isiyoonekana ni mito miwili ya Peponi na mito miwili inayoonekana ni mto wa Naili (Nile) na Furati (Euphrates).”

 

 

Hii hadiyth haina maana kuwa mito hiyo miwili inayoonekana kuwa asili yake ni Peponi, lakini ni kuonyesha tu mahali ambapo atakuwepo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na watu daima watabakia wenye kushikamana na Uislamu na kurithishana kizazi kimoja baada ya kingine. [Ar-Rahiyq Al- Makhtuwm].

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alisema: “Jibriyl alinipandisha mbinguni hadi tukafika Sidratul-Muntahaa (mkunazi ambao una mpaka wa mwisho) ambao ulikuwa umepamba kwa rangi ambazo haziwezi kuelezeka. Kisha niliruhusiwa kuingia Peponi ambamo nilikuta mahema (madogo madogo) au kuta ambazo zimejengwa kwa lulu na ardhi yake ilikuwa ni ya miski.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 1 Namba 345].

 

 

Wakati nilikuwa natembea humo Peponi (katika usiku wa Mi’raaj) niliona mto na katika kingo zake kulikuwa na vijihema ambavyo vimejengwa kwa kutumia lulu zenye uwazi katikati. Niliuliza: “Nini kile ee Jibriyl?” Akasema: “Huo ndio mto wa Al-Kawthar ambao Rabb wako Amekupa wewe.”  Basi harufu iliyotoka humo au kwenye matope ilikuwa ni miski. (Mmoja wa wapokeaji wa riwaya hii, Hudba hana hakina ilikuwa imetumika ibara gani). [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 8 Namba 583].

 

 

“Katika usiku wa Mi’raaj huko mbinguni pia nilimwona Maalik (Malaika) mlinzi wa Milango ya Motoni na Ad-Dajjaal; ni miongoni mwa miujiza ambayo Allaah Alinionesha huko.”

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha akasoma:

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَلَا تَكُن فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَائِهِ

Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Kitabu, basi usiwe na shaka katika kukutana naye.  [As-Sajdah 32: 23)]

 

Hivyo usiwe na mashaka juu ya kukutana na Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) huko mbinguni katika usiku wa Mi’raaj. [Al-Bukhaariy, Juzuu 4 Namba 462].

 

 

Na kwa riwaayah nyingine Anas bin Maalik amesema, “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Katika usiku wa Mi’raaj nilipopandishwa kupelekwa mbinguni nilipita karibu na watu ambao walikuwa wana makucha ya shaba na walikuwa wakijiparura nyuso zao na vifua vyao. Nilisema: Hawa ni nani ee Jibriyl?” Alijibu na kusema kuwa: “Hawa ni wale watu waliokuwa na tabia ya kusengenya na kuwazulia watu maneno machafu na kuharibu heshima za watu.” [Sunan Abiy Daawuwd, namba 4860].

 

 

Na katika riwaayah nyingine: Abuu Hurayrah anasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Katika usiku wa Mi’raaj nilipopelekwa mbinguni niliona watu ambao matumbo yao yalikuwa makubwa kama nyumba na ndani yake kuna majoka ambayo yalionekana nje ya matumbo yao. Niliuliza kuwa walikuwa kina nani, na Jibriyl alinijibu kuwa wao walikuwa wale watu waliokuwa wakila mali ya riba.” [Musnad Ahmad, Ibn Maajah na At-Tirmidhiy namba 2828].

 

 

Kasema Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu):  “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Usiku wa Mi’raaj nilipopelekwa mbinguni niliwakuta watu na midomo yao ikichanwa na mikasi ya moto. Nikamuliza Jibriyl ni nani hao na akasema walikuwa ni wahubiri miongoni mwa wafuasi wangu, ambao walisema ambayo wao hawakuyafanya.” [At-Tirmidhiy (ghariyb) Namba 4801].

