Hijrah: Chanzo Cha Mageuzi
Hijrah: Chanzo Cha Mageuzi
Allaah Amejaalia njia ya haki kuwa na ishara za wazi. Na Akajaalia kufikiwa katika lengo linalohitajika kwa juhudi na kujitolea. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ ۚ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ ۖ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ ۚ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّـهِ ۚ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١١١﴾
Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba watapata Jannah. Wanapigana katika njia ya Allaah, wanaua na wanauawa. Hii ni ahadi ya haki Aliyojiwekea katika Tawraat na Injiyl na Qur-aan. Na nani atimizae zaidi ahadi yake kuliko Allaah? Basi furahieni kwa biashara yenu mliyofungamana Naye. Na huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah:111]
Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alibeba bendera ya ushujaa mpaka ikawa ni yenye kunyanyuka katika kila sehemu ya pembe ya ulimwengu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa miaka 13 Makkah baada ya kupewa utume akiilingania kaumu yake katika Uislamu. Hakika alibughudhiwa, kuudhiwa na kukadhibishwa Da‘awah yake. Mbali na hayo walikuwa wanajua ukweli na uaminifu wake mpaka wakawa wanamuita As-Swaadiqul Amiyn (Mkweli Muaminifu).
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake walivumilia maudhi yao yote, adhabu na mateso. Katika mwezi wa Muharram Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliashiria kwa Swahaba zake kuhamia Madinah. Wakatoka wote isipokuwa wale waliokuwa na haja zao katika mji wa Makkah au walioshikwa na kufungwa kwa nguvu na makafiri.
Sababu ya Hijrah, ni pale Ma-Quraysh waliposhindwa kumkinaisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuacha Da‘awah yake na kuendelea kwake kumuabudu Allaah tu. Hivyo, walifikiria ima kumfunga au kumuua au kumtoa katika mji lakini uamuzi uliochukuliwa ulikuwa ni kumuua kabisa. Walichagua vijana wenye nguvu kutoka kila ukoo ili kutekeleza mkakati wao huo. Vitimbi vyao hivyo vilifichuliwa na Mwenye habari na Mjuzi, naye alitoka mbele ya vijana bila kuonekana na hao vijana waliokuwa wamekaa nje ya nyumba yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ ۚ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ ۖ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ﴿٣٠﴾
Na pindi (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) walipokupangia makri wale waliokufuru ili wakufunge, au wakuue, au wakutoe (Makkah). Na wanapanga makri, na Allaah Anapanga makri (kupindua njama zao), na Allaah ni Mbora wa wenye kupanga makri.[Al-Anfaal: 30]
Walifika kwenye pango na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akawalinda na maadui hao ambao walikuja mpaka kwenye mdomo wa pango la Thawr. Abubakar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipowaona makafiri wakiwa nje ya pango alisema: “Lau mmoja wao ataangalia chini ya miguu yake basi atatuona”. Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa utulivu na bila wasiwasi alimwambia: “Ee Abu Bakr! Dhana yako ni ipi kwa wawili ambao watatu wao ni Allaah” [Al-Bukhaariy na Muslim]. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Analizungumzia tukio hilo kwa kusema:
إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٤٠﴾
Msipomnusuru (Rasuli), basi Allaah Amekwishamnusuru, pale walipomtoa (Makkah) wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili; walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi. Basi Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona, na Akajaalia neno la waliokufuru kuwa chini. Na Neno la Allaah kuwa ndilo lililo juu. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 40].
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliwaokoa wao wawili na vitimbi vya mushrikina. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ataendelea Kuwahami na Kuwalinda walinganiaji wa haki mpaka Siku ya Qiyaamah.
Na hapo makafiri wakatoa zawadi ya ngamia mia moja (100) kwa atakaye wapata hai au maiti. Na hii hii ndiyo mbinu ambayo inatumiwa na makafiri wa sasa wanavyofanya wakati wanawatafuta watu. Na ndio wanazuoni wetu wakasema: “Ukafiri mila yao ni moja”.