 

 

Buraydah bin Al-Haasib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alieleza jinsi siku moja asubuhi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwita Bilaal na kusema: “Umefanya nini mpaka ukaingia Peponi kabla yangu? Sikupata kuingia Peponi pasina kusikia mchakacho wako ukiwa mbele yangu.” Bilaal akajibu: “Sijapata kuadhini ila baada yake kuswali rakaa mbili. Na sijapata kutenguka wudhuu ila nilitawadha papo hapo na kujiona kuwa nina deni kwa Allaah la rakaa mbili.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ni kwa sababu hizo.” [At-Tirmidhiy namba 326].

 

 

Na Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Nilijiona naingia Peponi na mara nikamwona bi Ar-Rumayswah, mke wa Abuu Twalhah. Nilisikia hatua za mtu. Nikauliza: “Wewe nani?” Mtu mmoja akajibu: “Ni Bilaal.”  Kisha nikaona kasri na mwanamke akiwa amekaa katika ukumbi wake. Nikauliza: “Kasri la nani hili?”  Basi kuna mtu alijibu: “Hilo ni la ‘Umar.” Nikatamani kuingia ili nione ndani kukoje, lakini nilikumbuka jinsi ‘Umar alivyo na wivu (ghiyrah) basi sikuingia.” Mara ‘Umar akadakiza “Fidaka Abiy wa Umiy, Yaa Rasula-Allaah! Nitathubutu namna gani mimi kudhania kuwa umenikosea wewe kwa kuingia kwangu?” [Al-Bukhaariy, Juzuu 5 Namba 28].

 

 

Kutokana na Hadiyth hizi tunaona jinsi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa mtu mwenye kulea watu wake na kuwafundisha mambo kwa hekima. Alipowafundisha tabia njema haikuishia bali yeye aliyafanya hayo kwa mifano ya wazi wazi kabisa. Alipata kusema: “Kama mtu atachungulia katika nyumba ya mtu bila rukhsa ya mwenyewe na huyo mwenye nyumba akachokora jicho lake, kutakuwa hakuna tatizo wala hilo jicho halitalipwa fidia”. [Sunan Abiy Daawuwd, namba 5153].

 

 

Kwa sababu yule anayechungulia katika nyumba za watu amefanya wizi kwa kuingilia siri za watu na hifadhi zao na hivyo Allaah Ametoa hukumu kali kwa kosa wizi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Mkono wa mwizi unapaswa kukatwa hata kama kwa wizi wa robo dinar.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 8 Namba 781].

 

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Anakutana Na Allaah - Je, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Alipata Kumuona Rabb Wake?

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ ﴿٨﴾

Kisha akakurubia na akashuka.

 

فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ أَوْ أَدْنَىٰ ﴿٩﴾

Kisha akawa kiasi cha umbali wa mipinde miwili au karibu zaidi.

 

فَأَوْحَىٰ إِلَىٰ عَبْدِهِ مَا أَوْحَىٰ ﴿١٠﴾

 (Allaah) Akamfunulia Wahy mja Wake yale Aliyomfunulia Wahy.

 

 

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ ﴿١١﴾

Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.

 

أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ ﴿١٢﴾

Je, mnambishia kuhusu yale aliyoyaona?

 

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ ﴿١٣﴾

Na kwa yakini amemuona (Jibriyl) katika uteremko mwingine.

 

عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ ﴿١٤﴾

Kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa.  

 

عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ ﴿١٥﴾

Karibu yake kuna Jannah ya Al-Ma-waa.

 

إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ ﴿١٦﴾

Ulipoufunika mkunazi huo unachokifunika

 

مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ ﴿١٧﴾

Jicho lake halikukengeuka wala halikupinduka mipaka.

 

لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ ﴿١٨﴾

Kwa yakini aliona miongoni mwa Aayaat (ishara, dalili) za Rabb wake kubwa kabisa. [An-Najm (53: 8-18)]

 

 

 

Waislamu wa mwanzo walitofautiana juu ya swala la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama alimuona Rabb wake kwa jicho lake au hapana.