‘Umar ibn al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) baada ya kushauriana na Swahaba waliokuwa hai wakati wa Ukhalifa wake waliamua kuanza tarehe ya Kiislamu kwa tukio hilo, kwani ndio ilokuwa chanzo cha ushindi na kubadilisha historia yote. Hapo wakawa Waislamu Mashariki ya ardhi na Magharibi yake wanafahamu kabisa kwa uhakika kuwa ni Hijrah ndiyo iliyoharakisha mapambano na kujitolea mhanga. Lakini ni masikitiko kuwa hatufahamu umuhimu wa tukio hilo isipokuwa ni msimu wa kidini ambapo tunakariri matukio ya kimada ya Hijrah na jinsi alivyohama Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake na walivyopokewa kwa ukarimu Madinah na kula pilau kumaliza kabisa shughuli yenyewe
Ama mazingatio, maana matukufu makuu huwa mara nyingi hatuyataji sana na tukiyataja basi hayafiki kooni. Hakika, Hijrah ina mambo mawili: Zingatio la kimada na la kiroho.
1. Zingatio la kimada: Hii inaanza wakati alipotoka Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Makkah na kurudi kwake akiwa mshindi, huku akinyanyua bendera ya Tawhiyd na kuvunja masanamu. Na faida hii tunaiona mpaka wakati wetu huu wa sasa ambapo watu wanaingia katika Uislamu bila hesabu.
2. Zingatio la kiroho: Hii ni matokeo ya mapinduzi makubwa katika nafsi ya Muislamu na Ummah kwa ujumla wake kwa kufanya Da‘awah, na kutoka katika giza la ujinga na shirki kuelekea katika nuru ya elimu na Imani. Hijra inatufundisha kuacha maovu na riyaa na kujitwika tabia ya ukweli na uwazi na kupeana nasaha na kuifanya ndio msingi wa mahusiano yetu na watu wote – viongozi na raia bila kuogopa. Aliingia wakati mmoja ‘Amr ibn ‘Ubaydah kwa Khaliyfah wa Bani ‘Abbaas, al-Mansuur na akamsomea aya ifuatayo:
إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ
Hakika Rabb wako bila shaka Yu tayari Awavizia. [Al-Fajr: 14].
Khaliyfah akasema: “Onyo hili ni kwa nani, ewe Abu ‘Ubaydah?
Akamjibu bila khofu: “Hakika ni kwa wale wanaofanya mfano unayofanya wewe. Mche Allaah, ewe Amiri wa Waumini! Hakika katika mlango wako upo moto unaowaka, haufuati Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wala Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nawe una jukumu na utaulizwa kwa unayoyafanya na wala sio wanayoyafanya. Hivyo, usitengeneze dunia yao kwa kuiharibu Akhera yako. Ama Wa-Allaahi lau wafanyakazi wako wangejua kuwa huridhiki ila uadilifu wangekuja karibu nawe. Ee Amiri wa Waumini! Hakika watu wamekuchukua kama ngazi, wewe ndiye mshikaji pembe na wengine ndio wenye kukama maziwa. Hawa hawatakunufaisha chochote kwa Allaah. nami nakunasihi ewe Amiri wa Waumini, hakika wamelaaniwa Bani Israili kwa ulimi wa Dawuud na ‘Iysa kwani wao walikuwa:
كَانُوا لَا يَتَنَاهَوْنَ عَن مُّنكَرٍ فَعَلُوهُ ۚ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿٧٩﴾
Walikuwa hawakatazani munkari waliyofanya. Uovu ulioje waliyokuwa wakiyafanya. [Al-Maaidah: 79]
Hijrah inatakiwa ibadilishe maadili yetu – ya mtu na jamaa, na inatakiwa itutoe katika usingizi na iwe nukta ya kuanzia, hapo ndio tutaanza ili kutengeneza jamii nzuri zaidi na yenye ufanisi wa nyumba zote mbili (duniani na Akhera). Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anahama aliomba kwa kusema: “Ee Rabb wangu! Hakika Wewe Unajua kuwa wao (yaani makafiri) wamenitoa katika mji ninaoupenda zaidi, hivyo nipatie maskani katika mji Unaopendwa zaidi na Wewe”
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atubariki, Aturehemu na Atupatie fanaka katika mwaka huu wa Hijri. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atupatie hima ya kurudi katika misimamo ya sawa na njia ya sawa inayompendeza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na kufuata mwenendo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). In shaa Allaah sote tuwe na azma ya kikweli kweli ya kubadilika na tutie bidii katika hilo na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atatusaidia katika hilo. Kwani Amesema:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ
Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. [Ar-Ra’d: 11]