 

 

Mama wa Waumini ‘Aaishah, Abuu Hurayrah na Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wanakataa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa macho yake. Kuna riwaayah kupitia kwa Ibn Abiy Haatim kwamba Ibn Mas’uwd alieleza Aayah zilizotajwa hapo juu, kwamba, “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Jibriyl katika umbo lake halisi mara mbili. Na mara Jibriyl alipokuwa katika umbo lake halisi basi alifunika anga yote kwa mwili wake. Kwa mara ya pili Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwona katika umbo lake halisi ni wakati wa safari yao ya kwenda mbinguni. Na hiyo ndiyo maana ya maneno:

وَهُوَ بِالْأُفُقِ الْأَعْلَىٰ ﴿٧﴾

Naye yuko juu kabisa katika upeo wa macho. [An-Najm (53: 7)]  [Tafsiyr Ibn Kathiyr].

 

 

Hivyo Aayah hii inaonyesha kuwa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alijongea na kuwa karibu na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Fat-hul-Baariy, ukurasa 263, 264 ya Juzuu 17].

 

 

Amesimulia Masruwq (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Nilimuuliza Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) “Ee mama wa Waumini, Je, Rasuli wa Allaah alipata kumwona Rabb wake? Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akasema: “Hicho ulichokisema kinafanya mwili wangu kusisimka na nywele kujivuta. Jua kuwa iwapo mtu atakwambia kitu katika hivi vitatu vifuatavyo ni mwongo: “Mtu akikwambia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake, ni mwongo huyo.” Kisha mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akasoma:

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote; Naye ni Mwenye kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika [Al-An’aam (6: 103)]

 

 وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ﴿٥١﴾

Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi, au Hutuma Mjumbe, kisha Anamfunulia Wahy Ayatakayo kwa idhini Yake; hakika Yeye ni Mwenye ‘Uluwa, Ametukuka, Mwenye hikmah wa yote. [Ash-Shuwraa (42: 51)]

 

 

Jambo la pili kama mtu atakwambia nini kitatokea kesho, ni mwongo.”  Kisha akasoma:

 

  وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ  

  Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho. [Luqmaan (31: 34)]

 

Na pia akaongezea jambo la tatu kwa kusema: “Yeyote atakayekuambia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alificha baadhi ya Wahy alioletewa na Allaah kutangaza, ni mwongo na akasoma:

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿٦٧﴾

Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake. Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu. Hakika Allaah Haongoi watu makafiri [Al-Maaidah (5: 67)]

 

 

Kisha Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliendelea kusema: “Lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Jibriyl (Alayhis-Salaam) katika umbo lake halisi mara mbili.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 6 Namba 378].

 

Kwa upande mwengine Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) alisema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Allaah, na akasema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake mara mbili. [Tafsiyr Ibn Kathiyr].

 

Al-Haafidhw Ibn Hajar alisema: “Maelezo ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) yamekuja katika hali ya kutodhibitiwa (hayaelezi kama Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake kwa macho yake au vipi) wakati kauli za Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na wenziwe zimedhibitiwa kwa kusema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumuona Allaah “Kwa macho yake”. Tunaweza kuunganisha kauli hizo mbili kwa kusema Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikataa muono “Kwa macho yake” na kauli ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa ni kamuona kiroho.” [Fat-hul-Baariy, 8/608].

 

 

Pili, kauli hizo mbili, ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa), kwa njia nyingine kuwa kauli ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alisema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake wakati akiwa katika usingizi, jambo ambalo ni ndoto ya kweli na isiyokuwa alimuona Siku ya Mi’raaj wakati kauli ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) inakataa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumuona Rabb wake wakati yeye akiwa macho, lakini kauli hiyo haikatazi kuwa  Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake akiwa usingizini. Alichokana hapa ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumuona Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa macho yake meupe, akiwa macho.

 

 

Wale ambao wanao msimamo kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake kwa macho yake meupe wanaleta Hadiyth Dhaifu. Hakuna Hadiyth Swahiyh ambayo inaeleza ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake kwa macho yake akiwa macho. Wenye msimamo huo wanaleta Hadiyth ya At-Tirmidhiy ambayo Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) anasema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake. Ikrimah alimuuliza: “Vipi Aayah ambayo inasema:

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ  

Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote. [Al-An’aam (6: 103)]

 

Alijibu: “Ni wakati tu Allaah amezungukwa na Nuru, lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Rabb wake mara mbili. “Hadiyth hii ni dhaifu.”

 

Kwa hali hiyo kwa namna jinsi ilivyo hakuna mgongano wa kauli, na Allaah Anajua zaidi. [Sharh ya Uswuul Al-I’itiqaad cha Al-Laalika’iy, 93/512, As-Sunnah 1/181 na Swifat Al-Maqdisiy ukurasa 109-111].

 

 

Zawadi Ya Mi’raaj

 

‘Abdullaah bin Mas’uwd alisema, “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa vitu vitatu: alipewa Swalaah tano, alipewa Aayah mbili za kumalizia Suwrah ya Al-Baqarah na kusamehewa kwa madhambi ya wale watu ambao hawamshirikishi Allaah miongoni mwa ummah wake.” [Muslim Namba 329].

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Allaah Alinipa ufunuo na Akasema kuwa Ummah wangu wanawajibika kuswali Swalaah khamsini (50) kila siku; usiku na mchana. Nilishuka kwenda kwenye mbingu ya Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) akaniluza: “Lipi Rabb wako Amekupatia kwa ajili ya ummah wako?” Nikasema: “Swalaah Khamsini.”  Akasema: “Rejea kwa Rabb wako na omba Akupunguzie katika idadi hiyo ya Swalaah, maana watu wako hawawezi kubeba mzigo huo mzito. Kama vile nilivyotiwa katika mtihani na wana wa Israaiyl na nikawajaribu nikawaona kuwa walikuwa dhaifu sana na hawawezi kubeba mzigo kama huo.”  Hivyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimgeukia Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) kama vile akitaka kupata ushauri wake juu ya hilo. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema: “Ndiyo, sawa, kama unataka hivyo.” Na wakarejea tena juu kwa Allaah.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608].

 

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Nilirejea kwa Rabb wangu na kusema, “Ee Rabb wangu, Fanya vitu viwe vyepesi kwa ajili ya Ummah wangu. Allaah Alipunguza  idadi ya Swalaah khamsini na kuwa tano kwa ajili yangu. Nilishuka chini nikaenda kwa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) ambaye alisema: “Hakika watu wako hawataweza kubeba mzigo huu mzito. Rejea kwa Rabb wako umwombe afanye wepesi wa hilo, Ee Muhammad! Mimi nilijaribu kuwalingania Ummah wangu wana Israaiyl ili wafanye kidogo zaidi ya hayo, lakini hawakuweza kuyafanya hayo bali waliishia kukata tamaa.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608]. 

 

 

Basi nikawa natangatanga kati ya mbingu ya Muwsaa na kwa Rabb wangu mwisho Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akasema: “Kuna Swalaah tano kila siku, usiku na mchana Ee Muhammad. Kila Swalaah imebeba uzito wa Swalaah kumi, na hivyo hizo ni khamsini vile vile. Mtu yeyote anayetia niyyah ya kufanya jambo zuri na asipolifanya basi atapata thawabu kwa hilo, na kama atalifanya hilo tendo, basi itaandikwa thawabu kumi kwa hilo. Wakati ambapo mtu aliyenuia kufanya uovu na akaacha kuufanya haitasajiliwa hiyo na kama atafanya uovu huo basi utasajiliwa uovu mmoja tu. Hapo nikashuka kwa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) na kumwambia hayo, Muwsaa akasema: “Nenda kwa Rabb wako ili afanye mambo yawe mepesi zaidi.” Juu ya kauli hiyo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Nimekuwa nikienda kwa Rabb wangu mara kwa mara hadi naona aibu kusimama mbele yake. [Muslim].

 

Juu ya hilo Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema: ”Kwa jina la Allaah! Shuka sasa!”  Kisha Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaamka akiwa ndani ya Masjid Al-Haraam (Msikiti Mtukufu wa Makkah)” [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608]

 

Na pia ndani ya maelezo ya Al-Bukhaariy kuna maelezo zaidi kuwa: “…nilipoondoka nilisikia sauti:  “Nimetoa amri Yangu na kisha nimewapunguzia uzito Waja Wangu.”

 

 

Utukufu Na Umihumu Wa Swalaah:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameitukuza Swalaah na kuipa daraja kubwa sana kwa kuifaradhisha katika usiku wa Mi’raaj. Amri zote zingine zililetwa na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) ardhini kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Swalaah ilifaradhishwa baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuitwa kwenda mbinguni na mawasiliano yalikuwa ni moja kwa moja kutoka kwa Rabb hadi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aayah nyingi za Qur-aan na Hadiyth nyingi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinashuhudilia utukufu na umuhimu wa Swalaah.

 

 

Ibn Hajar anaandika katika sharh yake ya Al-Bukhaariy (1/460), “Hekima ya kufaradhishwa Swalaah wakati wa Mi’raaj ni kuwa hapo ndipo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopata utukufu kamili kwa nje na ndani ya mwili wake. Alikoshwa kwa maji ya Zam Zam na kisha akanyunyuziwa na iymaan na hekima. Kwa kuwa Swalaah imetanguliwa na wudhuu, ilikuwa hasa mahali pake maamrisho ya Swalaah yaletwe akiwa katika hali hiyo yaani baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutakaswa na kusafishwa.”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema: 

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ  

Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. [An-Nahl (16: 18)]

 

 

Kupunguzwa kwa idadi ya Swalaah ni neema kutoka kwa Allaah na kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema: 

وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾

  Na wachache miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru. [Sabaa (34: 13)]

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الْإِنسَانَ لِرَبِّهِ لَكَنُودٌ ﴿٦﴾

Hakika mwana Aadam kwa Rabb wake bila shaka ni mtovu wa shukurani.   [Al-‘Aadiyaat (100: 6)].

 

 

 

 

Je, kuna neema gani tukufu ziaidi ya hii kuwa Swalaah ambazo zilikuwa ni khamsini zimepunguzwa na kuwa tano kwa siku, usiku na mchana  na kisha malipo ya hizo Swalaah tano ni sawa na Swalaah khamsini zile za mwanzo?

 

Ibn Hibbaan anasema katika Swahiyh yake (1/133): Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaradhishiwa Swalaah khamsini, amri hii ilikuwa ni mtihani mkubwa, mtihani ambao alitaka kumpima nao kipenzi Wake Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wakati akimwambia kuwa Ummah wake wakaswali Swalaah khamsini alikuwa anajua fika kuwa wataswali Swalaah tano tu na amri ya kuswali Swalaah khamsini ilikuwa ni mtihani tu! Hii ni sawa na maneno yetu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaweza Akaamrisha kitu kwa mja Wake ambaye atapokea amri hiyo lakini si lazima aitekeleze kwa vitendo. Mfano mzuri wa hilo ni pale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipomwamuru Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) kumchinja mwanae mpenzi. Utashi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wa amri hii ilikuwa ni kuwa Amri Yake ipokelewe na ikubaliwe kikamilifu. Na pindi wote mzazi na mtoto waliposalimu amri na kujisalimisha kwa Rabb wao, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alitoa kafara ya mtoto huyo badala yake kwa kafara kubwa sana. Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Angelikuwa Anataka yatekelezwe yale aliyoyaamuru basi Ibraahiym angelikuta mtoto wake kachinjwa kweli. Hali kadhalika kutoa amri ya kuswali Swalaah khamsini kwa kila siku ilikuwa ni amri ya kukubaliwa lakini kitu kingine ambacho ni chepesi kwa matendo chenye uzito sawa sawa ndiyo kifanyike ambazo ni Swalaah tano.”

 

 

Yeyote anayedharau Swalaah, siyo kwamba kakataa nguzo ya Uislamu bali pia kakataa zawadi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Swalaah ni nguzo ya kwanza katika mpangilio aliowekewa mwana Aadam na ndio ‘ibaadah ya kwanza kuulizwa mja siku ya Qiyaamah na pia ilikuwa ni amri ya mwisho ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiitamka mpaka mwisho. Wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa katika maradhi yake ya mwisho alikuwa akisema: “Swalaah, Swalaah na vile ambavyo mikono yenu ya kuume inavimiliki.” [Hadiyth Swahiyh imesahihishwa na Imaam Al-Albaaniy, Ibn Maajah na Musnad ya Ahmad].

 

 

Mtu anapokufa hasemi ila maneno yale ambayo anayaona kuwa ni ya muhimu sana kwake na anapendelea watu wachukue ushauri wake wa mwisho. Hivyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru kwa maneno hayo ambayo aliyaona kuwa ni ya muhimu sana. “Tuchunge Swalaah.”

 

‘Abdullaah bin Qart alisema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Tendo la kwanza ambalo mja atawajibika nalo siku ya Qiyaamah ni Swalaah. Kama Swalaah yake itakuwa ni nzuri basi matendo mengine yote yatakuwa ni mazuri. Na kama Swalaah itakuwa ni mbaya basi matendo mengine nayo yatakuwa ni mabovu.” [At-Twabaraaniy].

 

Alisema Abuu Buraydah bn Al-Haasib: “Rasuli wa Allaah amesema: “Kitu ambacho kinatutofautisha Waumini na makafiri na wanafiki ni jinsi tulivyo karibu na Swalaah. Mtu asiyeswali anaangukia katika kundi la makafiri.”  [At-Tirmidhiy Namba 1083]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa watu wa motoni watatupwa katika moto wa Jahannam na wataulizwa: Kitu gani kimekusababisheni kuingia katika moto wa Jahannam? Nao watajibu:

 

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ﴿٣٨﴾

Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma.

إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ﴿٣٩﴾

Isipokuwa watu wa kuliani.

فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ﴿٤٠﴾

Katika Jannaat wanaulizana.

عَنِ الْمُجْرِمِينَ﴿٤١﴾

Kuhusu wahalifu.

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ﴿٤٢﴾

 (Watawauliza): “Nini kilichokuingizeni katika motoni?”

 

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ﴿٤٣﴾

Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali. [Al-Mudathir (74 :38-43)].

 

 

 

 Hivyo jambo la kwanza ambalo wataungama itakuwa: “Walikuwa wameacha Swalaah.”

 

Umuhimu wa Swalaah unaonekana katika Msikiti wa Qubaa. Msikiti huu ulijengwa wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipohama kutoka Makkah kwenda Madiynah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa sehemu za Qubaa siku nne kabla hajaingia mjini Madiynah, hakupanga kukaa Qubaa wala hakujenga chochote hapa. Kitu alichofanya hapa alijenga Msikiti wa Qubaa. Kitendo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujenga Msikiti hapa Qubaa kinaonesha umuhimu wa Msikiti katika Uislamu. Hivyo basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipeleka kikundi cha Maswahaba kwenda kupigana Jihaad. Aliwaambia waahirishe vita hivyo, waache kila kitu wakisubiri adhana. Anasema Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Daima mtu alipotoka nasi kwenda kupigana Jihaad dhidi ya watu wowote wale, hakuturuhusu kupigana hadi asubuhi na atasubiri kusikiliza kama kutatokea adhana. Akisikia adhana basi ataahirisha vita hivyo na kama hakusikia adhana basi aliamuru vita hivyo viendelee…”  [Al-Bukhaariy, Juzuu 1 Namba 584].

 

 

Ndugu Waislam, tusome tukio hili kwa mazingatio makubwa kwa kuyafanyia kazi mafunzo yanayopatikana ndani yake, na si kwa kusherehekea, kufunga na kutenga siku maalum ya kula, kuswali Swalaah za aina fulani na du’aa za namna fulani, kugawa vyakula na kufanya mikusanyiko ya masimulizi ya kuburudisha kama ambavyo imekuwa ni ada kwa baadhi ya watu, hayo yote hayajathibiti wala kufanywa na wema waliopita. Tuige matendo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na watangu wema na tutafanikiwa In Shaa Allaah.

 

 

Vitabu vya Rejea:

 

Tafsiyr ya Ibn Kathiyr

Swahiyh Al-Bukhaariy

Swahiyh Muslim

Sunan Abiy Daawuwd

Kitabu cha Siyrah Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm

Mihadhara juu ya Mi’raaj ya Ihsaan Ilaahi Dhwahiyr.

 

 

Wa biLLaahi At-Atawfiyq

 

 

 

 

Share